Showing posts with label Uzalendo. Show all posts
Showing posts with label Uzalendo. Show all posts

Thursday, May 17, 2012

"JE Ni WAPi TULiKOSEA?"

Je! ni wapi tulikosea?

Tulisali dhambi zilipozidi, ukame ukapotea,
baraka za mvua zilipozidi, mafuriko yakatokea,
maisha yakapotea, Je! ni wapi tulikosea?

Tukajenga kwenye miinuko, wakasema tumekosea,

kila mahali tulipo, alama ya x imekolea,
maisha yanapotea, Je! ni wapi tulikosea?

Pazuri ndio kwao,
kicheko kirefu wameotea,
kwetu mabondeni vilio, jamani huku tunaelea,
maisha yanapotea, Je! wapi tumekosea?

Utawasikia hameni mabondeni, kukaa huko mnakosea,

Mara unasikia kaposho haka kadogo jamani, sio vibaya tukikaongezea,
maisha yakapotea, Je! ni wapi tulikosea?

Nakosea bure bila senti, natupwa Jela nikafundishwe,

wamekwapua fuko la vijisent, wanaunda Tume wasafishwe,
maisha yakapotea, Je! ni wapi tumekosea?

Japo hasira zetu ni kali, misaada yenu tutaipokea,

nyie mpini sie makali, sauti ya vuta ikitokea,
maisha yatapotea, Je! ni wapi tutakosea?

Bora maisha niyaonayo, kuliko
maisha bora ya ndoto
Za mjomba kama Mpoto, za kudanganywa kama toto,
ninaposema tena kumkichwa ni wewe! Je! utasema nimekosea?


by Abeid Kajia on Thursday, December 29, 2011 at 9:11am ·

Wednesday, March 14, 2012

"Siku Maji yakirudi nyuma"






Litakua  ni jambo la kushangaza pengine na kutupumbaza kuona siku hiyo... kivipi maji yamerudi nyuma badala ya kwenda mbele!..., ni mshangao ambao utatufanya wengi wetu tustaajabu ya kuwa ni kivipi maji haya yamerudi nyuma! Tutabaki tukijiuliza kwakua tumekua ni wagumu kuelewa kwamba maji yanaweza yakarudi kama mambo hayatakwenda namna yanavyotakiwa yaende au kama tutaendela na mfumo wetu wakuacha mambo yaende kama wanavyotaka na sio kama tunavyotaka sisi yaende kwa kujishirikisha kwenye shughuli za kila siku za ujenzi wa taifa letu. 


Tukiwa kama watazamaji wa mambo yanavyoenda kila kukicha bila kuwa watendaji na washiriki katika kufanikisha mambo yaende vile sisi tunataka, hatuna budi kukubalia na hali itakavyokuja kubadilika kwa kushuhudia maji yanayotoka katika Ziwa letu la Victoria yenye Upendo na Amani ya miaka hamsini kisha kupita katika Mto Naili yakiwa yanasambaza Upendo na Amani kwa nchi za Sudan, Libya, Somali na Misri na kisha kumwagika katika bahari ya Sham yakirudi na chuki, vurugu, vita, mageuzi kutoka nchi ya Misri, Libya, Somalia na Sudani na kurudi nchini kwetu na kusambaza ari hizo kwa wananchi wetu wenye amani na upendo, kwa kusahau kwetu misingi iliyotujengea na kutupa Amani na Upendo kwa miaka hamsini tukiwa huru kwa kujitawala.


Tumeshuhudia yaliyotokea Misri, tumekuwa wazungumzaji wazuri kwa yaliyotoka Libya, tumewahurumia na kushuhudia mgawanyiko uliotokea Sudani. Sasa kwa haya yaliyotokea katika nchi hizi hata nchini kwetu yanaweza yakatokea muda wowote na saa yoyote. Lakini itakuwa hivyo kama tutakuwa wagumu kutambua ni wapi panapokwenda tofauti na namna panavyotakiwa paende.


