Tuesday, October 9, 2012

DUNIA RANGI RANGILE ( 5 ) Sehemu ya Tano




                                           Na Lasima Nassoro
wiki iliyopita...Moris anasafiri kwenda Visiwa vya Anjuani kupeleka mzigo ingawa haujulikani ni mzigo gani bado ?..je Moris atafanikiwa?...je nini kitamtokea Moris?.... endelea kufatilia hadithi hii?...

      "wewe hapana wasiwasi, mimi kwisha ongea na bana Abdilah, amesema utakuta kijana wake akikusubiria kaskazini mwa ufukwe".

Teresia alipofika kijijini kwao, baada ya kusalimiana na mama yake na baba yake, akawauliza,
"ba mkubwa na ma mkubwa, hawajambo?".
Mama yake akamjibu, "Mzee Sosongo hali yake sio nzuri ila mkewe ye hajambo".
"kwani hali yake, ikoje?, anaumwa?".
"ndio, anaumwa sana, kama ungejua, ungekuja na Kibe ili amuone baba yake".
Kesho yake asubuhi,Teresia alikwenda kwa Mzee Sosongo kumjulia hali. Alipofika alimfikia mama Kibe akifagia uwanja.
"hodi mama",alisema Teresia.
"Teresia huyo, karibu mwanangu".
"shikamoo mama"
"marahaba mwanangu, habari huko mjini kwenu?".
"huko twashukuru, maisha yanaendelea, sijui nyie hapa".
"hapa ni hivyo hivyo, hauchi hauchi, unakucha".
"poleni sana, nimeambiwa baba anaumwa".
"hatujapoa maana kadiri siku zinavosonga hali inazidi kuwa mbaya, nikupokee ulivyobeba kama nivya kwetu".
"nivyakwenu, zawadi toka kwa Kibe".
"alifanikiwa kupata kazi?, na anaendeleaje na maisha ya mjini?".
"kazi alipata na ameshayazoea japo yupo mbali kidogo na ninapoishi".
"kuwa mbali au karibu na wewe si tatizo, muhimu ni kuwa amepata kazi, nisamehe mwanangu tumekuwa tu tunaongelea hapa bila kukukarisha ndani, karibu ndani mwanangu".
"asante, baba yupo wapi nikamsalimu?".
"yupo hapo chumbani, ingia tu maana sidhani kama amelala". Teresia akaenda chumba alichokuwepo Mzee Sosongo, akabisha hodi lakini hakujibiwa. Alikuwa akimsikia Mzee akikohoa, akaamua asukume mlango na kuingia. Mzee Sosongo alikuwa amejifunika blanketi, Teresia alipomuona Mzee Sosongo alivyo dhoofu, machozi yakaanza kumtoka, akamsogelea pale alipokuwa amejilaza.
Huku machozi yakimtoka akamuita, "baba, baba, baba". Mzee Sosongo akakohoa kitambo kidogo kisha akasema kwa sauti ya uchovu,
"we - we ,u  - na i - twa na - ni?".
Huku akilia kwa kwikwi, akapenga kisha akasema," naitwa Teresia baba, umenisahau?".
"Te-re-si-a,m-to-to wa-na-ni?".
"mtoto wa Kaborongo, mdogo wako".
"Te-re-si-a ma-ma,hu-ja-mbo?".
"sijambo, shikamoo baba".
"ma-ra-ha-ba ma-ma,u-me-kuja ku-ni-ona?".
"ndio baba,unaendeleaje?".
"ba-do na-u-mwa ma-ma, koh koh koh koooh koh,ha-ba-ri za hu-ko u-to-ka-ko?".
"huko hatujambo, Kibe anawasalimu sana".
Wakati wote huo Teresia alikuwa akitiririkwa na machozi, alimuonea huruma Mzee Sosongo alivyokuwa anaongea kwa tabu na jinsi alivyokuwa amedhoofu. Mzee Sosongo akamuambia Teresia,
"Ki-be ha-ja-mbo?, a-li-pa-ta- ka-zi?".
"ndio baba,hajambo na kazi alipata,amenipatia pesa kidogo na sukari niwaletee".
"tu-na-shu-ku-ru,je mu-me-o na-e ha-ja-mbo?".
