Monday, December 17, 2012

DUNIA RANGI RANGILE (11) Sehemu ya Kumi na moja NA YA MWISHO


                                   Mtunzi: Lasima Nassoro
  Samson alipokuwa katika mgahawa wa Makonde, alimuona  mtu akiingia,lakini  alikuwa hakumbuki vema kuwa alimuona wapi, alipomaliza kula na kulipa,akamkumbuka yule mtu aliyemuona akiingia pale mgahawani, roho ikamuenda mbio alipokumbuka kuwa yule jamaa anaitwa Cosmo,na alikuwa mtu mwenye roho ya ukatili sana, "huyu jamaa najua tu ametumwa na Kanjubai, kilichopo hapa ni kuhama usiku huu huu, maana kama ameshajua nilipofikia, anaweza akanidhuru au apotee na pesa zangu", hivyo ndivo Samson alivokuwa akiwaza. Alipofika hoteli aliyofikia,akachukua mizigo yake na kwakuwa alikuwa hadaiwi, akarudisha funguo na kuondoka. Akakodisha teksi yakumpeleka kituo cha mabasi, alipofika kituoni akakuta kuna basi moja ambalo lilikuwa halijajaa na lilikuwa linaelekea Harare. Akatabasam, huku akijisemea, 'kwaheri Cosmo, sijui utamuambia nini Kanjubai utakapogundua kuwa nimetoweka?',akakata tiketi na kwenda kukaa kiti cha nyuma kabisa,dirishani. Kibe alianza kuona matunda ya kazi yake baada ya kuanza kuuza, karoti, nyanya na vitunguu. Watu wengi wakawa wanakwenda kununua mbogamboga kwa Kibe, maana hakutumia kemikali za kuulia wadudu bali alitumia aina ya majani ya miti aliyokuwa ameonyeshwa na marehemu baba yake, haya majani aliyatwanga na kuweka mimea yake na mazao yakawa mazuri. Kibe alipoona amepata pesa nzuri, akaamua auze baadhi ya mifugo ili apate pesa ya kutosha kununua ng'ombe wa kisasa wa maziwa. Akajenga vizuri sehemu atakayo muweka ng'ombe wake wa maziwa, juu akaezeka kwa makuti. Alipokamilisha banda la ng'ombe,kama alivoelekezwa na mtaalamu wa mifugo, akaenda katika ranchi ya kituo cha mifugo kuangalia aina ya ng'ombe atakayo weza kununua. Alionyeshwa aina tofauti ya ng'ombe,akaelezewa kila aina ya ng'ombe na kiasi cha maziwa anachotoa kwa siku. Kibe akachagua ng'ombe aina ya Freshan,ambaye alikuwa na mimba ya miezi mitano. Siku moja Kibe alipokuwa amejipumzisha baada ya shughuli zake za mchana kutwa kumalizika,alikuja mjumbe wa nyumba kumi kumuelezea kuwa kuna mtaalamu atakuja pale kijijini kwao kesho yake ili awaelimishe wanakijiji kuhusu matumizi ya bio gas. Kibe akashangaa na kumuuliza yule mjumbe, "hii baio gesi,ni gesi ya namna gani?,isije ikawa ni hizi gesi zinazo choma nyumba huko mijini?". Mjumbe akamwambia,"kwa uelewa wangu mdogo ni kuwa, hii ni aina ya gesi itokanayo na kinyesi cha wanyama". "basi kama ni hivyo,nitakuja ila baada ya kupunguza kazi zangu". "sawa ila usichelewe maana unaweza ukakosa yale ya muhimu". Kibe alipoenda katika ule mkutano, alijifunza mambo mengi mazuri ya maendeleo, akaahidi kuwa lazima abadilishe maisha ya pale nyumbani kwao. Walielekezwa namna ya kutengeneza mashimo ya kuweka kinyesi cha ng'ombe na mashimo ya kuhifadhia gesi ile itakayotokana na kil kinyesi cha ng'ombe. Ilikuwa imepita miaka miwili toka Kibe aanze kuona mafanikio ya kazi zake, alikuwa amejenga nyumba nzuri ya matofali ya kuchoma,hakuwa anaenda tena machungani maana akifuga ng'ombe wa kisasa wa maziwa na mbuzi watatu wa maziwa,ambao alikuwa akiwamudu kuwalelea majani pale nyumbani, pia alianza kutumia bio gas, na alikuwa amenunu tv yake ndogo maana alikuwa anapata umeme wakutosha uliotokana na bio gas, mama yake alikuwa ameshaanza kusahau matumizi ya kuni maana alikuwa akipika na gesi itokanayo na kinyesi cha wanyama. Ilikuwa siku ya jumamosi jioni,Kibe akiwa anatazama taarifa ya habari, akaona habari iliyomustua, akamuita mama yake ili nae aione, habari yenyewe ilikuwa hivi, "JESHI LA POLISI LIMEFANIKIWA KUWATIA MBARONI WATU KADHAA KWA KUJIHUSISHA NA BIASHARA YA MADAWA YA KULEVYA, KUKAMATWA KWAO KUMEFANYIKA KUTOKANA NA UPELELEZI WA MUDA MREFU ULIOFANYA NA KACHERO AJULIKANAE KWA JINA LA FEDINAND, KACHERO HUYU BAADA YA KUGUNDUA KUWA KUNA SHAMBA LA MMEA AINA YA COCA ENEO LIJULIKANO KAMA TAMBAENI, MMEA HUU NDIO UNAOTUMIKA KUTENGENEZEA DAWA AINA YA COCAIN", taarifa ikaendelea kuelezea, "JESHI LA POLISI LILIPO VAMIA ENEO HILO KULITOKE