Kwa namna gani tunatakiwa tuwajibike vilivyo katika shughuli zinazotuhusu.Tusiishie kuwa watazamaji na wasemaji, eti kwakua kuna watu tumewateua wasimamie shughuli zetu basi sisi tukalale tusubiri watufanyie kila kitu , tabia hii itatuletea lawama juu yao na sio juu yetu kwakua hakuna anayetaka kubeba mzigo wa miiba alioujaza yeye mwenyewe. Huyu kakosea yule kamsema, yule aliyesemwa nae kaamua kusema mabaya ya mwenzake. Huyu anakataa kujiuzulu kwakua anapenda madaraka, amekosea lakini hataki kuwajibika kwakua anapenda madaraka. Maji yakirudi nyuma vipi atatulaumu kwanini yamerudi nyuma wakati yeye hataki kuwajibika!.


Tazama wanasema chochote ili vyombo vya habari vipate chakuandika, tazama namna vyombo vya habari vimeteka vichwa vya watu. Kinachoongelewa jioni ya leo kesho utakikuta kwenye kichwa cha habari. Maigizo ya wasanii wasiopenda jina la wasanii. Wanachezea matope kisha wanajisafisha kwa maji yenye matope na kujiita wasafi. Siku maji yakirudi nyuma watatuuliza nani ni mchafu.


Wanachukua kisicho halali kwa njia zisizohalali kwa kuihalalisha kua ni halali. Tazama yatima analia mpaka machozi yanakauka hana wakumdekea, kilicho halali yake kimehalalishwa tumboni kwa walaji, hana chake, aliyetoa katoa kwa asiyenacho, kapokea mwakilishi wake na kimeliwa na mwakilshi wake kwa kujaza tumbo lake, yatima hana chake, anatamani maji yarudi nyuma. Hali ibadilike apate chake, chozi lake thamani yake kwake kwani linampunguzia huzuni iliyomo ndani ya moyo wake. Bora limtoke apate faraja yake kwani baada ya chozi la mwisho kufutika ana imani furaha itajitokeza.


Najiuliza Siku Maji yakirudi nyuma sijui hali itabadilika, aliye na uwezo wa kuona mbali kwa jicho la tatu, ajaribu kutazama aone namna maji yatakavyorudi nyuma. Ukisoma makala hii kwa makini utanielewa kwanini nawasihi tuombe sana maji yasije yakarudi nyuma. Tazama namna umasikini wetu unavyoujenga utajiri wao, mwerevu atanielewa tofauti na hapo sintowashangaa sana mkinipinga, kwani mi husema niyaonayo. Ukibishana na mjinga atakushinda kwa ujinga, na wewe utakua mjinga mkubwa mbele ya mjinga, ni ujinga kuogopa kifo cha kuku wakati ndio kitoweo ulichonacho, narudia tena matatizo yetu ndio mtaji wao.


Tunapokosa matumaini wao hutupa faraja kwa “mkinichagua mimi nitatatua shida zenu, nawahakikishia kua thamani ya shilingi itapanda, nitawajengea barabara, shule, hospitali, visima vya maji nchi yetu itakua na maendeleo na itapiga hatua kubwa kiuchumi duniani. Miaka inakwenda anashika hatamu, miaka inakwenda awamu inakwisha, hajafanya kitu anarudi tena na matumaini mengine na ahadi nyingine nyingi, akimaliza amamu zake mwingine anapokea kijiti, anaendelea kukikimbiza kwa ahadi zisizotekelezeka na zilizotelekezwa. Sisi tumebakia kulalama kwa maneno makali bila yakujua kesho yetu itakuaje. Tuombeeni maji yasije yakarudi nyuma sababu itakua ni vilio juu ya kilio.


Tuombe usifike wakati ujasiri ukaushinda uoga, kwani kifo kitakua ushujaa na uhai utabakia aibu, wananchi watakapoona fahari ya kupoteza walichokuanacho kwa ujasiri wakupigania wasichokuanacho. Hawatasikia la mwadhini wala la mnadi swala, vijana watakapopita mbele kwa ujasiri wakutaka kumvisha paka kengele. Tuombee maji yasije yakarudi nyuma.


