Monday, September 24, 2012

DUNIA RANGI RANGILE ( 3 ) Sehemu ya Tatu

Sehemu ya Tatu
                                            
                            Mtunzi: Lasima Nassoro 
Wiki iliyopita tuliona kibe alivyifika mjini kwa Kanjubai, sasa yuko safarini anapelekwa eneo lake la kazi, je ni wapi na ni kazi gani,ungana na Mtunzi wako Lasima Nassoro kwa uhondo zaidi...
   Asubuhi na mapema walianza tena safari, walisafiri mchana kutwa. Walipita sehemu iliyokuwa kama jangwa, haikuwa na miti isipokuwa miba na miamba hadi wakafika katika msitu mkubwa. Ilipotimu saa tano usiku walifikia nyumba iliyokuwa katikati ya msitu mnene, Moris akamuambia Kibe,
"tumefika, nisubiri hapa, niende nikaangalie kama huyu jamaa yupo".
Geti lilikuwa limefungwa, akaamua kupanda ukuta ili aweze kuingia ndani, aliporuka ukuta akakutana na mbwa wakali, wale mbwa wakaanza kubweka huku wakitaka kumrarua. Lio akiwa chumbani kwake, akachukua bastola yake, akahakikisha kuwa ina risasi, akaenda dirishani kuchungulia nje, akaaona jamaa aking'ang'ana kupambana na mbwa, akaamua kutoka kupitia mlango wa nyuma, akanyata hadi alipomfikia yule jamaa, akamuwekea bastola ya kisogoni na kumuambia,
"leo utajua kilichomtoa Kanga manyoya". Moris aliposikia sauti ya Lio, akacheka,
"hahaha, Lio, Lio, Lio"
Lio baada ya kugundua kuwa mtu aliyevamia nyumba yake ni boss wake, naye akacheka kisha akamuambia,
"boss, una bahati niliamua kutoka, maana nilitaka niiachie risasi nikiwa ndani, bahati hukuwa katika tageti, imekuaje unafika saa hizi, halafu unaruka ukuta?"
Moris akavuta pumzi ndefu kisha akasema,
"nilijua umelala, naninavyokujua huwa ukilala kuamka ni shughuli pevu, ndio maana nikaamua
kuruka ukuta, hawa mbwa kidogo wanitoe roho".
"wanakufahamu hawa, walikuwa wanakutisha tu ili na mimi nitoke huko ndani, hujanijibu kuwa wafanya nini hapa saa hizi?".
"kuna dogo nimemleta, afanye kazi huku".
"kila idara mbona ina watu wa kutosha?".
"muweke kule kwenye vinu, baadae ukiona kuwa ni kijana muaminifu, unaweza ukamhamisha na kumpeleka kitengo kingine, huyo dogo nimemtoa kwa mkuu, yeye ndie aliyeniambia nimlete".
"sasa yuko wapi?"
"nimemuacha hapo nje ya geti, yupo garini"
Morisi akafungua geti na kwenda kuingiza gari, walipofika ndani, Morisi akamuambia Lio,
"Lio, huyu ndio dogo mwenyewe, anaitwa Kibe, Kibe huyu anaitwa Lio, atakuwa boss wako hapa, yeye ndiye msimamizi wa shughuli zote huku".
Baada ya Kibe kusalimiana na Lio, Lio akamuambia,
 "natumaini utakuwa mchapakazi mzuri,maana huwa sipendi watu wavivu, kama wewe ni mvivu, ujue kazi za huku hazikufai" Kibe akajibu,
"kazi ndio niliyoifata huku, kwahiyo ni jukumu langu kufanya kwa bidii hilo lililonileta hapa".
Lio akamgeukia Moris, "huko mlikotoka si mmekula?".
Moris akatabasam kisha akasema, "kwani wewe ni mgeni wa barabara ya kujia huku? huo mgahawa au hoteli itakuwa inaendeshwa na nyani au sokwe? maana hao ndio waliojaa njia yote".
