Monday, November 5, 2012

DUNIA RANGI RANGILE ( 7 ) Sehemu ya saba                                                

                                               Mtunzi: Lasima Nassoro
  ilipoishia...baada ya kupata taarifa za msiba wa baba yake kibe anaamua kurudi kijijini, je nini kitatokea huko kijijini?..fuatilia sehemu ya saba ya hadithi hii uipendayo...
 
  Kibe alipofika kijijini alimkuta mama yake akiwa na baba yake mdogo Mzee Kaborongo, Mzee Kaborongo alimuona Kibe kabla ya Mama yake, akamuambia Marina,
"naona tumepata mgeni".
Marina alipoona kuwa mgeni ni mwanae,  akasimama na kwenda kumpokea,
"karibu mwanangu,karibu baba".
"asante mama" Kibe akamshika mama yake mkono
"makiwa mama"
"yamepita baba, habari za huko utokako?".
"nashukuru Mungu, shikamoo mama".
"marahaba pole kwa safari ".
"asante".
Kibe akamfuata mzee Kaborongo pale alipokuwa amekaa
"makiwa baba"
Mzee Kaborongo akamjibu, "yamepita,habari za mjini?".
"sio mbaya, shikamoo baba".
"marahaba, dada yako ,Teresia hajambo?"
"hajambo, anawasalimu sana".
"tumezipokea, umeshazoea mji?".
"si sana maana sehemu niliyokuwa nafanyia kazi ni mbali sana na mjini"
Marina akaingiza mizigo ya Kibe ndani, alipotoka akatoka na mkeka na kuutandika karibu na alipokaa Kibe na Mzee Kaborongo. Kibe akaelezewa mzee Sosongo alivougua hadi akafariki. Mzee Kaborongo akamuambia Kibe, "Mzee Sosongo hatunae ila ametuachia msingi wakufanya ukoo wetu uendelee mbele, cha msingi ni ushirikiano kama utakuwa na jambo linakutatiza, mie nipo, usije ukasema baba yako mzazi amefariki kwahiyo huna tena wa kumkimbilia".
Kibe akamjibu, "sawa baba".
Mzee Kaborongo akasimama akasema,
"mama Kibe, ngoja nirudi nyumbani nikaangalie cha kufanya kabla giza halijaingia. Kibe akatoa bahasha na kumkabidhi  Mzee Kaborongo,
"baba barua yako hii nimepewa na dada nikuletee".
"asante,ngoja niende, mengi zaidi tutaongea kesho, kwani si bado upo?".
"ndio, nitakuwepo kwa muda hapa".
Baada ya mzee Kaborongo kuondoka, Kibe akamfuata mama yake ndani.
"mama umeona zawadi nilizokuletea?"
"sijaona maana hujaniambia kuwa kuna zawadi zangu".
"kwahiyo hujafungua hiyo mizigo kuona kuwa nimeleta nini?"
"si heshima kufungua kitu ambacho hujaambiwa ufungue, kama umeniletea zawadi unatakiwa uniambie, mama zawadi yako hii nimekuletea".
"basi mama nimekosa, nimekuletea vitenge, sijui kama utavipenda ama la maana sijui rangi uipendayo".
Mama Kibe akachukua vile vitenge na kujifunga kingine akajitanda, kasha akamuambia Kibe,
"mbuzi wa kupewa, haangaliwi kama ana mapengo, nashukuru sana mwanangu, kuhusu rangi, rangi ile inayopendeza machoni ndiyo niipendayo nahii rangi hakika yapendeza macho, Mungu akazidishie
mwanangu".
"asante mama, nashukuru kama umevipenda, nimeleta sukari na unga wa ngano pia".
Muda wa mifugo kurudi nyumbani ukawadia, Kibe akatoka kuiongoza ili iingie zizini.
Wakati Kibe anaiongoza mifugo iingie zizini, akasikia wimbo ukiimbwa redioni, baadhi ya maneno ya wimbo huo ni,
"nyamaza kuliia, wanitia uchungu kwa kuondokewa na baba yetu...
"baba alituasa yakuwa dunia ni rangi rangile, walimwengu ni wabaya, yapasa kuwabaini wema nawabaya...
"baba alisema, maringo na majivuno yapasa tuyaepuke maana hapa duniani twapita, yatupasa kutenda mema na kumcha Rabana maana kwake tulitoka napia tutarejea".
Kibe aliposikia maneno yale toka redioni, machozi yakamtoka, alihisi kama anaimbiwa yeye. Aliporudi ndani Mama yake akaona Kibe amekuwa na huzuni sana na macho yake yamekuwa mekundu, akamuambia,
"Kibe mwanangu,baba yako hayupo nasi kimwili ila  kiroho yupo nasi, unapohuzunika namna hiyo, huko alipo hapati pumziko la amani, atafurahi kama utakuwa unamuombea dua njema na kujibidiisha kimaisha, sote pua zetu zimeangalia chini, hiyo ina maana kuwa sote tutarudi mavumbini ambapo ndipo tulipotoka".
Kibe hakusema kitu maana uchungu ulikuwa umemjaa rohoni, machozi yalimjaa machoni. Baada ya wiki mbili kupita toka Kibe alipofika kijijini, mama yake akamuuliza,
"Kibe, kama ni maombolezo, umeomboleza vya kutosha, je huko mjini warudi lini?".
Kibe akatabasam kisha akasema,
"mama yaani umeshanichoka mara hii?".
"siwezi kukuchoka mwanangu, kama ulikaa tumboni kwangu kwa muda wa miezi tisa yenye karaha na sikuchoka, sembuse wakati huu ambao unanisaidia?, ninachofia ni kuhusu kibarua chako baba, hakuna laziada".