Wengi wameniuliza mbona kila siku wewe huongea tu matatizo bila kutoa suluhisho la matatizo. Ni kwamba shida zetu zinaletwa na matatizo na matatizo yanaletwa na sisi wenyewe kwakua tumekua wagumu wa kuelewa na wakuona ukweli na kuchukua hatua. Tunatatua shida na kuacha tatizo, bila kujua tatizo ni vigumu kwetu sisi kumaliza matatizo yetu. Mfano vijana wanashida ya kupata ajira kwakua kuna tatizo katika mfumo mzima wa ajira kwa vijana, sasa badala ya kuubadilisha mfumo mzima ambao ndio tatizo, tunatatua shida ya ajira kwa kuwapa baadhi ya vijana ajira na kujivunia kua ukosefu wa ajira umepungua.

Nimendika nilichokiona na kinachokuja mbele yetu kama hatakua mstari wa mbele katika kubadilisha mfumo nyonyevu unaotunyonya fikra zetu hai kwa kutuosha kwa starehe zisizo na umuhimu katika maisha yetu ya sasa na ya baadae. Tumetekwa na vyombo vya habari kwakua hatutaki kuchanganya akili zetu na tulichokisikia na tulichoambiwa ama tulichokiona. Mbayuwayu alitaka kua na mdomo uliochongoka, aliambiwa ili uwe mzuri basi aende juu kisha ashuke chini na augonge mdomo wake kwenye jiwe, akafanya kama alivyoshauriwa ila alipokaribia jiwe lile akasema “AKILI KUMKICHWA” nisije ni kafa bure, akaokoka kifo kwa kusikia alichoambiwa na kuchanganya na akili yake, je wewe unachanganya akili yako na ulichoambiwa au unaenda tu kwa amri ya mwenye cheo?, siku maji yakirudi nyuma utanikumbuka kwa kusema kumkichwa ni mimi… ila mimi sintochoka kukukumbusha ya kua KUMKiCHWA NI WEWE!

  

Wednesday, September 7, 2011

“MiWANi YA BABU”

                Mwanzoni mwa miaka ya nyuma hali ilikua tete katika kijiji chetu na kupelekea babu kufanya mabadiliko makubwa katika mfumo wakuendesha kaya na koo zote, babu yetu ndiye aliyekua mkuu wa kaya zote, yeye ndiye aliyepewa mamlaka ya kuongoza kaya zote katika kijiji chetu kwakua alikua na ujuzi na alipata miwani iliyomuezesha yeye kuona na kuweza kuongoza kaya zote. Wakati babu anakabidhiwa uongozi wa kijiji chetu kulifanyika tambiko kubwa katika moja ya kaya za vijiji vyetu, kaya ambayo babu alipendekeza iwe makao makuu ya kijiji chetu, na kaya nyingine alitaka iwe ya kufanyia biashara. Chakushangaza mpaka leo kaya hiyo bado haijafanywa makao makuu ya kijiji wakati shughuli nyingi za kijiji zikipelekwa kwenye kaya ya kibiashara, hii inaonesha ni kwa namna gani ushauri uliotolewa na babu kwa kutumia miwani yake unavyopuuziwa.

              Tokea babu alipofariki kijiji chetu kimekua kikiyumba sana, kwa kua tokea mwanzo hata wakati wa uwepo wa babu tulikua hatuna msingi imara wakuweza kukiendesha kijiji chetu pasipo kutegemea wageni kutoka vijiji vya nje. Hii ilitokana na shinikizo alilolipata babu la kuondolewa madarakani, ambayo ilimlazimu babu kuachia uongozi wakijiji baada ya kuona shinikizo linazidi juu ya mfumo aliouchagua kua ndio utakaofaa kuendesha kijiji chetu. Wakati babu anafariki aliniachia miwani yake, aliniambia mjukuu wangu miwani hii kama utaitumia vizuri basi itakusaidia kuona pale wanapoficha, utawanona pale watakapodanganya, na utawaona wale wasiotaka kufuata misingi tulioinanzisha, na utawaona wasaliti watakaokisaliti kijiji chetu, ila kwakua mjukuu wangu miwani hii ni ufunguo wa maisha yenu, yako na kizazi cha baadae, nakusihi miwani hii iwe msingi wa kukukomboa wewe na kizazi chako, kisha na nyinyi kwa pamoja muwakomboe na wenzenu dhidi ya ubaghili na ubinafsi wa nafsi utakaoingia katika kijiji chetu, kwani kuondoka kwangu najua mengi yatabadilika na nimeshawaona wengi mafisi wakikitamani hiki kijiji chetu ila miwani hii ndio ukombozi wenu, naomba muitumie kwa malengo ya kuleta mabadiliko chanya katika jamii ya kijiji chetu.