"haya boss, nilifikiri mmepika huko njiani, ngoja niangalie chakufanya".
Lio akaenda jikoni kwake na kurudi akiwa amebeba sahani mbili zilizojaa wali na nyama, moja akampa Moris na nyingine Kibe, akawaambia,"hiki ndicho kilichopo, kwanza ni bahati tu niliamua kupika kingi, msiposhiba mutajazia na maji".
"tutashiba, na hii nyama ni aina gani?" hayo yalikuwa maneno ya Moris.
"we kula, usitake kujua ni aina gani ya nyama, ulifikiri tunafuga huku?".
"nafahamu kuwa hakuna mfugo hapa, nilitaka tu kujua ni aina gani ya nyama pori?".
"hiyo ni nyama ya swala".
"ooh! ndio maana tamu sana, bado umebakisha nyingine?".
"una maana gani, sinimekuambia hakuna chakula kingine zaidi ya hicho?"
"namaanisha kuwa kama una akiba ya nyama ya swala anigawie kesho nikiondoka nipeleke kwangu".
"hiyo utapata, lakini imekaushwa"
"safi sana, hiyo ndio nzuri, ukiipika hiyo uiunge vizuri na tui zito la nazi halafu upate na ugali mlaini na pilipili, hapo utatolewa mezani".
"hahaha, unapika mwenyewe? au kuna shemeji anayekupikia?"
"shemeji atoke wapi bwana, nilipokuwa mdogo mama yangu alinifunza kupika, kwahiyo nafurahia kupika nikitumia ujuzi nilioupata toka kwa mama yangu".
Wakati wote huo Lio alipokuwa anaongea na Moris, Kibe alikuwa kimya huku akimchunguza Lio alivyo, Lio alikuwa pandikizi la mtu, mweusi na alikuwa na mapengo, meno matatu au manne ya mbele hayakuwepo, halafu alikuwa ametoboa sikio la kushoto na alikuwa amevaa hereni, mkono wake
wa kushoto alikuwa amechora nge. Kibe akaanza kuingiwa na wasiwasi baada ya kumuangalia na kumchunguza Lio kwa muda, akawa na mawazo kuwa pengine hawa watu wanajihusisha na
biashara haramu maana kama ingekuwa halali, kwanini inafanyika katikati ya msitu mnene, ila hakutaka kuonyesha hofu yake maana japo hajakaa na Lio kwa muda mrefu, roho yake haikuwa na imani dhidi ya Lio, alimuona kuwa ni mtu ambaye anaweza kumtoa mtu roho. Baada ya kumaliza kula, Kibe akaonyeshwa sehemu ya kulala, huku akiambiwa kuwa kesho yake ndio atapelekwa katika kituo chake cha kazi. Baada ya kupanda kitandi, akafumba macho na kuomba mizimu ya kwao imulinde na chochote kibaya. Asubuhi na mapema, Lio alimuamsha Kibe, akamuonyesha maji ya kunawa uso, kisha akapewa uji.
"kaka Moris yuko wapi?" Kibe alimuuliza Lio.
"ameondoka kitambo sana , amesema anataka awahi kufika mjini maana kuna kazi nyingi sana zinamsubiria, maliza uji haraka twende maana saa zinakwenda. Alipomaliza kunywa uji, Lio akamuambia Kibe atoke waende, wakapanda gari aina ya Land Rover kisha wakaelekea juu mlimani, Kibe akamuuliza Lio,
"hicho kituo cha kazi kipo mbali sana?".
"ukienda kwa gari sio mbali sana, ila kwa mguu ni mbali kiasi".
"sasa nikishaanza kazi, nitakuwa nafikaje huko kwa  wakati? kama mtu akienda kwa mguu ni mbali".
"utakuwa unakaa huko huko pamoja na wenzako".
