Monday, November 26, 2012

DUNIA RANGI RANGILE ( 10 ) Sehemu ya Kumi

                                                              
                      Mtunzi; Lasima Nassoro

ilipoishia ni kwamba Samson aliamua kumpa siri ya kazi yake Teresia ? je Teresia ataweza kuficha siri hiyo?,nini chanzo cha Samsoni kutoonekana,na amekimbilia wapi? je nini kitatokea akigundulika alipo?endelea....
   Teresia alipoona hakuna cha kufanya, akaamua kwenda kulala, alihangaika kitandani bila kupata usingizi,ilipofika saa saba usiku, akaamka na kupiga magoti, akasema, "Mungu wangu, najua mimi ni mkosaji mbele yako baba, nimefanya yale yasiyostahili machoni pako na jamii pia, lakini kwani mtoto akinyea kiganja kinakatwa?, nakuomba ewe Rabana, uliyetuumba sisi wana waadamu kwa pande la damu, uliyeumba majini kutoka katika ndimi za moto, ulituumba ili tukuabudu, baba, pia tukukimbilie pale tulemewapo na mizigo, nakuomba unifungulie njia na kunionyesha nini cha kufanya eeh baba, Samson ni mume wangu japo hatuja halalisha mbele yako baba, najua nimkosaji mbele yako ila ninachokuomba, umpatie ulinzi huko alipo, muepushe na maadui wanaomtakia mabaya, kama atarudi salama, nakuahidi kuwa tutaenda kanisani ili tufungiwe ndoa na majina yetu uyaandike huko mbinguni, usituache sisi waja wako japo tuwakosaji, AMINA". Alipomaliza maombi,akarudi kitandani na alijihisi kuwa amepata msaidizi wakumsaidia kupata suluhu ya shida zake. Akiwa pale kitandani,alikumbuka jinsi Samson alivyomuingiza katika biashara ya cocain, akakumbuka kuwa ilikuwa siku ya jumamosi jioni, Samson alimfuata pale kibandani kwake,alipofika alikuta vijana watatu wakila chakula, Samson akawasalimu kisha akamfuata Teresia kule jikoni, akamuambia , "leo nataka namimi nile hiki chakula unachouza maana toka tuanze kuishi pamoja sijawahi kuja kula hapa".
Teresia akamuambia, "lakini utalipa maana katika biashara hakuna mchezo".
"usijali mama,and speaking about biashara,nataka uwe msaidizi wangu wa ile ishu yangu niliyokueleza".
"ishu gani hiyo?,kama ni ile ya ile inayohusu co. . .  . Kabla hajamalizia, Samson akamziba mdomo na kumuambia,"shhhh, unataka uanike mchele kwenye kuku wengi?, si tulishayaongea na ukakubali kuwa niendelee tu, na kama nilivo kuambia, jamaa wameshajua kuwa unafahamu kuhusu hii biashara na hii biashara inahusisha watu ambao kuua kwao ni sawa na kumchinja kuku, sasa ninachotaka kufanya, unawaona wale vijana pale?". Teresia akachungulia na kuwaona wale vijana watatu wakila, akamjibu,
"ndio nimewaona".
"sasa wale vijana ni watumiaji wa white sugar".
Teresia akashangaa, "white sugar ndio nini tena?". Samson akamjibu kwa kunong'ona, "white sugar ni cocain, sasa nataka niwatambulishe kwako ili wakitaka bidhaa waje hapa wakuone".
"Sam, mbona unataka kuniingiza katika matatizo?, tulikubaliana kuwa we uendelee ila usinihusishe".
"sio mimi nilie amua kuwa uingizwe kwenye huu mtandao, mkuu ndie aliyesema uingizwe, hii ni kutokana na uchunguzi wa kina waliokufanyia baada ya kugundua kuwa tunaishi pamoja".
"wamegundua au umewaambia?".
"sijawahi kumuambia mtu kuwa nina mke ninae ishi nae, huu mtandao ni mpana sana, kuna watu kazi yao ni kupeleleza mienendo ya watu wengine, hivo wamenichunguza na wakampa mkuu habari kuwa nina mke ninaye ishi naye".
Baada ya Teresia kuelezewa kuwa kazi yake itakuwa kuchukua cocain ambazo zimeshafungwa katika kipimo kinachouzwa na kukaa nazo hapo kibandani kwake, wateja wataelezwa kuwa wakitaka waje pale kibandani na kujipatia hashishi. Samson akamtambulisha Teresia kwa wale vijana na huo ndio ukawa mwanzo  wa Teresia kujiingiza katika biashara ya kuuza dawa za kulevia. Teresia akakumbuka pia siku alipoanza kutumia cocain, alikumbuka kuwa ilikuwa jioni wakiwa wamejipumzisha katika makochi huku wakitazama tv, Samson akaleta unga kidogo katika karatasi akawa anaunusa, Teresia alipomuona akamuuliza, "sasa huo unga una raha gani? si kama tu ugoro aliokuwa ananusa bibi yangu?". Samson akamuambia, "huu si kama ugoro, ukipata hii kitu dunia yoote inakuwa yako, hakuna kitu inayokufanya uwe na raha katika huu ulimwengu kama hii kitu,hebu jaribu kidogo halafu utanieleza". Teresia akachukua kidogo akaweka puani na kuvuta, baada ya muda mfupi, akaanza kucheka hovyo na kuanza kuimba nyimbo zisizoeleweka. Wakati anaendelea kuwaza jinsi alivoingia katika mtandao wa dawa za kulevia, Teresia akapitiwa na usingizi, alipostuka ilikuwa saa mbili asubuhi. Samson akiwa anaelekea katika fukwa za maputo, alihisi kuwa kama vile kuna mtu anae mfuatilia lakini hakuwahi kumuona huyo mtu. Akajisemea, "Kanjubai wakati huu,umekula huu na hasara juu, umesahau kuwa kuti mgema alilozoea kukalia ndio lililo muangusha, nimechoka kutumwa kila siku, huku ukinufaika wewe, wakati mimi maisha yangu bado hayajaimarika". Alipofika katika fukwe, akanunua dafu na kwenda kukaa katika gogo la mnazi lililokuwa karibu na maji ya bahari yanapoishia kugonga yanapoletwa na mawimbi. Wakati anendelea kunywa maji ya dafu,akawa anafikiria jinsi atakavozitumia pesa alizo pata baada ya kuuza mzigo aliopewa na Kanjubai, akatabasam alipokumbuka jinsi alivyogeuza njia badala ya kwenda Lilongwe kama alivoagizwa, akaenda Maputo ambapo alikuwa ameshapatana na jamaa mmoja toka Duban, baada ya kukutana nae na kumkabidhi nusu kilo ya cocain, alikabidhiwa mkoba uliojaa pesa, dola milioni mbili. Samson akapanga kuwa, kwasababu ana pesa za kutosha kuanzisha biashara tofauti na cocain, akapanga kuelekea Namibia. Alipanga kuwa akifika kule,atasoma masoko ya bidhaa mbalimbali na atakapotambua biashara itakayo mpa faida nzuri, basi ataanza maisha mapya huko na hatorudi tena nyumbani kwao. 'sijui Teresia ameshapata habari kuwa nimetoweka na mzigo wa Kanjubai?' hayo yalikuwa mawazo ya Samson. 'akigundua kuwa nimetoweka,atafikiria kuwa nilikuwa simpendi, japo kiuhakika nampenda sana, ooh Teresia my dear, ningetamani sana kama tungekuwa wote huku,twende tukaanze maisha yetu upya na tufunge ndoa kanisani ili Mungu atupe uzao wenye baraka'.