"hajambo  anawasalimu sana".
Wakati Teresia na Mzee Sosongo wanaendelea na maongezi, Mama Kibe akaingia mle chumbani, akamuambia Teresia,
"mwanangu, njoo huku walau upate kikombe cha chai". Teresia akanyanyuka pale alipokuwa ameketi na kumfuata mama Kibe hadi jikoni. Wakati anaendelea kunywa chai, akamuuliza mama Kibe,
"baba toka ameanza kuumwa, mlishawahi kumpeleka hospitali?".
"baba yako mbishi sana, hataki kwenda hospitali na hata hizo za kizungu hazitaki, anasema eti zina sumu".
"kwani ni nini hasa kinachomsumbua?".
"miguu inavimba, anasumbuliwa na kifua na kuna wakati tumbo lilikuwa limevimba".
"sasa anatumia dawa gani?".
"anatumia dawa za mitishamba".
"hizo dawa zinamsaidia? kwani bado anavuta kiko?".
"tunaweza tukasema zinamsaidia maana tumbo halijavimba tena toka azianze, kiko havuti tena".
"je anakula vizuri?".
"hapana mwanangu, chakula chake ni uji na supu, chakula kigumu akila anatapika".
"je akipewa ndizi zilizopondwa na kuwa kama uji anatapika pia?".
"hicho sijawahi kumpa, labda nijaribu".
"hicho niachie, naomba unitayarishie ndizi na kama kuna nyama naomba uinjike jikoni".
"nilifikiri una haraka, unataka urudi nyumbani".
"leo nimekuja kushinda hapa, nitaondaoka jioni ila kama hutaki usaidizi wangu.....
Marina akamkatisha Teresia,
"hapa ni kwenu na nitafurahi sana ukishinda hapa maana kila wakati ukija hapa una haraka".
"baasi kama ni hivyo hata kulala nitalala huku, naomba unitayarishie
hizo ndizi nianze kuzimenya".
"nyama nilishainjika nilikuwa nataka nimuandalie supu,kuhusu kumenya ndizi hizo niachie maana zina utomvu"
"mama! mbona wataka kunifanya kama sijawahi kumenya ndizi?, sinimekulia hapa, tafadhali nakuomba uniletee hizo ndizi na kisu na wewe ukaendelee na shughuli nyingine".
Baada ya ndizi kuiva Teresia akaziponda hadi zikawa laini kasha akachukua supu na kuchanganya.
Marina alipomfata jikoni akamuuliza, "haya mwanangu, niambie mapishi yanavoendelea".
"hebu kiangalie kama hiki akila, atatapika?".
Marina akaweka kidogo katika bakuli na kuonja,
 "kitamu sana, hiki atameza bila shida na hatatapika, ngoja nikuletee bakuli uweke ili nikamlishe maana hawezi kula mwenyewe".
"kama hawezi kula mwenyewe leo itakuwa zamu yangu ya kumlisha".
"utamuweza?, japo anaumwa nimbishi kweli, kwasababu wewe umepika, ngoja namie nikamlishe".
"hapana mama, nimekuambia leo ni zamu yangu, nipe hiyo bakuli". wakati Teresia anaendelea kumlisha Mzee Sosongo, Mzee Sosongo akamuambia,
"Te-re-si-a ma-ma'
"rabeka baba"
"ka-wa-i-da mtu a-ki-wa m-ze-e kama mi-mi,ya-bi-di ku-wa-na-si-hi
wa-pe-ndwa wao,maana ha-tu-ju-i siku wa-la saa ma-u-ti yata-ka-po tu-kumba....
Teresia akamkatisha Mzee Sosongo.
"baba mbona waongelea tena mambo ya kifo?, usikate tamaa Mungu ndio muweza na bila shaka atakuafu"
