DUNIA RANGI RANGILE
(Sehemu ya Kwanza)
Mtunzi: Lasima Nassoro
"Uvivu ni adui mkubwa kwa ujenzi wa taifa, tena ndio usababishao njaa, ewe ndugu yangu… amka kumekucha , kamata jembe na panga twende shamba, ewe karani amka kumekucha kwani hizi ni saa za kwenda kazi, ewe mwanafunzi amka kumekucha chukua kalamu na kitabu uende shule". Huo ulikuwa wimbo uliokuwa unaimbwa redioni asubuhi na mapema, wakati huo bi Marina alikuwa amekwisha tayarisha uji na kiporo cha mihogo alichokuwa amemwekea mwanae. Akaenda chumbani kwa mwanae kumuamsha,
"Kibe , Kibe mwanangu"
"naamu" hiyo ilikuwa sauti ya Kibe akiwa bado ana usingizi.
"jitahidi baba uamke maana kumeshakucha"
Kibe akiwa bado ana usingizi, akajikokota kutoka kitandani na kumfata mama yake jikoni. "shikamoo mama"
"marahaba, umeamkaje?"
"nashukuru nimeamka salama, sijui wewe?"
"hata mie niamka salama, nenda ukanawe uso halafu uje upate staftahi maana saa zimekwenda"
"hata mie niamka salama, nenda ukanawe uso halafu uje upate staftahi maana saa zimekwenda"
"sawa mama,je baba bado amelala?"
"yupo macho, si unasikia redio inalia, msemeshe tu atakuitika". Baada ya kunawa uso, Kibe akaenda kumsalimia baba yake Mzee Sosongo kisha akaenda jikoni kufungua kinywa.
"sasa leo unaenda kuchungia upande upi?" Marina alimuuliza mwanae.
"hata sijajua maana siku hizi majani yamekuwa ya shida"
"hii mvua isiponyesha mifugo itapata sana shida"
Baada ya kumaliza staftahi Kibe akafungulia mifugo,
Baada ya kumaliza staftahi Kibe akafungulia mifugo,
"mama ngoja niende maana leo nimechelewa sana, na kwanini hukuniamsha mapema?"
"nafahamu kuwa unachoka sana mwanangu, ndio maana sikuwahi kukuamsha ili walau upunguze uchovu"
"ngoja basi mie niende, utaniagia kwa baba".
"haya, nenda baba na mizimu ya mababu ikulinde na lolote baya"
"taire mama".
"taire mama".
Kibe akaondoka na mifugo kwenda kutafuta malisho. Kibe alikuwa mtoto pekee wa Mzee Sosongo na Bi Marina, walikaa muda mrefu sana bila kujaaliwa kupata mtoto hadi wakakata tamaa maana walikuwa wameanza kuzeeka. Japokuwa Kibe alikuwa ndiye mtoto wao pekee, Mzee Sosongo na Bi Marina hawakudekeza mtoto wao. Mara zote walimuasa kuwa, uvivu ni adui wa maendeleo, na ili ufanikiwe lazima ujitume kwa moyo wako wote. Kibe aliporudi jioni kutoka machungani alikuta kuna wageni. Baada ya kuingiza mifugo zizini akamfata Mama yake jikoni..
"habari za kushinda mama"
"nzuri mwanangu, je wewe umeshindaje?"
"nimeshinda vema mama, ila nina njaa kweli, kuna chochote cha kula?"
"angalia hapo kwenye kitala nimekuwekea chakula, uje uchukue na maziwa ushushie"
Wakati Kibe anaendelea kula akamuuliza mama yake,
"hivi mama hao wageni wanaoongea na baba ni akina nani?".
Huyu wa kike si ni Teresia mtoto wa baba yako mdogo Kaborongo? na huyo mwanamme ni mumewe amemleta ili tumfahamu"
"nilishamsahau, ni muda mrefu umepita toka nilipo muona". "alikuwa anamwambia baba yako kuwa kwasababu umemaliza darasa la saba na hukuchaguliwa kuendelea sekondari basi uende nae mjini akakutafutie chochote cha kufanya".
