Thursday, January 19, 2012

Tuesday, January 10, 2012

BAHASHA YA KAKI

Elimu yangu ndani ya bahasha ya kaki


Wahenga walisema kinachozunguka mwishowe hurudi kinapotoka.Nimezunguka kila ninapoenda mwishowe nikajikuta narudi nyumbani sababu ndipo nilipotoka. Miguu,kichwa vinaniuma na mwili mzima umechoka kwa kutafuta kisicho machoni mwangu, kwa kutafuta bahati nisiyoijua kwamba itakuja lini, japo nimejawa na matumaini kwamba siku yangu itafika, wapo walionitangulia nawapa pongezi zao, wapo walio kwenye machakato kama wangu hao nawapa pole zao kwakua najua maumivu ya namna jua linavyoutendea haki utosi. Sasa ngoja nirudi nilipotoka, bahasha ya kaki imeshalowa jasho la uchungu, jasho lisilo na tumaini ya shilingi, narudi nyumbani nichukue bahasha nyingine mpaka kieleweke. Kwakua tumaini langu liko kwenye hii bahasha ya kaki, natumai utaisoma na kielewa imebeba nini ndani yake. Usiipite wala usiiweke pembeni. Hili ndilo  tumaini langu kwakua sijafundishwa mfumo wa nenda shule kisha tengeneza shilingi.

Ingawa tupo kwenye mwanga lakini kiza kimetanda na shilingi ndio imeshadondoka. Milango ya soko iko huru, mwenye macho sasa hawezi kutazama shilingi ilipo, kinachohitajika ni fikra za kuona zaidi ya macho. Wapo watakaojitoa kwenye mchakato huu kwa kukata tamaa kwakau kiza ni kinene, wapo watakaoupita mchakato huu kwa kupapasa chini mpaka shilingi itakapopatikana, wapo watakao saidiwa kwa kupewa tochi kutafuta shillingi ilipo, na tupo tutakaoisakanya shilingi hii gizani mpaka mwanga wa jua utakapowaka kwa matumaini kwamba ipo siku shilingi itapatikana.
          
            Tazama maisha yamekua kama mchezo, tena mchezo wakuigiza, na chakushangaza zaidi mwongozaji nae amekua muigizaji. Kumbuka ya kwamba kwenye mchezo wowote mbinu mbalimbali hutumika alimradi mchezo ukamilike, haitajalisha zimetumika mbinu halali ama zisizo za halali, kwakua halali imeshapotezwa na wasiopenda halali. Asiyekubali sasa anashirikiana na anayekubali, anayepinga amekubaliana na anayempinga. Hakuna mpiganaji tena wote wamefanywa sawa na uwazi na ukweli, wote wanapigania maisha bora ya nafsi zao kwa maigizo. Ukiongea sana unaitwa mropokaji, ukinyamaza unaitwa mwoga usiyejua chakufanya. Ukifanya kwa vitendo unaitwa mkorofi usiyependa amani, ukiandika maandishi unaitwa mchochezi. Chochote kinasemwa popote kupoteza uhalisia wa jambo husika. Matokeo yake tumeamua kukaa kimya kwakua ni waoga wa kuogopa uoga wetu.
         
          Aliyepewa tochi tayari keshaiona shilingi, aliyeikosa tochi bado anagangamala kuitafuta shilingi ilipo kwa matumaini ipo siku itapatikana. Tazama watoto wa wakulima mikononi mwao utawaona wakipita na bahasha za kaki, sehemu ya kushikia bahasha imekua nyeusi kwa mafuta na jasho la mkononi. Jasho linamtoka na kukauka, leso imelowa, kiatu kimejaa vumbi, ametoka nyumabani msafi sasa anarudi kama ametoka shambani. Ni mtoto wa mkulima aliyekulia kwa sera za “ndio uti wa mgongo wanchi yetu”. Hana ndugu wakumpa tochi, baba yake hana rafiki wakumwangazia njia yakupata shilingi, jua ni lake vumbi ni yake. Amekua kijemedari kwa mfumo wa nenda shule tafuta shilingi, hajui mfumo wa nenda shule tengeneza njia za shilingi.

          Bahasha ya kaki mkononi mwake, anatafuta kisicho kwenye mamlaka yake. Bahasha ndani kuna bahasha anashawishi apewe kisicho machoni na mikononi mwake. Hana chake, haijui kesho yake, anachojua ni bahasha ya kaki iliyojaa vyeti vyake, elimu yake ndani ya bahasha, tumaini lake ndani ya bahasha. Bahasha inayopitia mikononi mwa watu na viatu. Bahasha mpya ya kaki inayomleta tumaini kwamba kila mtu ana siku yake kijana. Hapo ndipo nilipoigundua tofauti ya akili na bahati. Nilizoea kusikia “kana akili haka kajamaa, kamefaulu mitihani yake yote”. Mara unasikia “kana bahati haka kajamaa kameshapata shilingi yake”. Sasa yupi mwenye bahati na yupi mwenye akili? Au mwenye bahati hana akili na mwenye akili hana bahati ? Au akili na bahati ni sawa? Kipi sasa ni cha muhimu akili au bahati mbele ya bahasha ya kaki ya kumulikiwa kwa tochi penye kiza kinene?..kumkichwa ni wewe!