Wednesday, September 26, 2012

"MZIGO WA LAWAMA"




Ni wewe! Sio mimi! Kama sio wewe ni yeye! Sio sisi ni wao!  ni baadhi ya kauli za mkwepaji na wakwepaji wa lawama, hakuna anayependa kuubeba mzigo wake hata kama ni wa uzito wake, hata kama ameujaza mwenyewe. Katika kitabu kitakatifu cha biblia kuna mstari unasema"kila mtu atabeba msalaba wake" na katika kitabu kitakatifu cha Quran kinasema "hata kama ni mdogo mithili ya mdudu sisiminzi ni wakwako utapimwa na utapata malipo yako kwa ujazo wake". Ila je uko tayari kuubeba mzigo huu?

Binadamu huwa tuna hulka ya kukataa uhalisia, ila kwakua kuna ukweli ambao hauwezi kua uongo na uongo ambao hauwezi kua ukweli, basi tujue kuwa tutaubeba tu. Tazama Mfano huu
      "Mbegu ya mti inawekwa kwenye udongo wenye rutuba, kisha inawekewa mbolea ili ikue na ichanue na ili uwe mti bora na wenye afya inabidi utunzwe kwa makini, kama ni mti wa matunda basi utoe matunda bora na kama ni wa kivuli au mbao basi uweze kukidhi mahitaji ya aliyeweka mbegu ile. Mti huu utakutana na dhahma mbalimbali kama vile mvua, upepo, jua, moto hata kufikia kukatwa na watumiaji kwa matumizi yao".

Ila je unatambua kua wakati wa mvua mti huu huvumila sio kwakua hauna mahali pakujikinga bali umekubaliana na hali halisi, iwe mvua liwe ni jua kali mti huu utavumilia, upepo mkali utapita na hata kama moto utatokea mti huu utabaki palepale. Sasa nikuulize wewe, ninyi na wao Je!  uko/mko tayari kubeba lawama za mti kama mti ukitaka kulalamika? Jiulize kama mti ungekata tamaa kwa changamoto mbalimbali katika ukuaji wake Leo ungepata matunda yaliyo bora kutoka katika mti bora? Je Leo ungepata kivuli? Leo ungejivunia mbao za mninga?

Kilichopangwa kutokea hutokea, kilichotakiwa kufanyika hufanyika, palipokosewa hurekebishwa, tunajifunza kwa makosa, tunakuzwa kwa mafunzo, tunafunzwa na matatizo. Mzigo wa Leo ni bora kuliko wa Kesho, uzito wa Jana ni mwepesi kuliko wa Leo, wa Leo ni mzito kwakua upo nao Leo. Huwa tunadhani kwamba matatizo ndiyo yanyotunyima kuchanua na kusahau ya kua jua, mvua na upepo ndivyo vinavyosaidia katika uchavushaji na ukuaji.

Kiukweli palipo na uchanya uhasi lazima uwepo, palipo na ubaya pana uzuri, hizi fikra za kweli palipo na ukweli. Tambua pale unapolalama kwa uhasi unajinyima nafasi na wakati mzuri wa kutafakari uchanya wa mambo. Mfano kama mti ungekua unalalama na kutoa visingizio, je ni nani angekubali kubeba lawama zake?

Jiulize pale unapokosea au unapokosewa kuna umuhimu wa kumbebesha mtu lawama? Mimi nadhani cha muhimu ni kutazama palipokosewa kisha kujifunza na kurekebisha kosa hilo kwa pamoja. Tusipoteze muda wa kutafakari nini kifanyike kwa kung'ang'ania kumtafuta mtu wakumbebesha lawama. Kinyume na hapo basi sintopenda niubebe mzigo huu wa lawama kwakua Kumkichwa ni wewe!

No comments:

Post a Comment