"nilikuwa nakutania tu mama, kujibu swali lako kwamba narudi lini mjini, jibu ni  'LA', sitarudi tena mjini, nataka nikae hapa niangalie hii mifugo yetu".
"kama mifugo ndio inayokufanya usiende, hilo lisikupe shida maana hata baba yako alikuwa haendi machungani kama alivyokuambia kipindi kile kabla hujaenda mjini kuwa kuna mtu anapewa mbuzi jike kil baada ya miezi minne".
"huyo anaechunga, kwa mwaka atakuwa na mbuzi watatu, kama anachuka mifugo ya mabona manne,   kwa mwaka atakuwa na mbuzi kumi na wawili, hivyo huo ni mtaji tosha kwake".
"kwahiyo unataka ubaki hapa ili ufanye hiyo kazi ya kuchunga mifugo ya watu?".
"sina maana hiyo mama, ninachotaka mimi nikuangalia mifugo yetu nasio ya watu wengine".
"kwani hiyo kazi uliyokuwa unafanya huko mjini, imekaje huitaki tena? au kuna mtu umemkosea huko sasa unataka ujifiche huku kijijini".
"wala hakuna niliyekosana nae, kwanza wengi wao walinipa pesa za rambirambi walipojua kuwa nimefiwa, nimeamua tu kuwa sitaki tena kuajiriwa, nataka nijiajiri mwenyewe na ajira yangu ni hii mifugo yetu pamoja na kilimo, mjini kuna soko kubwa sana la bidhaa zitokanazo na mifugo pia mbogamboga zinaliwa kwa wingi huko"
"haya baba, kama ndivyo ulivyoamua...
"usihuzunike mama, chamsingi ni kuniombea heri ili nifanikiwe, kwanza hiyo kazi niliyokuwa nafanya sikuipenda, nilikuwa nasubiria tu nipate wasaa wa kutoka huko tulipokuwa".
"ninachotaka na kukuombea ni mafanikio mwanangu, kuhusu kazi utakayofanya, mie sina kipingamizi bora iwe kazi halali mbele ya sheriana machoni pa Mungu".
 "inshaallah Mama Mungu asikie na ajibu maombi yako".
Kibe akaanza maisha rasmi ya kijijini, wakati huu akiwa na malengo ya kufanikiwa kimaisha kupitia kilimo na ufugaji. Alianza kuandaa shamba la kupanda mbogamboga, baada ya kulima kwa kukatua vizuri, akawa anapeleka mbolea ya samadi walau mifuko miwili kila asubuhi kabla ya kwenda kupeleka mifugo malishoni. Alitengeneza vitalu, akamwaga mbegu za nyanya, vitunguu, pilipili mboga na karoti. Baada ya kuotesha, ikawa desturi yake kuamka alfajiri na mapema kwenda kunyweshea mimea yake aliyootesha, kwakuwa kulikuwa na mto uliokuwa unapita karibu na bustani zake zilipo, hakupata shida ya kusomba maji. Teresia baada ya kupata habari kuwa Kibe hatorudi tena mjini, akaamua
kwenda kumtaarifu Bwana Kanjubai. Alipofika kwa Kanjubai, alimkuta akiongea katika simu, Kanjubai akamuonyeshea ishara yakuwa aingie na akae katika kochi. Kanjubai alipomaliza kuongea katika simu, akamsalimu Teresia na kasha kumuuliza nini kilichomleta. Teresia akamjibu,
"aah Bwana Kanjubai, vibaya hivyo ndugu yangu, kwani siwezi kuja kukusalimia bila yakuwa na tatizo?".
"i didn’t say that, wajua I am a very busy man so niambie kama kuna tatizo au ni salamu tu because saa saba sharp natakiwa niwe nipo airpot naelekea Cape town".
"sawa,nimekuja kukutaarifu kuwa Kibe,hatarudi tena huku kufanya kazi".
"kwani yeye ameonaje hadi hataki tena kazi?".
"nimeambiwa kuwa amesema hataki tena kazi ya kuajiriwa".
"sasa atafanya nini huko kijijini? yeye hajui kuwa siku hizi kila kitu ni pesa?".
"ameamua kuwa mkulima, baba yake amemuachia mifugo hivo ameona kuwa nijukumu lake kuiangalia hiyo mifugo, ukizingatia kuwa amezaliwa peke yake ni vizuri kukaa na mama yake ili amsaidie kazi maana mama yake ameshakuwa mzee".
"okay, nilifikiri pengine amegundua shughuli zetu so anataka kutuchomea utambi".
"kwahilo usihofu, Kibe hata hiyo cocain hajawahi kuisikia na hata kama ameisikia atamueleza nani?, toka azaliwe hajawahi kutoka kijijini, akienda mbali sana ni vijiji vya jirani, kusafiri kwake ni hivi nilipokuja nae huku".
Kanjubai akasimama na kwenda kusimama karibu na dirisha, akanyanyua pazia kidogo kuchungulia nje kama vile kuna anachoangalia. Alisimama pale dirishani kwa muda bila kusema kitu, kisha akageuka na kumuangalia Teresia, akasema,
"mume wako umeongea nae mara ya mwisho lini?".
Teresia moyo ukamuenda mbio baada ya kuona Kanjubai alivyobadilika sura ghafula, akamjibu,
"kwani hujaongea nae toka aende Lilongwe?".
"Damn it Teresia, stop beating around the bush, nimekuuliza umeongea na Samson mara ya mwisho lini, that's a simple question?".

Je ni kweli Bwana Kanjubai ameafiki Kibe Kuacha kazi, je nini kimemkumba bwana Kanjubai? usikose sehemu ya nane ya hadithi hii...itaendelea....

No comments:

Post a Comment