Monday, September 24, 2012

"Chini ya Jua Nimeweza"



Maswali mengi yaliibuka,yameibuka na mengine yataibuka, kivipi ameweza?..ila jibu ni moja tu..kumkichwa ni wewe!

Hakuna asiyeweza, hata asiyeweza anaweza kwa kukubali kua hawezi. Maisha ni safari na safari yoyote huanza kwa hatua, je uko tayari kupiga hatua ya kwanza? je umeshapiga hatua ya kwanza? Je umeangalia umbali wa unapoelekea au umbali wa ulipotoka?..

Umakini ni kitu cha muhimu sana ila upendo ni kitu kizuri zaidi. Je unapenda unachokifanya kwa umakini? je unafanya kwa umakini unachokipenda?. Jana inatofauti na leo na leo sio sawa na kesho, muda unatuacha, muda uko makini, muda haupotezi muda, je muda wako unautumia kwa umakini?.

Tumeumbwa kisha nasi tukaunda, tunaunda kwakua tumeumbwa na akili, tumepewa uwezo wa kufikiria ndani na nje ya sanduku. Kilicho nusu kinaweza kua kimejaa nusu au kimepungua nusu. Uamuzi ni wa fikra zako kwa macho na masikio yako.

Unaamini au unajiamini ni juu ya imani yako, je unaweza, umeweza au utaweza?hiyo ni siri yako ndani yako juu ya uwezo wako na mapungufu yako. Hakuna kinachoshindikana chini ya jua. Visingizio na lawama havina tija zaidi ni hasara na kupoteza uaminifu juu yako. Unapoaminiwa kisha ukavunja uaminifu haimaanishi aliyekuamini ni mjinga kwa kukuamini, bali amekupa kitu usichostahili kupewa"uaminifu".

Kwa uaminifu chochote hufanikisha, imani yao kwako ndio mwanzo wa yote, fikra zao kwako ndio muendelezo wa yote, mafanikio yao kupitia wewe ndio mafanikio yako wewe. Uamuzi ni wako kufanikisha kwa kujenga ama kufanikisha kwa kubomoa. Safari hii sio lelemama, inahitaji upeo wa kuona mbali, kutazama zaidi ya ulipotoka na ulipo. Safari ya kujua nini kinachohitajika lakini kimekosekana, safari ya kuacha fikra mimi na kufuata fikra wao ndani ya mimi.

Wengi wao watafurahia na kukupongeza kwa hatua uliyofikia, na baadhi yao wataenda kinyume nao, ila wewe unajionaje?, unaweza ukaonekana paka mbele za watu lakini kumbe wewe ni simba! Au ukaonekana simba kumbe wewe paka! Wewe ama wao?, heshima bora huja baada ya dharau. Wewe unataka ipi?

Nilipogundua kua naweza kusema siwezi, nikajiuliza je ni siwezi kusema naweza au naweza kusema siwezi? Hapo ndipo nilipochanganyikiwa, nikaona nifanye kwanza kisha matokeo yatadhihirisha kua naweza ama siwezi?

Je naweza? Je siwezi? Haya ni maneno tu, vitendo ndio vina majibu sahihi, anayekuambia kua hauwezi ni yeye aliyesema sio wewe! Amua kwakua mimi najua unaweza kwakua mimi nimeweza basi hata wewe unaweza. Kumbuka wote tuko chini ya jua, wote tuko chini ya mwanga unaotuongoza. Tambua unachokipenda kukifanya, kisha fanya unachokipenda kwa moyo wako wote(100% ),weka firka zako zote, weka nguvu zako zote. Gusa kiini cha uwezo wako kwa nia moja ya kwamba unaweza, umeweza na utaweza. Mwanzo huwa ni mgumu kwakua hatujui mwisho utakuaje!..ndio maana kunakitu kinaitwa Tumaini..usipoteze Matumaini, usikate tamaa kamwe, ukianza anza hakuna kurudi nyuma,ukiteleza amka jipanguse kisha endelea..hatuviiti vikwazo bali ni changamoto na huu ndio utamu wa safari hii..mpaka hapa nilipofika katika safari hii ni changamoto ndio zimenijenga kutoka siwezi mpaka naweza....hata wewe ukiamua utaweza kwakua hakuna kinachoshindikana chini ya jua..Kumkichwa ni wewe!

No comments:

Post a Comment