             Sasa ni miaka mingi imepita tokea kuondoka kwa babu yetu na jemedari aliyelisongesha gurudumu la maendeleo katika kijiji chetu na kuondoka kwake ni kweli mengi yamebadilika, ila kwa kutumia miwani ya babu nimeona mambo mengi yanavyopelekwa ndivyo sivyo, kama babu alivyonisisitizia ya kwamba "kuondoka kwangu mjukuu wangu kwa kutumia miwani yangu utaona mengi yatakavyopelekwa ndivyo sivyo"

             Tazama yanayofanywa na wasomi wa kijiji chetu, wameshasahau ya kwamba mategemeo ya wanajamii kwa wasomi ni mabadiliko kutokana na kisomo walichokipata, na sio uharibifu kwa kisomo walichopata. Nakumbuka babu alisema “msomi asisahau jembe, jembe ndilo limempa uwezo wa kuishika kalamu”, lakini kwa miwani ya babu leo namuona msomi analitupa jembe lililompa akili namna ya kushika kalamu. Wasomi wamekua ni watu wasiotaka kuleta maendeleo chanya bali wametuleta uhasi na uhasama ndani ya kujiji chetu. Wamekua ni watu wenye tamaa na wasio na nia nzuri na kijiji chetu. Imefikia mpaka wanakijiji wamepoteza imani na wasomi wa kijiji chetu kutokana na tamaa zao za madaraka, maisha mazuri, kujilimbikizia mali huku wakiwaacha wanakijiji wetu katika kipindi kigumu sana kwani hali ya maisha ya sasa ni tofauti na kupindi alichokuwapo babu.

             Miwani ya babu imeona kuwa amani tuliyonayo katika kijiji chetu sio amani kama mioyoni mwetu tuna malalamiko juu ya mfumo wa maisha ya sasa yalivyo na hatuna pakuyapeleka, kwani kwa kutumia miwani ya babu nimeona ya kwamba “amani ni maandalizi ya vita vingine”, na wakati wa vita hivyo tutajaribu kutafuta amani ya kweli ila nayo tutaitumia kuanzisha tena vita nyingine, amani tutakayoipata ni kupumzika kwa amani kwa matumaini ya kupata amani. Babu alisisitiza kuwa kama tunataka tuwe na kijiji cha amani basi yatupasa kuacha chokochoko za kutaka kuvunja muunganiko wa kijiji chetu, tusizungumzie sana kuvunjika kwetu kwamba ndio kutakua chanzo cha maendeleo. Miwani ya babu hapa inaona ubinafsi katika pande moja kwamba kuunganika kwa kijiji chetu na chao ndio chanzo cha maendeleo yao kurudi nyuma. Ila kama wangelijua umuhimu wa muunganiko wa kijiji chetu na chao basi wasingechokoa kuitafuta vita wakati tuko katika kuitafuta amani ya kunyanyasika kisaokolojia na kifikra. Na hii miwani ya babu haitaacha kamwe kuona na kuongea kwakua hatuna imani na amani tuliyopewa na viongozi wa kijiji chetu. 

Nakumbuka babu alituambia tusiuguse mbuyu ule mpaka tutakapopata wataalamu wa kuvuna mabuyu ya mti ule, sasa hali imebadikika tokea kuondoka kwa babu, wageni wengi toka vijiji vya nje wanamaliza mabuyu na kutuachia mibuyu mitupu. Miwani ya babu imeona usaliti wa viongozi wa kijiji chetu ambao babu aliniambaia kwa kutumia miwani hii utawona wasaliti. Kijiji chetu kimejaa wasaliti kwakua hakuna aliye na uzalendo, uamninifu, anayewajibika, anayesimamia haki. Kupotea kwa misingi hii kunasababisha viongozi wa kijiji chetu wenye tamaa kulipeleka ndivyo sivyo gurudumu la maendeleo ya kujiji chetu. Mibuyu yote wamewaachiwa wageni eti wao ndio wanautaalamu wakuyavuna mabuyu hayo, ila sisi tutapata faida kwa kuwakatoza ushuru na kwa kupata gawiwo kwa mavuno hayo. Kwa kweli mimi nimeshindwa kuwaelewa viongozi wa kijiji chetu. Yaani wanawaachia wageni wamumunye utamu wote wa mabuyu, kisha sisi watuachie matetere ya ubuyu, hivi tunakipeleka wapi kijiji hiki?.

