Tuesday, November 20, 2012

DUNIA RANGI RANGILE ( 9 ) Sehemu ya Tisa


                              Mtunzi: Lasima Nassoro  
Samson amekimbia na mzigo wa Bwana Kanjubai? je samson amekimbilia wapi? je nini kitatokea akigundulika alipo?...endelea....      
Wakati Teresia akiendelea kuwaza kuhusu mustakabali wa maisha yake, simu ikaita, akakurupuka toka pale alipokaa kwenda kuchukua simu akifikiri ni  Samson anayempigia, alipoangalia jina la mpigaji akaona ni rafiki yake aitwae Jamila, "vipi shost, mbona leo haujafungua kibanda chako?", Jamila alimuuliza Teresia. 
Teresia hakufurahi alipoona kuwa mpigaji hakuwa Samson hivo hakupenda kuwa na mazungumzo marefu na Jamila, akamjibu,
"sijisikii vizuri leo, nahisi nitakuwa na malaria".
"hata mie nilifikiri tu kuwa utakuwa unaumwa maana si kawaida yako kuacha kufungua, pole mwaya, nitakupigia kesho kuangalia kuwa unaendeleaje, ila kama hujaenda hospitali, kesho asubuhi na mapema uende ukachekiwe, sawa shosti?".
"nashukuru, nitafanya hivo, usiku mwema",
alipomaliza kumuaga Jamila, Teresia hakusubiri jibu maana anamfahamu vema Jamila kuwa kama hata kata simu, Jamila ataanzisha stori za umbea alizo sikia mchana kutwa.Teresia alikuwa akitazama Tv lakini akili yake na mawazo yote yalikua kwa Samson, alikumbuka jinsi walivoanza urafiki wao baada ya Samson kuwa mteja wake mzuri, karibia kila siku ambazo hakusafiri, alikuwa akienda kula chakula katika kibanda cha Teresia, siku hiyo Samson akamuambia Teresia,
"leo usiku naomba nikutoe"
Teresia akajifanya hajamuelewa, "unitoe nini?,na kwanza sijakuambia kuwa nina kitu nataka nitolewe".
Samson akatabasam kisha akasimama pale alipokuwa amekaa na kwenda alipokaa Teresia,akashika pua ya Teresia na kuitingisha tingisha,akamuambia,
"you are a naught girl".
"wengine hatujui kidhungu,usije ukawa unanitukana".
"hahaha,sijakutukana,nimesema kuwa umeumbwa ukaumbika".
Samson akakaa karibu na alipokuwa amekaa Teresia. Teresia alipoambiwa kuwa  ameumbika,akahisi soni ikimuingia machoni, akashindwa kumuangalia Samson machoni, akaamua kutoka pale na kwenda kukusanya vyombo vilivyotumika. Kabla hajafikia vile vyombo,Samson akamshika mkono na kumzuia
asiondoke pale alipo,akamuambia,
"mbona wataka kunitoroka kabla hatujafikia muafaka?"
Kitendo cha Samson kumshika mkono,Teresia alihisi kama ameshika waya wa umeme,mwili wote ulimsisimka, akakosa jibu la kumuambia Samson. Samson alipoona Teresia hasemi lolote, akamkalisha mbele yake nakumuangalia machoni,"bibie,mbona umekuwa mpole ghafla,nimesema neno lolote lililo kukerehesha?". Teresia akatingisha kichwa kuonyesha ishara ya kuwa hakuna, bila kusema neno.
"kwani umekuwa bubu?, Teresia chiriku ameenda wapi?". Baada ya Samson kumuachia,Teresia alirudia hali yake ya kawaida,akamuambia Samson,
"nilikuwa nakupima kama wewe ni jasiri au la".
Samson akasimama,
"wanipima kuwa mi ni jasiri kwa kigezo gani?, kwanza hakuna kitu nilichoona hapa cha kunipima".
"nilipokaa kimya,nilikuwa nakupima kama utakasirika na kuamua kuondoka ama utaonyesha kujali".
Samson akacheka,
"kama hilo ndio lilikuwa kusudio lako,umenipata maana nilijihisi mkosaji, sasa tuachane na hayo,je umekubali twende club?".
"twende club kufanya nini?,mie sinywi pombe".
"acha ushamba,sio club za pombe,ni club za magoma kitakita,kwani hupendi muziki?".
"napenda ila sijawahi kwenda disco toka nizaliwe".
"basi ngoja iwe mara ya kwanza,twende ukasikie muziki kama ule usemao",
Samson akarekebisha koo kisha akaanza kuimba,
"nachungulia dirishani ooh,naona ni mvua yanyesha eeh, hakuna kilichobakia ooh, ila ni uchungu na huzuni eeh,mpenzi nauliza utarudi lini eeh, uje unitoe upwekwe na huzuni eeh,s heri rudi rudi mpenzi wa roho, sheri rudi mie nakufa kwa pendo, elewa dada nakupenda kwa uzuri wako, nakuomba utoroke eeh maana nakufa kwa upwekwe,njoo dada tuishi kwa upendo, ni wewe tu uliyeuteka moyo wangu,nakupenda kwa dhati", wakati wote huo Samson alipokuwa anaimba,alikuwa amefunga macho, Teresia akamuangalia jinsi alivojengeka kimaumbile, akahisi kumpenda Samson, alitamani awe wake peke ake. Samson alipofungua macho, akaona jinsi Teresia alivokuwa anamuangalia kwa macho ya mahaba, moyo wake ukamuenda mbio, akatamani amkumbatie na kum'busu lakini aliona kuwa anaweza kuharibu kila kitu, akajiambia mwenyewe kichwani mwake,'hawa watoto wa kutoka kijijini, hawatakiwi papara, mwendo wa kinyonga tu hadi tutafika', akatabasam. Teresia akamuuliza,"watabasam nini?".