MAJIBIZANO YA RISASI AMBAPO WATU WATATU WALIUWAWA,  AKIWEMO MTU MSAIDIZI WA KANJUBAI AITWAE LIO", msoma habari pia akataja majina ya watu waliokamatwa ambao walikuwa wakishirikiana na bwana Kanjubai, miongoni mwao ni, "TERESIA KABORONGA, MORIS TENDAWEMA, TWALIBE IBRAHIM". Kibe akafunga macho na kuziba uso wake kwa viganja vyake, mama yake akamuuliza, "nimesikia jina la Teresia likitajwa hapo, ina maana na yeye alikuwa anauza dawa za kulevia?". "sijui mama, ila pengine alikuwa anauza maana alikuwa anafahamiana vema na hao watu, na hapo walipotaja kuwa hizo dawa zilikuwa zinatengenezewa, ndio nilipokuwa nafanyia kazi". Marina kusikia vile akahamaki, "mbona tuliambiwa na Teresia kuwa ulikuwa ukifanya kazi kwa muhindi?". "ndio nilikuwa nikifanya kazi kwa muhindi ambaye ni huyo bwana Kanjubai ambae polisi wamesema kuwa hawajui alipotorokea". "kwahiyo nawewe ulikuwa ukiuza hayo madawa?". "hapana,kwanza mimi hata nilikuwa sielewi kilichokuwa kikiendelea". "una maana gani ukisema ulikuwa hujui kilichokuwa kikiendelea?". "mimi kazi yangu ilikuwa kutwanga hayo majani na kila nilipo wauliza wenzangu kuwa yale majani tuliyokuwa tukitwanga kila siku yalikuwa na kazi gani?,walikuwa wananijibu kuwa nisitake kujua,eti mie nilichofata pale ni pesa tu". Marina aliposikia kuwa mwanae hakujua kuwa anafanya kazi ihusiyo dawa za kulevia,roho ikamtulia,akamuliza Kibe,"sasa ulijuaje kuwa hayo majani yalikuwa ya hayo madawa?". "kuna rafiki yangu mmoja, anaitwa Fabian,yeye alikuwa kitengo kingine tofauti na kitengo chetu,huyu ndie alinielezea yanapopelekwa yale majani baada ya kutwangwa na kitu ambacho kinatengenezwa huko ambayo ndio hiyo cocain waliyoitaja,niliambiwa hivo nilijiapia kuwa kama nitapata nafasi ya kuondoka pale,sitorudi tena". "sasa nimeelewa kuwa kwanini ulikuwa hutaki kurudi, ila kwanini hukuniambia?, ulinifanya niwe na mawazo kuwa pengine umeharibu vitu au umeiba pesa za watu ndio maana hukuwa unataka kurudi huko". "nisamehe mama maana nilimuahidi huyo rafiki yangu kuwa sitomuambia mtu yeyote, maana siri ingetoka halafu waseme ni mimi niliyeitoa, wasingesita kunisaka na kuniua". Marina akarudi jikoni kuendelea kutayarisha chakula cha usiku. Kibe alifuatilia ile habari lakini hakusikia Fabian akitajwa kuwa amekamatwa, pia hakusikia jina la mumewe Teresia likitajwa ,akawa anawaza, 'pengine Fabi aliamua kuacha na Samson, sijui alikuwa anajua kuwa Teresia anauza cocain?, au nayeye alikuwa muuzaji na wakati wenzake wanakamatwa hakuwepo maana anasafiri kila wakati'. Kibe alipoona hakuna kitu cha kumfurahisha katika tv, akaamua kuizima na kufungulia redio ,akatafuta stesheni yenye muziki, akawekea stesheni yenye muziki uliokuwa ukiimba hivi, "hata uwe mzuri wakupindukia aah, tabia yako ikiwa mbaya ni bure kabisa... "hata ujipambe kwa vito ung'ae kama nyota aah,tabia yako ikiwa mbaya ni bure kabisa... "hata uwe na maringo, utembee kama twiga,mtabia yako ikiwa mbaya ni bure kabisa,tabia njema utakwenda popote, heshima kijana, tanguliza kwanza mbele ujeuri m'baya ooh". Kibe wakati anaendelea kusikiliza muziki,akasikia mama yake akimuita aende kula. Kibe alipofika jikoni akakuta mama yake amepika chapati za kusukuma na kuku wa kienyeji aliyeungwa kwa kweme, pia alikuwa amepika chai nzito ya maziwa. Kibe akatabasam, akatamani kama baba yakeangekuwepo, akamuambia mama yake, "mama, kweli dunia ni rangi rangile, leo hii sisi ndio tunakula chapati kama chakula cha usiku?,mtu angesema miaka mitano iliyopita kuwa ipo siku ambayo tutakula hivi na kuishi katika nyumba kama hii yenye umeme,nisingekubali hata kwa mtutu wa bunduki". Marina akatabasam, huku akiweka mboga kitika bakuli la kibe, akamuambia,"hakuna lenye mwanzo lisilo na mwisho,na maisha ni kupanda na kushuka". "kweli mama,kilichobaki sasa nitafute mchumba nioe, nataka hii nyumba ijae kelele za watoto". "nafurahi kama umelitambua hilo mwanangu, na nakuombea kwa Mungu akupe mke mwema". "amin,amin mama,INSHAALLAH mungu apokee dua zako".
                                                         ~ ~ MWISHO ~ ~

No comments:

Post a Comment