Walipofika juu mlimani, Kibe akaona nyumba zilizojengwa kwa miti na kuezekwa kwa nyasi, kisha akaona watu wasiopungua kumi, kila mmoja akiwa na kinu na mtwangio mkononi huku wakitwanga. Lio akasimamisha gari, akamuambia Kibe kuwa ashuke maana hapo ndipo  atakapofanyia kazi. Wale watu walipoona gari limesimama, wakaacha kutwanga na kulifuata lile gari, kijana mmoja aitwae Twalibe, akamsalimia Lio kasha Kibe, akamuuliza Lio,
"boss,leo mbona umetutembelea asubuhi subuhi kuna nini?". Lio akafungua mlango wa gari akashuka akasema,
 "nimewaongezea mtu mwingine maana nimeona kazi zinawalemea".
"tutashukuru sana boss, ndiye huyu?"
"yah, ndiye huyu anaitwa Kibe, Kibe hawa ni wafanyakazi wenzako, watakuonyesha namna ya kufanya kazi na mtakapo maliza kazi jioni, watakuonyesha sehemu ya kulala, Twalibe, si kuna vinu vya akiba?".
"ndio boss, vipo, ashindwe tu mwenyewe".
"haya mpeleke umuonyeshe vinu vilipo, kazi iendelee, nitarudi jioni kuangalia mlipofikia".
Lio akarudi katika gari kisha akaondoka. Twalibe akampeleka Kibe chumba ambacho vinu vimewekwa, wakachukua kinu kimoja na mtwangio wake, Kibe akamuuliza Twalibe,
"ni kitu gani kinatwangwa?".
Twalibe akamjibu,
"kuna majani fulani huwa yanaletwa hapa kila jioni, kazi yetu ni kuyatwanga kisha jioni boss analeta mengine na kuchukua yale yaliyotwangwa,t wende nikakuonyeshe yalipo ili uanze kazi".
Kibe akapelekwa chumba kingi kilichojaa magunia yaliyojaa majani, wakachukua gunia moja na kuelekea sehemu ile ambayo wenzao walikuwa wakiendelea kufanyia kazi.
Wakati wanaendelea kufanya kazi, Twalibe akamuuliza Kibe,
"kwani wewe umetokea wapi?".
Kibe akamjibu, "nimetokea kijiji kiitwacho SISI KWA SISI, ulishawahi kukisikia?".
"hapana, mie nimekulia mjini , sijawahi kufika kijijini".
"kwani ulikosa kazi nyingine huko mjini hadi uje kufanya kazi huku porini?".
"mie sijasoma,kama mtu umesoma na una vyeti vyako,hapo ndio utapata kazi za ofisini, ila watu kama sisi, kazi za mikono ndio saizi yetu, si umewahi kusikia kwa mtaji wa masikini ni nguvu zake mwenyewe?".
"sawa, sasa haya majani yana kazi gani?".
"mie sijui na sitaki kujua,ninachojua ni kuwa mwezi ukiisha Napata mshahara, kama haya majani wanauza au la, wanajua wenyewe".
Kibe akaamua kutouliza maswali zaidi, alijua kuwa wakati utafika ambapo majibu ya maswali yanayomtatiza atayapata. Walifanyakazi hadi muda wa chakula cha mchana ulipofika. Wakati wanaendelea kula, Kibe akamuuliza Twalibe,
"hiki chakula tunatakiwa tulipie?".
"la hasha, chakula na malazi ni juu ya muajiri, boss hapendi wafanyikazi wake wapate tabu".
"na mshahara ni mzuri au kiasi kidogo tu".
"kwa mtu ambaye hana kisomo na ukilinganisha na kazi tunayofanya, zinatutosha kusukuma maisha yetu, ila kwa yule ambaye hana mpangilio wa maisha anaweza kusema hazimtoshi".

Je haya ni majani gani? nini hatima ya Kibe? je nini kitamtokea kibe wakati yuko mbali na nyumbani kwao?...itaendelea wiki ijayo...

No comments:

Post a Comment