Thursday, October 18, 2012

DUNIA RANGI RANGILE ( 6 ) Sehemu ya Sita

                                              Na Lasima Nzao
   Mzee Songoro ndio hatunae tena..kibe bado hajapata taarifa za Kifo cha baba yake..je nini kitatokea..endelea

  Baada ya mazishi ya mzee Sosongo,Teresia alirudi mjini kuendele na shughuli zake. Baada ya wiki kuisha akaenda kwa bwana Kanjubai kumpa taarifa za msiba wa baba yake Kibe.
"sasa wewe nataka hii kijana irudi kijijini, yeye ilishaanza zoea kazi".
hayo yalikuwa maneno ya Kanjubai akimueleza Teresia. Teresia akamjibu,
"nimekuambia kuwa baba yake mzazi amefariki hivo lazima aende nyumbani akamuone mama yake na pia aone alipozikwa baba yake, baada ya hapo si atarudi aendelee na kazi yake?".
"hapo sasa mimi iko elewa wewe, kesho Moris atakwenda chukua yeye alete hapa, kwani siataweza kwenda menyewe huko kijijini?".
"akipakizwa katika gari la kuelekea huko kijijini atafika bila shida, sasa si utampa pesa za rambirambi?".
"Teresia!, Teresia!, wewe nafikiri pesa iko okotwa?, yeye anapata mshahara hiyo inatosha yeye".
"nafahamu kuwa anapata mshahara,lakini hii ni shida iliyompata mfanyakazi wako bwana Kanjubai, ni kiasi gani unachopata kutokana na kazi anayokufanyia?, ukijali masilahi ya mfanyakazi wako nayeye atajali na kujituma kwa bidii kazini".
"wewe iko maneno mengi sana, basi nitaangalia chakufanya but this because of you otherwise i wouldn't give him a dime".
"nashukuru kama umenielewa, sasa nataka mzigo mwingine maana ule wa mwisho haukukaa sana".
"hii ni kazi ya Moris, subiria yeye arudi toka huko alipoenda then atakupa".
"sitamsubiri nina haraka, kama wewe huwezi kunipa basi akija mueleze aniletee pale kijiweni kwangu".
"unataka akuletee kete ngapi?".
"mwambie aniletee kete tano".
"no problem, kwaheri".
"kwaheri Kanjubai". Kibe baada ya kujifanya uchunguzi kwa muda mrefu hakuna jibu alilopata, siku moja baada ya kazi akaambiwa kuwa ni zamu yake ya kusubiria watakao chukua malighafi ya siku hiyo.
Akiwa amekaa katika gogo huku akiwaza jinsi wazazi wake wanaendelea,Fabian akamfata pale alipokuwa, "inakuaje mtu wangu, mbona waonekana kama umehamia ulimwengu mwingine?".
"ooh bwana Fabi, niko poa mtu wangu na nafikiria kuhusu haya maisha".
"wanasema kuwa maisha ni kama kitabu kila siku unafungua ukurasa mpya".
"kweli mtu wangu, vipi huko juu kazi inaendaje?".
"huko shwari, unajua toka siku ile uniulize lile swali lako nimekuwa nakuchunguza ili nione kama we ni mtu wa siri au la".
"sikiliza nikuambie Fabian, mimi nilikwenda jando na jambo muhimu  tuliyofunzwa ni kuwa msiri, yale yote tuliyoelezwa yaliishia kulekule porini, hivyo kama hilo ndio lililokuwa linakupa hofu, shaka ondoa".
"shaka sina tena, ndio maana leo nataka nikueleze ujue kinachoendelea hapa, kama utataka kuendelea kufanya kazi hapa hiyo itakuwa juu yako".
"sawa, nitegulie kitendawili na unieleze yote".
"poa, siku ile uliniuliza kuhusu haya majani munayotwanga kila siku yana kazi gani,au sivyo?".
Kibe alipoambiwa hivo,akamsogelea Fabian hadi wakawa wanagusana
mabega,akamjibu, "haswaa". Fabian akatabasamu kisha akaendelea, "umeshawahi kusikia mmea uitwao coca?".
"sijawahi ila najua soda iitwayo coca".
"basi kuanzia leo ujue kuna mmea uitwao coca na yale majani munayotwanga ni majani ya huo mmea".
"kwahiyo soda ya coca hutengenezwa na haya majani tunayotwanga kila siku?".
"acha papara, umeuliza swali sasa tulia kama unanyolewa ili upate majibu".
"ni ile shauku  ya kutaka kujua maana nimesumbua kichwa hadi nimechoka, endelea kaka".
"sasa yale majani yanatengenezea cocain,si unajua cocain kuwa ni nini?".
"sijui na sijawahi kusikia hilo neno, kwani ndio nini hiyo?".
"umewahi kusikia madawa ya kulevya?"
"ndio si wanaita unga au hashishi?".
"baasi huo unga ndio cocain au mandrax, sasa yale majani mukitwanga hapa yanachukuliwa na kupelekwa kuchemshwa hadi yatoe nta, hii nta huchanganywa na dawa nyingine pamoja na mafuta ya taa hadi mwisho unapatikana unga mweupe pee kama poda, hiyo sasa ndio cocain".
Baada Fabian kumaliza kumuelezea Kibe,Kibe hakusema kitu, alihisi mwili kumtetemeka.
Fabian alipoona kuwa Kibe ameingiwa na woga, akamuambia, "oyaa mbona umekuwa mpole ghafla kama umemwagiwa maji ya baridi?"
"sio hivyo kaka hizi habari ulizonipa zimeniogofya, kusema ukweli sikutegemea kuwa kazi nifanyao ni haramu"
