Tuesday, October 2, 2012

DUNIA RANGI RANGILE ( 4 ) Sehemu ya Nnena Lasima Nassoro


Je haya ni majani gani ni shauku ya Kibe kutaka kujua...! je nini kitamtokea kibe wakati yuko mbali na nyumbani kwao? endelea kufuatilia hadithi hii?..
       Kadiri siku zilizoendelea, Kibe alizidi kuwa na shauku ya kujua yale majani wanayotwanga kila siku yana kazi. Akaamua kujenga mazoea na kijana mmoja kati ya wale waliokuwa wanakuja jioni kuchukua yale majani waliokuwa wakiyatwanga, aliyekuwa anaitwa Fabian. Siku moja baada ya kumaliza kazi, Fabian na wenzake waliwasili kuchua mzigo wa siku hiyo, Kibe akamfata Fabian,
"mambo vipi Fabi?".
"ooh mtoto wa sisi kwa sisi, bado upo tu hapa hujaenda kujipumzisha?".
"si nilikuwa nasubiri nikuone, au hujui kuwa tushakuwa marafiki?".
"nani kakuambia mie rafiki yako?".
"acha hizo mtu wangu, urafiki si wa kuambiwa, huanza tu wenyewe bila kutambua".
"nilikuwa tu nakutania, mambo poa kama uonavyo tunawajibika".
"unajua Fabi, kuna mambo yanasumbua akili yangu, na nafikiri pengine wewe unaweza kunipatia majibu".
"kama nitakuwa na jibu nitakuambia, ni nini hicho kinachokusumbua?".
"hebu twende tukakae chini ya ule mti pale".
Wakaenda hadi katika mti mkubwa wa ukwaju , wakakaa katika magogo yaliyokuwa chini ya ule mti. Kibe akakohoa kidogo kisha akasema,
"kwanza nakuomba uniapie na kuni ahidi kuwa haya nitakayokuuliza hutamuambia mtu yoyote".
Fabian akamuangalia Kibe kwa sekunde kadhaa bila kusema kitu kasha akatabasam na kusema,
"kwani unataka kuua mtu hadi uniapishe?".
"nipo siriasi Fabi, kuna saa ya utani lakini huu sio utani".
"sawa, naapa kwa jina la Mwenyezimu na jina la Mama yangu aliyenizaa, utakalonieleza litaishia hapa".
"sawa,  jambo lenyewe ni kuhusu hii kazi tunayoifanya".
"una maana gani ukisema kazi tunayoifanya?".
"nina maanisha haya majani tunayoyatwangwa kila siku, yana kazi gani?".
"nani aliyekutuma kuulizia mambo yasiyokuhusu?".
"kuuliza sio ujinga na hakuna aliyenituma, tafadhali kama wajua niambie".
Fabian akakaa kimya kitambo bila kusema kitu huku akitafakari kuwa amuambie Kibe au la na je akumuambia, ataweza kuchunga ulimi wake bila kumwambia yeyote?. Kibe alipoona Fabian hasemi chochote, akamwambia,
"nilifikiri wewe ni rafiki yangu wa kufa na kuzikana ila naona huna imani na mimi, tusahau kama nilikuuliza swali kama hilo".
"umeniuliza swali ambalo kwangu ni gumu sana na majibu yake sio rahisi kama unavyofikiria".
"nilifikiria utanipatia majibu ya mambo yanayo nitatiza kumbe sivyo, nitatafuta majibu toka kwa mtu mwingine".
Baada ya Kibe kusema hayo, akanyanyuka toka pale alipokuwa amekaa na kuondoka. Fabian alipoona Kibe amesimama na kuondoka nae akasimama na kupiga hatua za haraka ili kumfikia, alipomfikia akamshika bega na kusema,
"nipe muda nitafakari uliyonieleza, ila usije ukamuambia yeyote kuwa umeniuliza swali kama hilo, sawa?".
