Monday, September 17, 2012

DUNIA RANGI RANGILE (Sehemu ya Pili)


Mtunzi: Lasima Nassoro Latif Nassoro

Katika sehemu iliyopita tuliona namna kibe alivyotakiwa aondoke kijijini kwao aelekee mjini kufanya kazi..leo hii hadithi inaendelea..je atafika mjini?,,,je ni kazi gani anayokwenda kuifanya? ungana na Mtunzi wetu Lasima Nassoro ujue nini kimeibeba dunia rangi rangile...

 
                   Kibe aliporudi akaambiwa ajiandae ili akalale kwa baba yake mdogo tayari kwa safari kesho.
Baada ya Kibe kuwa tayari, Mzee Sosongo akachukua maziwa ili atambike, akamwaga kidogo chini karibu na mafiga kasha akasema,
"Thekere, chukua maziwa haya, kuwepo kwetu hapa ni sababu yako maana babu wa babu wa babu yangu alikuwa mwanao, kuna mwanao hapa anaenda huko mjini, twakuomba ukamuongoze na umfungulie njia na umuwekee mkono apate hicho akifuatacho huko, umlinde na umuepushe na hila za wanadamu wabaya".
Baada ya kumaliza kusema hayo, akamwaga maziwa kidogo, yaliyobaki akanywa kidogo,akampa mkewe nae akanywa kidogo kisha Kibe akaambiwa amalizie yaliyobaki. Mzee Sosongo akasimama kisha akatema mate kidogo kiganjani mwake na kumpaka Kibe katika paji lake la uso nakusema,
"huko uendako, nyota yako ikang'ae kama mwezi, maadui wawe marafiki zako, majini yageuke kuwa malaika, wachawi wageuke kuwa waganga, wenye husda na chuki wageuke kuwa na upendo, na marafiki wazidishe urafiki wao, lolote utakalo fanya liwe na mafanikio, ukiokota jiwe libadilike liwe dhahabu"
Kisha akakaa, akasema, "Kibe mwanangu, huko uendako ni ugenini, heshima na adabu ndio silaha ya mafanikio yako, unapokosa omba msamaha, huko uendako utayaona mengi mwanangu, mengine mazuri na mengine mabaya, fuata yale mazuri na yatakayo kusaidia maishani, uepuke vishawishi vya mjini maana ukifata vishawishi, utasahau ulipotoka, pombe mwanangu ndio chanzo cha maovu yote humu duniani, epuka pombe, kufikia hapo sina la kuongezea, pengine kama Mama yako ana lake la kukuambia".
"hayo uliyo muambia yanatosha, mie namtakia tu safari njema"
Kibe akasimama pale alipokuwa amekaa na kwenda kupiga magoti mbele ya baba, kisha akasema,"Baba pamoja na Mama, hayo yote mliyonieleza nitajitahidi kuyatekeleza, kama nitaona maisha ya huko
yamenishinda, nitarudi"
Mzee Sosongo akamnyanyua na kusema ,
"sawa baba, chukua mizigo uende maana giza linazidi kuwa nene, na usije ukatusahau ukiwa huko" "sitowasahau wazee wangu, kwaheri Baba, kwaheri Mama, mbaki salama"
Taswira ya mji aliyokuwa nayo Kibe kichwani mwake ilikuwa tofauti na ile aliyoikuta, alishangaa kuona majengo marefu na barabara za lami,
"hivi dada haya majumba, walitumia mti gani mrefu kiasi hiki kutengeneza ngazi ya kujengea?
" Teresia akamjibu, "hawakutumia mti, kuna chuma maalum za kutengenezea majukwaa ndio walizo tumia"
"na hizi barabara nyeusi hivi walitoa wapi unga wa udaga mwingi kiasi cha kutosha barabara zote hizi?"
"hahaha ,Kibe wanifurahisha kweli,hiyo inaitwa lami na sio unga wa udaga uliotumika"