"acha ni-o-ngee kwa-nza,upe-ndo na kusuluhisha pale mna-po ko-sana, ndio m-si-ngi wa ndoa, wa-o-na mimi na ma-ma yako, japo tu-li-che-lewa kupata mto-to hatukuwahi ku-ja-ri-bu kutengana, na-ku-ambia hi-vo mana nyie vi-ja-na wa siku hizi hamkawii kuachana, mkikorofishana kido-go huo ndio mwisho wa ndoa, Kibe ni ndu-guyo, hu-ko alipo we-we ndio mle-zi wake, akipotoka muonye na mreke-bishe, koh koh koooh kooh koh...
Wakati mzee Sosongo anaendelea kuongea, akapaliwa na kuanza kukohoa, akakohoa hadi akatapika kile chakula alichokuwa amekula. Marina akamuambia Teresia amuache apumzike kwanza, wakamletea maji
akanywa kidogo huku akihema kwa tabu sana.
"mama, mi nilikuwa naona tumpeleke hospitali".
"mwanangu, baba yake alisema, kama kuna anaetaka amuachile laana basi ampeleke hospitali".
"lakini jinsi anavyoumwa hivi, angeweza kupatiwa matibabu nakupata afueni".
"labda ukaonge nae pengine wewe anaweza kukusikiliza"
Teresia akarudi kule chumbani, akakuta Mzee Sosongo ametulia, akafikiri amelala, akarudi kumueleza mama Kibe.
"nafikiri amelala maana ametulia".
Marina kusikia vile akastuka, akatoka pale jikoni na kwenda kumtazama Mzee Sosongo maana haikuwa kawaida yake kulala mchana. Alipofika akamuita,
"baba Kibe, baba Kibe",
hakujibiwa, akaamua amshike mkono. Aliposhika mkono wake ulikuwa wa baridi, akawekea mkono kifuani kwake ili kuangalia mapigo ya moyo, akagundua kuwa Mzee Sosongo alikuwa amefariki. Baada ya kugundua kuwa Mzee Sosongo amefariki, akapiga ukunga,
"uuuwii, uuuwii, baba Kibe umeniacha mpenzi, ulikuwa rafiki, mpenzi na mume mwema kwangu, nitaishi vipi bila wewe jamani mume wangu, kwani umeniacha Sosongoo uuuwiii".
Teresia aliposikia Marina akipiga ukunga akakimbilia kule chumbani kumfuata,
"mama kwani imekuaje?, mbona walia?, jamani baba amefanyaje mama?".
Marina akamjibu huku akilia.
"Teresia mama, baba yako hatunae tena, baba amefariki Teresia".
Teresia naye akaangua kilio na kwenda kumkumbatia Mzee Sosongo,"baba, baaaba, baba kwanini baba, kwanini umetuacha baba, ulikuwa kiongozi wetu wa familia, tulikuwa twahitaji sana hekima zako baba, sasa umetuacha",
hayo yalikuwa maneno ya Teresia, huku akilia kwa sauti ya juu. Teresia alilia hadi akaishiwa nguvu, Marina alipoona Teresia anaishiwa nguvu akamshika mkono na kumtoa pale alipokuwa amemkumbatia Mzee Sosongo na kumpeleka chumba kingine kisha akamkorogea sukari katika maji na kumpa anywe,
"kunywa haya maji ili upate nguvu na ujikaze maana kifo ni wajibu, tumuombee tu kwa Mungu ili ampe pumziko la amani huko aendako".
Majirani waliposikia vilio, wakafika pale kwa Mzee Sosongo kujua nikipi kilichojiri. Walipotambua kuwa Mzee Sosongo amefariki, mmoja wa wazee aitwae Njuguna akaombwa aende kwa mdogo wake Sosongo, Kaborongo akamueleze kuhusu kifo cha nduguye.

     Mzee Sosongo ndio hatunaye tena, Je maisha ya Kibe yatakuaje bila uwepo wa baba yake Mzee Sosongo?...Je Kibe akizipata taarifa za msiba wa baba yake atachukua hatua gani?.........je Moris atafanikiwa?...je nini kitamtokea Moris?.... endelea kufatilia hadithi hii kwa wiki lijalo?

No comments:

Post a Comment