"poa, mie sina shida hapo utakapona umefikiri vya kutosha utaniambia".
Fabian akawafata wenzake na kumalizia kupakia mizigo katika gari kasha wakaondoka. Baada ya Kibe kuachana na Fabian, alijaa mawazo, alikuwa akiwaza Fabian alivyosema, na kujiuliza kuwa Fabian alikuwa na maana gani alipomuambia, 
‘usifikiri ni jibu rahisi kama anavyofikiria’, 
ina maana ninavyo hisi kuwa kuna biashara haramu inayofanyika hapa ni kweli?,
 'eeh Mungu nipe ujasiri na uwezo wa kufumbua mafumbo kama alivyokuwa mfalme Suleiman'. 
Siku ile Kibe alichelewa kwenda kulala baada ya kula chakula cha usiku, alikuwa anawaza namna ya kumshawishi Fabian ili amtegulie kitendawili kile lakini hakupata jibu. Kesho yake Kibe alikuwa wa kwanza kufika katika kituo chao cha kazi, nia yake ilikuwa  kuchunguza yale majani wanayotwanga kila siku kama anaweza kuyatambua. Wakati anaendelea kuchunguza wazo likamjia kuwa pengine yale yalikuwa majani ya bangi ,moyo ukamuenda mbio baada ya kukumbuka kuwa kuna siku alihisi harufu ya bangi pale karibu na wanapolia chakula, alipofuatilia akagundua kuwa aliyekuwa akivuta hiyo bangi alikuwa boss wao, Lio.
 'kama hii ni bangi, kwanini inatwangwa?', Kibe aliwaza. 
Baada ya wenzake kuwasili wakaanza kumtania, 
"imekuaje leo umewahi hivyo?, unafikiri utapandishwa cheo na kwenda kule katika kitengo cha kuchemsha?". Huyo alikuwa kijana aliyeitwa Omondi, akaendelea kumwambia Kibe,
"wenzako tumekaa miaka mingi hapa lakini hakuna kubadilishwa idara wala nini".
Kibe akamwambia,
"kila wakati huwa nachelewa, leo na mimi nimeamua niwahi, si unajua kuwa ada ya mja hunena , muungwana ni vitendo, hivyo nataka boss ajue kuwa nimekuja hapa kwa shughuli moja tu,
'KAZI'.
Wakati wanaendelea na kazi, Kibe akawa anafikiria Omondi alivyosema, 'unafikiri utapelekwa kitengo cha kuchemsha?'. Wafanyakazi wenzake walikuwa wakiongea na kucheka, huku Kibe akijiuliza, 'hivi bangi inachemshwa?, na kama inachemshwa, inachemshwa ili ifanyiwe nini?'. Wakati wa chakula ulipofika, Kibe akamuona Moris, ilikuwa mara ya kwanza kumuona toka siku ile walipoachana pale kwa Lio, akaenda kumsalimia. Moris akamuambia,
"yaelekea umeshazoea mazingira".
"nashukuru nimezoea, je umewahi kumuona Dada Teresia?".
"nina muda sijaonana nae ila mkuu Bwana Kanjubai alionana nae juzi, akamuambia mwisho wa wiki hii atakwenda kijijini kwenu hivyo kwa kuwa nilikuwa na safasi ya kuja huku, akaniambia nikuone kama una pesa za kuwatumia wazee wako unipatie ili kesho kutwa Alhamisi Teresia akija kumuona Bwana Kanjubai, ampatie".
"nitakupa kabla hujaondoka".
"sawa, fanya hivo maana sina muda mrefu hapa, nataka leo hii hii nirudi mjini".
Kibe akakimbia kwenda katika makazi yao kuchukua pesa za kuwatumia wazazi wake.
"kama utamuona dada Teresia, mwambie awape wazazi wangu salamu zangu".
