Wednesday, December 19, 2012

Teknolojia hizi na Kizazi hiki.




               Nakumbuka miaka ya Tisini kuelekea elfumbili tulikuwa ni watoto wabunifu kweli kweli, kipindi hicho Runinga zilikua ndio zinaingia kwa wingi nchini kwetu. Na kutazama ilikua ni kwa ratiba, kwa wengine ni mpaka usome au ulale mchana. Yote haya ni malezi ambayo wazazi wetu walitujengea ili kutujenga kwa wakati huo. Na kwa baadhi yao asilimia kubwa nadhani wamefanikiwa kutupatia malezi bora.

             Sasa tokea kuingia kwa Runinga hadi sasa ni miaka kama kumi na tano hivi teknolojia ya simu zenye mtandao, computer, playstation(game) na mitandao ya kijamii imeshaingia na kusamba kwa kasi kwenye jamii zetu. Lengo la hii makala sio kuhoji uwepo wa teknolojia hizi bali ni kujua je matumizi yake yanazingatiwa katika kuijenga jamii iliyobora ama kinyume chake.

             Nakumbuka miaka hiyo ya tisini tulikua tunaipa Tv umuhimu mdogo sana ,ila michezo ya utoto tulikua tunaitilia maanani, tulitengeza magari, manati, baruti, nyumba za matope, tulijihusisha na michezo kama mpira wa miguu, rede, kombolela na mingine mingi. Yote hii ni katika kuichangamsha akili na kuifanya miili iwe katika afya njema.

            Leo hii ukipita mitaani huoni mtoto hata mmoja, ila ukifika sehemu wameandika "PLAYSTATION” "INTANET CAFE", "TUNAONESHA VIDEO HAPA"..utakuta watoto wamejazana. Watoto wamekua sehemu ya biashara, na baadhi ya wanajamii wanaitumia nafasi hii kutengeneza hela kwani hakuna anayejali kua kizazi hiki kinapotea.

            Labda tuseme kua tutapata kizazi bora cha teknolojia mpya au la hasha ni kupotea kwa kizazi bunifu. Nisingependa kugusia juu wa kutokujaa  nusu na kuacha kujaa nusu kwa bilauri hii ya maji ila kwa hali halisi ilivyo kuna umakini unatakiwa uzingatiwe ili kupata kinachokaribiana na ubora kama sio bora.

            Rai kwa wazazi na walezi ni umleavyo ndivyo akuavyo, na kila kitumiwacho zaidi ya kiwango basi kitaleta madhara, na pia kile kitumiwacho tofauti na malengo yake kwa uhasi pasi na uchanya pia kuna madhara yake. Uono wangu ni kua je tuko tayari kukabiliana na mabadiliko ya kizazi hiki cha teknolojia hizi. Kinachoruhusiwa kuingia katika akili ndio kinacholeta uzuri na ubaya, je ni kweli tutapata wabunifu, je tutajivunia matendo yao na tabia zao walizojifunza kwa kuona.

           Tusiache tu mambo yaende, tusifurahie tu mambo yanavyoenda eti kwakua sio kizazi chetu, tusijivue majukumu yetu bali tuhusike kikamilifu katika kujenga bora kwa ubora tunaoutaka sisi wenyewe. Walishasema sio mtoto wako ila ni mjukuu ndio majuto. Nakusihi uzingatie niyaonayo kwani wakati ukiwa wao hakuna kilichokibaya kwao, hivyo wanahitaji mwongozo kutoka kwako, wanahitaji ushauri wa ingekua mimi ningefanya hivi, wanahitaji ukaribu wetu kwao, wanahitaji hadithi za Mzee Matola, Awafu mwenye nguvu,  Fikiri kabla ya Kutenda, Adili na Nduguze.  Wafunzwe vyakuwajenga, wafunzwe kuwa wabunifu, wafunzwe kujiamini, wafunzwe kutambua baya na jema, ilmu ya duniani na ilmu ya imani. Tambua ya kwambwa kwa teknolojia hizi na kizazi hiki Kumkichwa ni wewe!

No comments:

Post a Comment