Thursday, May 17, 2012

"KOMBOLELA"

I can be President...Yes! you can baby brother..



Kwa sala naanza kuhesabu, moja mpaka hamsini,
tucheze kwa adabu, huku tunajiamini,
mchezo huu wa mababu, sijaoteshwa na majini,
ninaposema kombolela, kumkichwa ni wewe!.


Tumeganga kumtafuta mchawi, tukasahau vya akilini,
uchumi wa jirani unastawi, sisi upendo na amani,
baada ya kutoa matawi, mti tukaubwaga chini,
ninaposema kombolela, kumkichwa ni wewe!.


Aliyestaafu kala jana, leo twamfatilia nini,
tutaishia kumtukana, ana hisa mgodini, 
kama ukweli na uwazi havikufana, sasa maisha bora ya nini,
ninaposema kombolela, kumkichwa ni wewe!.


Nchi yetu masikini, umekua wimbo jukwaani,
sera za jembe la mpini, zinamzeesha babu shambani,
kwanza kilimo redioni, fuko la pipi bungeni,
ninaposema kombolela, kumkichwa ni wewe!.


Kama za mwizi arobaini, mbona kafikisha hamsini,
tokea miaka ya sitini, vifaranga tutanyonya lini,
kwa zetu fikra masikini, wametugeuza majinuni,
ninaposema kombolela, kumkichwa ni wewe!.


Tukikubali kua waamuzi, tusikatae pia lawama,
tusisahau ule uchaguzi, kwenye mstari tulisimama,
sasa nani mwamuzi, aliyechaguliwa au aliyesimama,
ninaposema kombolela, kumkichwa ni wewe!.


Ninaposema kombolela, naomba unielewe,
umwamshe aliyelala, mwambie KUMKiCHWA ni wewe,
kwakua tuliaanza kwa sala, mwenye niambaya asinielewe,
nitakaposema tena kombolela,wa kujikomboa ni WEWE.


Kajiabeid(c)kumkichwa2011

by Abeid Kajia on Saturday, April 23, 2011 at 5:38pm ·


No comments:

Post a Comment