"mie sitaki kwenda huko mjini, kwanza nikiondoka nani atakae kuwa anachunga mifugo?, umri wa baba umekwenda sidhani kama anaweza kukimbizana tena na mbuzi".
"baba yako bado hajaamua, alisubiri urudi kutoka machungani ndio akuelezee nawe pia utoe maoni yako".
"maoni yangu ni kuwa sitaki kwenda huko mjini, kwanza huyu dada mwenyewe sijamzoea sembuse kukaa nae?"
"subiri hadi baba yako atakapokueleza ndipo na wewe utoe maoni yako, na usije ukasema nimekueleza maana wamjua baba anavopenda kila jambo aanze yeye kulisema".
"sitamuambia, ngoja nikaoge maana baridi ikizidi kuniingia mwilini sitakoga tena"
"sitamuambia, ngoja nikaoge maana baridi ikizidi kuniingia mwilini sitakoga tena"
Mzee Sosongo akamuita mkewe baada ya wageni kuondoka. Mkewe alifika pale alipo mzee Sosongo akamkuta akikohoa, akasubiri hadi alipoacha kukoho,
"Baba Kibe, nimekuambia uache kuvuta sigara lakini hutaki, waona jinsi kikohozi chako hakiishi japo unakunywa dawa kila
siku?"
siku?"
"Mama Kibe, hiki ninachovuta sio sigara bali ni kiko, 'KIKO' kwani huelewi?"
"kwani ukivuta kiko au uvute sigara, moshi si ndio unaingia mwilini mwako?".
"haya nimekusikia maana ukianza kuongelea kitu humalizi" "suala si kumaliza au kutomalizi, muhimu ni kuelewa na kuchukua hatua kwa yale uelezwayo"
"sawa mke wangu, nimekuelewa nitajihidi kujaribu kuacha, ila sio rahisi ufikiriavyo…sasa nilichokuitia hapa ni kuhusu haya huyu mtoto wa Kaborongo aliyotueleza, je wewe unafikiriaje!"
"sio wazo baya ila unatakiwa umueleze Kibe usikilize kuwa nayeye anaamuaje"
"Kibe bado mdogo, hajafikia umri wa kujiamulia mwenyewe, sisi ndio tunatakiwa tujadili kisha tumueleze tutakayoamua"
"sawa nimekuelewa, mfano tumeamua kuwa aende huko mjini, je ni nani atakuwa anachunga?"
"suala la kuchunga hilo halina shida, siku hizi kuna huyo kijana aitwaye Sereng'ei, huwa anachukua mifugo ya wale ambao hawana mchungaji na kuipeleka malishoni, na kila baada ya miezi mitatu unampa mbuzi jike au kondoo jike"
"sasa wewe unaamuaje? tumwambie aende huko mjini?"
"mie naona aende akaangalie kama atapata cha kufanya, pia kutamfanya alinganishe maisha ya mjini na ya huku kijijini,akiona kuwa maisha ya mjini hayampendezi basi arudi". Kibe alipoelezwa kuhusu maamuzi wazazi wake waliyofanya kuwa aende huko mjini, alipinga wazo hilo kama alivyomueleza mama yake pale mwazo walipokuwa jikoni. Mzee Sosongo akakohoa na baada ya kutulia akasema,
"mwanangu, tambua kuwa yote haya ni kwa ajili yako, ni kwa faida ya maisha yako hapo baadae, hakuna mzazi amtakiae mwanae mabaya, na furaha ya mzazi ni kumuona mwanae akifanikiwa kimaisha, hatuja kuambia kuwa ukienda huko mjini basi ukae huko huko na usirudi tena huku, hapa ni kwako na tambua kwamba, hakuna tembo alemewaye na mkonga wake".