Kibe alimuambia Moris baada ya kumkabidhi pesa za kuwatumia wazazi wake. Moris akaondoka na kwenda kwa Lio, alipofika akamkuta akipika chakula cha mchana, akamuambia,
"sasa Lio, mie nataka nirudi maana huu mzigo unatakiwa kama itawezekana, kesho usiku uwe umewasili visiwa vya Komoro".
"boss, subiri walau msosi uive ule ndio uondoke".
"hapana, hata hivyo nimechelewa, kwani kuna shida yoyote ambayo unahitaji usaidizi?".
"kwa sasa hakuna ila wakati mwingine utakapokuja, naomba uniletee mifuko ya kupakia mzigo maana iliyopo inakaribia kwisha".
"hilo halina shida, mafuta taa, asidi na vimiminika vingine vipo vya kutosha?".
"afadhali umenikumbusha, haidrokloriki asidi, imepungua na ile kama unavyojua ndio muhimu zaidi ili kufanya mzigo uwe wa daraja la kwanza, ethanol japo haijapungua saana niyakuongeza pia".
"poa, hayo nimeyasikia, ikiwezekana kesho usiku hivyo vitu vitaletwa hapa, na usisubiri hadi malighafi ipungue, kuna soko jingine mkuu anafuatilia, hiyo dili ikikubali utafurahi mwenyewe".
"shaka ondoa boss, unajua hizi shughuli zetu zinatakiwa kujipanga kimaisha wakati muda haujayoyoma".
"una maana gani? ,usiniambie umeanza kuingiwa baridi".
"hahaha, mimi Lio, The Lion of Juda, niingie baridi, hilo halitowahi tokea, mie ni mkongwe katika hizi shughuli, nilichokuwa namaanisha nikuwa, twajua ya leo, yakesho hatuyajui hivyo mtu unatakiwa upigane leo ili kuijenga kesho".
"kwani siku hizi, busara unazitoa wapi?".
"usitake nicheke boss, kama nisingekuwa na busara unafikiri Mkuu angeniweka sehemu nyeti kama hii?, hapa panatakiwa akili na busara na ujanja pia".
"ila si unajua kuwa unapoingia katika hizi kazi, ni ngumu kutoka?, na kama ukiamua kutoka huo ndio mwisho wa kula ugali hapa duniani?".
"mbwa hafundishwi kunusa boss, hilo nalitambua kama kiganja changu".
"poa kama walitambua hilo,ngoja mie niwahi,nitakuja baada ya siku mbili, ila kesho hizo malighafi zinazohitajika zitaletwa".
"poa, safari njema, siku ukija nakuomba uniletee walau kreti mbili za bia".
"we si umezoea kunywa gongo, ukinywa bia siutalazwa hospitali?".
"utani huo boss, we fanya hivyo ikiwezekana uniongezee na chupa moja ya whiski".
"poa, kwaheri ila usiwe unakunywa tu pombe hadi usahau jukumu lililokuweka hapa".
"shaka ondoa, boss".
Moris alipofika mjini, bwana Kanjubai akamuambia ajiandae kwa safari ya kuelekea visiwa vya Anjuani.
"sasa boss, nitatumia usafiri gani?", Moris alimuuliza Kanjubai.
"kwani wewe iko sahau kuwa nimenunua boti mpya juzi juzi?, hiyo ndiyo utatumia, utaandamana na vijana wa kazi, nawe pia usisahau bastola yako, you know just in case yakiharibika, uwe na silaha ya kujitetea".
"sawa, na huyo jamaa wa huko Anjuani umeshawasiliana naye?,  maana nataka
nikifika tu kama mipangilio itakuwa sawa nataka nigeuze".
     Je haya ni majaani gani na ni mzigo gani unaopelekwa Visiwa vya Anjuani?..je Moris atafanikiwa?...je nini kitamtokea Moris?.... endelea kufatilia hadithi hii?...

No comments:

Post a Comment