"haya sasa umejua, na usije ukamuambia yeyote nilichokueleza maana hiyo ni siri kubwa ukiitoa ujue unakaribisha mauti yako".
"usijali kaka, nilishasikia sana habari za wauza unga, sasa hata hamu ya kufanya kazi tena imeisha".
"kazi lazima ufanye maana huumwi, we fanya kazi huku ukitafakari niliyokuambia kisha uamue kama utataka kuendelea ama la, na kama ukiwaambia kuwa hutaki tena kazi yaweza ikakuletea madhila maana watakuuliza kwanini unaacha kazi".
"ngoja nifikirie kwanza maana hizi ni habari nzito sana kwangu, nikuulize swali?".
"uliza tu"
"hii cocain wanauzia wapi? na ushawahi kuionja kuwa ni tamu ama la?"
"unataka uionje?"
"siwezi na sitowahi kutumia hiyo kitu,nijibu basi swali langu".
"kuhusu sehemu inapouziwa sijui ila soko lipo tena kubwa sana na kuonja niliwahi kuionja, sio tamu, ladha yake niya uchachu".
"sasa kama ni chachu, wanapata raha gani kuitumia?"
"kile ni kilevi ndugu yangu, unanusa au unalamba kidogo baada ya muda unajihisi kuwa upo ulimwengu mwingine wenye raha zote za dunia hii".
"kwahiyo bado unatumia, maana unavyoielezea yaelekea umzoefu".
"hahaha,nimekuambia nilionja nikifikiri ni tamu kama glucose lakini sijawahi kuitumia, najua madhara yaletwayo na hizo dawa hivyo siwezi kutumia"
"kumbe ina madhara? mie nilifikiri ni ulevi pekeyake".
"ile kitu ukianza kuitumia kuiacha itakuwa shida, na usipoipata wakati itakapokuwa imekuzoea, utakuwa hoi kwa ugonjwa, kila kiungo kitakuwa kinauma".
"duuh! sitaki hata kuiona, nashukuru sana Fabi, kwa kunifumbulia fumbo lililokuwa linanitatiza toka nifike hapa".
"hakuna shida mtu wangu chamsingi haya niliyokueleza yaishie hapahapa, kama utataka upigwe risasi ya kichwa basi utoe hii siri, usije ukasema sijakuonya".
"shaka ondoa kaka,ngoja mie nirudi kwenye makazi yetu nikaoge maana nimechoka sana"
"poa, kwaheri Kibe"
"kwaheri kaka".
Kibe alipofika katika makazi yao, akamkuta Moris akimsubiria. Moris akamuambia kuwa amekuja kumchukua maana Teresia amerudi toka kijijini na Mzee Sosongo anaumwa sana hivo Kibe anatakiwa aende. Kibe akajitayarisha kisha wakaondoka na Moris. Alipofika mjini akapelekwa kwa Teresia.
Teresia alipomuona machozi yakaanza kumtoka, akamkumbatia Kibe kwa muda bila kusema lolote huku akilia kwa kwikwi. Kutokana na hali ile Teresia aliyoionyesha, Kibe moyo ukamuenda mbio, wazo likamjia kuwa baba yake atakuwa hayupo tena duniani, akajikaza kiume na kumuambia dada yake,
"dada mie ni mtoto wa kiume kama kuna lolote baya we nieleze tu maana mabaya na mazuri tumeumbiwa sie wanaadamu".
Teresia akatulia kisha akaenda kukaa katika kochi, Kibe akamfata pale alipokaa, akakaa pembeni yake na kushika viganja vyake akamuambia,
"kwanza shemeji yupo wapi?". Teresia akavuta pumzi ndeefu,
"shemeji yako amesafiri jana atarudi baada ya wiki mbili".
"sawa dada nipe hali halisi uliyoikuta huko kijijini na usinifiche maana mie sio mtoto mdogo".
Kibe akatabasam na kumuangalia machoni,"oooh Kibe mdogoangu, kifupi nikuwa baba hatunae tena, mzee Sosongo ametutoka". Kibe alipoambiwa hivyo alihisi kama amekatwa maini,alikuwa anahisi
kulia,lakini machozi hayakutoka, akabaki kuangalia tu dari, Teresia akamkumbatia na kumuambia,
"usiogope kulia mdogoangu, lia maana itakusaidia kutoa uchungu rohoni".
Teresia alimalizia tu maneno yake, akaanza kulia tena kwa sauti. Kibe hakutokwa na machozi ila alihisi kuishiwa nguvu, wakati Teresia anaendelea kulia huku akiwa amemkumbatia Kibe,alihisi kuwa Kibe
amekuwa mzito ghafla, akamsukuma ili amuangalie machoni lakini alikuwa amelegea.
Teresia kuona vile akamlaza katika kochi kisha akafungua vifungo vya shati nakuanza kumpepea, baada ya muda Kibe akafungua macho, Teresia akampa maji yenye glucose akanywa.

Baada ya muda akarudia hali yake ya kawaida na akamuuliza Teresia,
"baba amefariki lini?"
"hii ni wiki ya pili toka afariki, nilipoenda kipindi kile nilipokutumia taarifa kuwa naenda kijijini,hali yake haikuwa nzuri".
"sasa mbona sijapewa taarifa pindi tu alipofariki?"
"Kibe mdogoangu, wafahamu vema mazingira ya kijiji chetu, na hupo unapofanyia kazi hakuna simu hadi mtu atoke huku aende huko kutoa taarifa".
"sawa dada,kesho asubuhi nataka niende nyumbani".
"sawa mdogo wangu".

................itaendelea wiki lijalo....

No comments:

Post a Comment