"usinicheke dada, mwenzio nataka kujua, si unaelewa jinsi mazingira ya kule kwetu yalivyo?"
"sio kwamba nakucheka ila wanifurahisha jinsi unavyolinganisha unachokiona hapa na kule kijijini". Maisha ya mjini yakampendeza Kibe, akawa akimuambia Teresia kuwa kama atafanikiwa kimaisha angependa nayeye ajenge nyumba nzuri mjini na kule kijijini. Teresia alitabasamu tu kila wakati Kibe akimueleza juu ya ndoto yake, siku moja Teresia akamwambia Kibe,
"Kibe mdogoangu, kila mtu anapenda awe na maisha mazuri, nyumba nzuri na gari la kutembelea lakini si kila mwenye ndoto hizo huweza kuzitimiza, unajua kwanini?"
"sijui Dada yangu, labda unifahamishe pia namna ya kutimiza ndoto hizo"
"juhudi na maarifa ndio silaha ya mafanikio, ukiwa na nia ya kufikia malengo fulani, njia haikosekani si unajua mchagua jembe si mkulima?"
"naifahamu hiyo methali, ila sijaelewa una maana gani"
"namaanisha, ukitaka mafanikio usichague kazi ya kufanya maana huwa kiwango cha elimu cha kukufanya uchague kazi"
"siwezi kuchagua kazi, siku nikiipata nitajibidiisha sana ili nibadili maisha yangu na ya wazazi wangu" "usijali, keshokutwa nitakupeleka kwa muhindi mmoja ambaye aliniahidi kuwa atakupatia kazi"
"nitashukuru sana dada"
Siku aliyoahidiwa kupelekwa kwa muhindi ikafika, walipofika walipokelewa na mtu ambaye Kibe alifahamishwa kuwa ndie atakaye mpatia kazi.
" bwana Kanjubai, kama nilivo kueleza kijana ndie huyu, baba na baba yangu wametoka tumbo moja, baba yake ndiye mkubwa kwa baba yangu"
hayo ni maneno aliyosema Teresia baada ya kukaribishwa ndani na kukaa.
Kanjubai naye akasema,"basi mimi nimeona yeye, nilipoona umekawia kumleta, nikafikiri pengine wewe ilidanganya mimi"
"kwanini nikudanganye bwana Kanjubai?,nilikuwa nasubiri azoee mji, unajua hajawahi toka kijijini toka azaliwe"
"ooh! okay,basi natumai yeye iko zoea sasa mji"
"si saana, ila ana ndoto ya kufanikiwa maishani, anataka awe na nyumba nzuri hapa mjini"
Wakati wote huo Kibe alikuwa amekaa kimya akisikiliza mazungumzo kati ya Teresia na Kanjubai, aliposikia Teresia akimueleza Kanjubai juu ya ndoto yake, akatabasam,Kanjuubai akamuangalia kisha akamuambia,
"kama wewe iko na ndoto ya kuwa na maisha zuri, usiwe vivu maana wazungu
wanasema, work like bee and eat honey or work like fly and eat waste" Ikawa zamu ya Kibe kuongea,
"nitajitahidi kadiri ya uwezo wangu kufikia hayo malengo yangu"
Teresia akasema, "sasa bwana Kanjubai,mie ngoja niende tutaonana siku nyingine kunielezea mambo yatakavyokuwa yamefikia, Kibe, wewe utabaki hapa maana Kanjubai anataka akufunze kazi kwanza kabla ya kukuajiri"
"sawa dada,hakuna shida,maadamu kazi ndio nimeifata huku mjini,hakuna shida nitabaki"
"sawa, kwaheri bwana Kanjubai"
"kwaheri Teresia, mimi tapigia wewe kukufahamisha kijana anavo endelea"
Baada ya Kibe kula chakula cha mchana, akapelekwa katika chumba chenye kitanda pekeyake na hicho kitanda kilikuwa katikati ya chumba, akaambiwa apumzike humo hadi hapo atakapo hitajika.