Babu alituhimiza kua kijiji chetu kisiwe na utengano wa koo, tusijitambue kwa koo wala tusiendekeze ubinafsi wa koo. Ila kwakutumia miwani ya babu naona ubinafsi wa koo umeingia katika kijiji chetu. Hii inajitokeza kwa baaadhi ya koo fulani kuweka ubinafsi kwa tamaa ya kujiletea maendeleo wao kwa wao, na ilidhihirika wakati wa kumchagua viongozi wapya wa kijiji chetu, kwani ukoo wa babu ndio unaoongoza kijiji  chetu tokea kuwepo kwa babu hadi sasa. Imefikia kipindi maendeleo yanagawanywa kwa kuangalia ukoo, hali hii inaleta uhasama ndani ya kijiji chetu kwani ndio moja ya amani amabayo sio amani bali maandalizi ya vita vingine. Ingawa babu alisema “vita vikali vitatokea ndani ya ukoo wangu na vitazidi vita kati ya ukoo wangu na ukoo mwingine” kwa tamaa ya madaraka iliyowatawala viongozi wa kijiji chetu na hali ya malalamiko ya wanakijiji ilivyo sasa, panaweza pakazuka vita kali sana.  Na kwakua kijiji chetu hakijawahi kuingia katika vita kati ya ukoo na ukoo, hali itakua mbaya sana kwani hatujui ni kwa namna gani tutaweza kuimaliza vita hiyo na kufikia  muafaka.  Miwani ya babu pia imeoma ubinafsi wa viongozi wa kijiji chetu kutaka kuwatumia vijana na wanakijji kama ngao yao wakati wa wamapigano yao. Wamekua ni watu wa kuwajaza vijana uongo ili vijana waone kwamba wanapigania haki kumbe hakuna chochote wanachopigania bali matakwa na tamaa za madaraka ya viongozi.

Ndio maana Babu alitushauri kwamba tusome kwa bidii ili tuwe na ufahamu wa mambo, kwamba tuwe na malengo na tunavyovitafuta. Alituambia malengo ya elimu tunayopata ni kutuwezesha kukabiliana na mazingira yetu yanayotuzunguka. Alisema kipimo kizuri cha akili tuliyonayo ni namna utakavyoikabiliana na hali itakavyotujia au mazingira yatakavyokujia  katika kipindi ambacho haujajiandaa au haukuifahamu. Na kwa kutumia miwani hii ya babu, maneno  haya aliyoyanena mwishoni ndio miwani ya babu aliyonipa kuweza kuchambua hali ilivyokua, ilivyo na itakavyokua. Hivyo nakushauri kijana mwenzangu, tumia miwani hii ya babu kutambua ni miwani gani ya babu aliyotuachia. Ukishaitambua miwani hiyo basi ukae chini na kuangalia wapi ulipotoka, wapi ulipo na ni wapi unapoelekea. Usikubali kupelekwa  pelekwa tu na mfumo nyonyevu kama bendera mbele ya upepo. Kama kijana wa kileo unatakiwa ujue nini kinaendelea katika dunia yetu na wapi kijiji chetu kilipo, na kwa namna gani unaweza kushiriki kama kijana kusongesha mbele gurudumu la mendeleo. Tambua kijana kwamba hakuna kisicho na umuhimu kilicho hai {chenye kuishi}, hivyo uwepo wako unamaana kubwa sana kama utatambua kwamba uwepo wako una maana kubwa. Ndio maana sintochoka kukuambia na kukukumbusha ya kwamba umoja wetu ndio nguvu yetu, tukijiunga mimi na mimi tunapata sisi. Kumbuka kumkichwa ni wewe!