"sawa baba nimekuelewa, nitakwenda, ila nikiona mambo hayaniendei vizuri nitarudi"
Mama yake ambae wakati wote huo alikuwa kimya, naye akasema,
"na hatuombi yakawe mabaya, baba yako atachukua maziwa ili aieleze mizimu ya mababu zako kuwa ikakutangulie na kukuongoza huko utakapo kwenda, si ndivyo baba Kibe?"
"ndivyo hivyo Mama Kibe, kipindi nikiwa na rika kama la Kibe ,baba yangu aliniambia kuwa, kama unakwenda safari ya mbali na unaondoka bila kuiambia mizimu, basi huko uendako hutafanikiwa".
Baada ya siku mbili kupita toka Teresia aje nyumbani kwa baba yake mkubwa Mzee Sosongo, akarudi tena kuwaaga. Teresia baada ya kusalimiana na Mzee Sosongo na mkewe bi Marina, akawauliza ,
"Kibe hajarudi toka machungani?"
Mzee Sosongo akasema,
"siku hizi majani yamekuwa ya shida sana, hivyo wanakwenda kutafutia mifugo malisho mbali, hadi afike hapa giza linakuwa limeanza kuingia".
Teresia akamuuliza tena mzee Sosongo,
"na mumejadiliana kuhusu yale
niliyowaeleza siku ile ya kuhusu kwenda na Kibe mjini?"
niliyowaeleza siku ile ya kuhusu kwenda na Kibe mjini?"
"ndio , tumejadiliana na Kibe amekubali muende wote".
"sawa baba, sasa mie kilichonileta hapa ni kuwaaga, kesho nataka nirudi mjini"
"na mumeo,mbona yeye hukuja kutuaga?"
"hajisikii vizuri, toka tumekuja amekuwa akisumbuliwa na homa, amenituma niwape salaam zake na anawaomba radhi kwa kushindwa kuja kuwaaga"
"ukifika mwambie tumezipokea na twamuombea apone".
"sasa baba,sikai sana maana mama ameniambia twende niwahi kurudi ili akanitolee mihogo kwenye lile shamba letu la kule bondeni, Kibe akirudi, mwambie aje alale kule kwetu maana tutaondoka mafungulia ng'ombe ili tuwahi basi la Mkikicho"
"sawa mama, nawatakieni safari njema, na kama ujuayvo huyu mdogo wako hajawahi kutoka hapa kijijini toka azaliwe hivyo nakuomba mama, mkifika huko mjini usije ukamuacha akapotoka, muonye na kumpa muelekeo pale utakapoona amekosea".
"sawa baba nimekuelewa"
Teresia akatoka na kumfata bi Marina jikoni,
"mama mie nataka kuondoka"
"mbona haraka hivyo mwanangu? siburia chakula kiive ule ndio uende"
"hapana mama, ngoja niende maana mama ananisubiria ili twende katika lile shamba letu la kule bondeni tukachimbe mihogo"
"haya mwanangu, kesho mtakapo safiri, nawatakieni safari njema"
"amina Mama, na nyie mbaki salama"
"asante mwanangu"
Teresia alipoondoka, Mama Kibe akamfata Mzee Sosongo kule alipo,
"sasa mume wangu, Kibe atabeba nini akienda huko mjini?" "kuna ile ndizi iliopo kule mwisho mpakani na shamba la bwana Kihara, nenda ukaikate ili iendelee kuchuruzika utomvu, mpaka Kibe arudi itakuwa imechuruzika utomvu wote"
"atabeba ndizi pekeyake au tumchanganyie na viazi vitamu?" "fanya hivyo utakavoona inafaa, ila usije ukamuwekea mzigo utakaomlemea"
"sawa mume wangu"
Kibe aliporudi akaambiwa ajiandae ili aende kulala kwa baba yake mdogo, tayari kwa safari kesho.
……..itaendelea wiki lijalo.
No comments:
Post a Comment