Samsoni akamjibu,
"unajua kama ukiamka asubuhi na kitu cha kwanza kukiona chapendeza machoni,shurti utabasam".
"lakini sasa hivi si asubuhi, ni usiku".
"nafahamu hivo,wakati naimba nilipofungua macho, macho yangu yakakutana na ua waridi lipendezalo kuliangalia wakati wote bila kuchoka".
"eeeh! makubwa,haya hilo ua liko wapi?, maana mie silioni,isije ikawa upo ulimwenguni mwingine mie sijui".
"nimimi peke yangu nilionae,sasa club tunaenda?".
"sawa, ila sitaki nichelewe kurudi maana wajua shughuli zangu,saa kumi na moja alfajiri natakiwa niwe nimeshaamka".
"usijali, tukiruka ngoma mbili tatu, tutarudi".
"sawa, ila sikujua kuwa we ni muimbaji".
"kwani nimekuambia kuwa mimi ni muimbaji?".
"hujaniambia bali nimekuona ulivyokuwa unaimba huo wimbo kwa hisia kama vile wamuimbia mpenzi wako".
Samson akacheka kisha akamuambia ,
"sasa katika waimbaji na mie nitasema nimo?, si watu watanikimbia na kuniacha peke yangu wakisikia hili lisauti langu linalo fanana nala chura".
"hamna,umeimba vizuri kweli, ningeweza ningekutunza".
"kama hivo ndivo,basi kesho msosi utanipa bure,t ena si kidogo kama huu unaonipimia?, msosi wa kushiba na kikombe cha chai au kahawa".
"hehehee, uliona wapi mbuzi na kuku wakishirikishwa kupanga tarehe ya krisimasi?".
"una maana gani?".
"maana yangu nikuwa,mtu hajichagulii zawadi, we subiria na uwe mpole kama kondoo apelekwae mnadani".
Huo ndio ulikuwa mwanzo wa mapenzi kati ya Samson na Teresia,ambapo baadae waliamua kuishi pamoja kama mke na mume. Teresia aliendelea kukumbuka jinsi alivyokuwa akimuuliza mara kwa mara Samson kuwa ni aina gani ya kazi aliyokuwa akifanya,mara zote jibu lilikuwa,
"vuta subira mama,ipo siku utamjua the really Samson".
Siku moja wakati Teresia anasafisha nyumba, akaamua atoe nguo zote kabatini ili azikung'ute vumbi la kabati, alipotoa nguo za Samson, pakiti iliyojaa unga kama wa ngano ikadondoka, Teresia akaichukua na kuichunguza kama imetoboka au la, alipoona hakuna sehemu iliyotoboka, akaamua kuirudisha sehemu alipo ikuta kisha akapanga nguo kama zilivokuwa. Samson aliporudi, Teresia akamuuliza kuhusu ile paketi ya unga. Samson akahamaki,
"nani aliyekuambia uchakure nguo zangu?".
Teresia  akamwambia,
"sam, mbona umestuka hivo kama nimeua?, nilikuwa napanga nguo vizuri kabatini na kwabahati mbaya hiyo pakiti ikaanguka, kama nilifanya kosa kwa kupanga nguo zako vizuri, naomba
unisamehe na nakuahidi sitogusa tena nguo zako zikiwa kabatini".
Samson akaona kuwa huo ndio muda muafaka wa kumueleza Teresia kazi anayofanya. Teresia alipotulia, Samson akamwambia,
"hujafanya kosa kupanga nguo zangu, na pengine hii itanipunguzia wahaka niliokuwa nao". Teresia akashangaa maana hakuelewa Samson alichokuwa anaongea,
"una maanisha nini unaposema nimekupunguzia wahaka?".
"Tere my dear, si unajua nikiasi gani ninavo kupenda?".
"najua Sam hata mimi nakupenda sana ila sijaelewa nini unachomaanisha". 
Samson akamsogelea Teresia na kukaa, akashika viganja vyake, akamuambia,
 "kwanza nitakayo kueleza, usije ukamueleza mtu yoyoteyule, yote yaishie humu ndani, sawa?".
"mbona wantisha Sam?, yote haya yanahusiana na ile pakiti niliyoiona? au kuna jambo lingine".
"inahusiana na hiyo pakiti, kwani unajua kuwa ni kitu gani kilichopomle ndani ya pakiti?".
"sijui ila niliona imefanana kama unga wa ngano vile".
"ule sio unga wa ngano,inaitwa COCAIN".Samson aliposema hivo,akatulia ili kumpima Teresia kuwa amezichukuliaje hizo habari. Teresia aliposikia neno COCAIN,midomo ikaanza kumcheza,asijue la
kusema,akabaki akiwa ameachama mdomo kwa mshangao. Samson alipoona kuwa Teresia amestuka sana, akamuambia, "Tere darling, mbona umestuka hivo?, ile sio sumu ni kilevi tu kama vile pombe".
"sikutegemea kitu kama hicho,si unajua kuwa cocain ni haramu?".
"niharamu kama unataka iwe haramu,nisikilize kwa makini Tere,umekuwa unaniuliza mara kwa mara kuwa kazi nafanyia wapi na mara zote nimekuwa nakuambia uvute subira".
"ndivo ila sioni kufanya kwako kazi kunahusiana vipi na cocain".
  Samson ameamua kumpa siri ya kazi yake Teresia ? je Teresia ataweza kuficha siri hiyo?,nini chanzo cha Samsoni kutoonekana,na amekimbilia wapi? je nini kitatokea akigundulika alipo? usikose sehemu ya kumi ya hadithi hii...itaendelea....

No comments:

Post a Comment