Kanjubai baada ya kugundua kuwa Samson yupo Maputo, alimuagiza mpelelezi wake aliyejulikana kama COSMO kwa jina la utani, kuwa amchunguze kama bado yupo na mzigo wake au ameshauza. Cosmas au Cosmo kama alivyojulikana, alimfatilia Samson hadi akagundua hoteli anayo kaa. Alifanya jitihada hadi akaweza kuingia chumba alichokuwa analala Samson, akatafuta kila sehemu kuwa pengine ataona mzigo alio agizwa na Kanjubai. Alipokosa kuona sehemu zote zile alizohisi kuwa anaweza kuweka, akaamua kufungua mkoba aina ya brifcase, alitumia ujuzi wake kufungua, alipo ufungua, akakutana na mabunda ya pesa yaliyokuwa yamejaa, akachukua bunda moja ili kuhakikisha kuwa ni halali au si halali. Alipogundua kuwa zote ni halali,akarudisha zile pesa na kufunga ile brifcase kama alivoikuta. Akatoka pale na kurudi sehemu ile ya ufukwe aliyo muona Samson. Hakumuona pale alipomuacha, akamtafuta lakini hakumuona, akaamua kumpigia Kanjubai simu na kumueleza kuwa, Samson alikuwa ameshauza ule mzigo. Kanjubai akakasika, "are you sure na unacho eleza mimi?".
"am very sure boss, infact nimekuta brifcase imejaa American dollar, na hesabu yangu ya haraka haraka ni kama dola milion moja unusu kwenda juu". Kanjubai kuambiwa vile,akalegeza tai yake shingoni, akavua miwani yakena kuiweka mezani, akamuambia Cosmas, "sasa kwanini hujachukua hiyo pesana kuniletea?".
"hujaniambia kuwa kama nitaona pesa za huo mzigo nizichukue, so unataka nifanye nini kwa sasa?".
Kanjubai akasimama kutoka katika kiti alichokuwa amekaa na kukaa juu ya meza iliyokuwa pale ofisini kwake, akamwambia Cosmas,
"kama utaweza kuchua hizo pesa,zichukue uniletee kisha nitajua nini chakumfanya huyu paka mweusi".
"sawa boss, nitakupigia kukueleza kitakacho endelea hapo kesho".
Cosmas alipokata simu akaamua kutafuta chakula ale maana jua karibia lilikuwa linatua nayeye hakula chochote toka alipokunywa chai asubuhi. Alienda katika mgahawa uliokuwa unaitwa MAKONDE REUSTAURANT, akaagiza atengenezewe samaki m'bichi kwa ugali. Baada ya nusu saa akaletewa samaki aina ya sato na ugali kama alivoagiza. Wakati anaendelea kula,akamuona Samson akitoka katika ule mgahawa, 'kumbe huyu jamaa alikuwa humu ndani na nilipoingia humu sikumuona, ila sidhani kama ananijua',hayo yalikuwa mawazo ya Cosmas, mara baada ya kumuona Samson akitoka. 'we nenda tu ukajipumzishe au sijui waenda kujirusha, lakini mwisho wako unakaribia', Cosmas aliwaza huku akikata mnofu wa samaki na kuubugua, akamuita muhudumu aliyekuwa akipita karibu ya meza aliyokuwa amekaa, "muhudumu, naomba pilipili tafadhali". Baada ya kumaliza kula,akaagiza aletewe kikombe kimoja cha kahawa.

Je nini kitaendelea baada ya Cosmo na Kanjubai kugundua maficho ya Samson huko Maputo,Je huu ndio utakua mwisho wa Samson? Je Kibe na familia yake wanaendelea aje? Usikose Sehemu ya kumi na moja na ya mwisho wa hadithi hii...itaendelea wiki lijalo...Ahsante!!!

No comments:

Post a Comment