Baada ya mlango kufungwa Kibe akakaa katika kile kitanda, akasikia mdundo wa muziki lakini hakujua ulikuwa unatokea wapi maana hakuona redio humo chumbani,akaamua kujilaza kitandani huku akifikiria,'kweli pesa ni sabuni ya roho, kitanda kizuri kama hiki ukute hakuna hata mtu
anayekilalia'. Kibe akawa anasikiliza kwa makini maneno ya muziki uliokuwa unasikika humo chumbani,
"i'm the worm that cometh, iam him, iam hell, i'm the devil all in one, the eyes that hide the face inside come stare into my eyes. A killer is listening to horrors in my head.. He is bleeding, sliding on the razor's edge.. All pigs die, iam hell Godless , me iam pagan idolatry, kneel before the horror"
Hayo ni baadhi ya maneno yaliyo kuwa katika wimbo huo. Japokuwa Kibe hakuelewa maana ya maneno ya wimbo huo, hakuupenda. Usiku ulipo ingia,Kibe aliletewa chakula,akaambiwa ale na alale maana kesho yake watasafiri kuelekea sehemu ya kazi. Asubuhi na mapema,Kibe aliamshwa na mtu ambaye toka alipofika jana hakuwahi kumuona, alikuwa amevalia suti nyeusi na miwani mieusi.
"we dogo amka twende,utafurahia kitanda chako pindi utakapo kuwa na pesa"
hayo yalikuwa maneno ya huyo mtu aliyekuwa amevalia suti nyeusi. Kibe akaamka,akapelekwa bafuni akaoga kisha akapewa chai ya rangi na maandazi makubwa mawili. Alipo maliza kula, Kanjubai akaingia pale alipokuwa Kibe, akamuambia,
"Kibe,huyu anaitwa Moris, yeye atapeleka wewe sehemu ya kazi, kuna nguo yoyote ulikuja nayo tofauti ya hiyo ulio vaa?"
Kibe huku akimuangalia huyo jamaa mwenye suti nyeusi na miwani
myeusi, ambaye anaitwa Moris kama alivoambiwa na Kanjubai, akajibu,
"sikuja na nguo nyingine"
"basi hakuna shida, nguo utapata huko, haya Moris mpeleke na ukifika uniambie jinsi kazi inavokwenda"
Moris akasimama nakusema,
"hakuna tabu boss, kila kitu kitakuwa shwari, twende dogo".
Kibe akasimama na kumfata Morisi, wakaingia katika gari aina ambayo madirisha yake yalikuwa na giza, kisha wakaanza safari ndefu ambayo hakujua wanapoelekea. Walisafiri siku nzima bila kusimama, walitoka sehem ya mji wakaingia mbuga,giza lilipoingia, Moris akapaki gari pemben ya barabara na kumuambia Kibe,
"tutapumzika hapa na afajiri tutaendelea na safari". Kibe huku akipiga miayo, akauliza,
"ina maana bado hutujate kufika?"
"bado sana,tukijitahidi kuwahi kesho asubuhi, pengine mpaka usiku saa nne au tano tutakuwa tumefika, kula chakula upumzike maana najua hujazoea safari ndefu"
"sasa tulala wapi?"
"lala kiti cha nyuma, mie nitajinyoosha hapa nilipokaa".

Safari ya kwenda kazini ndio hiyo imenza, Je kibe anapelekwa wapi? Kanjibai na Moris ni nani?usikose sehemu ya tatu ya hadithi hii iliyojaa uhalisia wa maisha ya kijana wa kitanzania...Je ni kweli Dunia ni Rangi Rangile?...itaendelea wiki lijalo..jumatatu kama ya leo..Unaweza kuandika maoni ako hapa chini kuhusiana na hadithi hii...je inakupendeza na kukuvutia?

No comments:

Post a Comment