Wednesday, November 28, 2012

"Dunia ya Ushindani"

Photo by Af Arusha

Hizi mbio za sakafuni tazama ukingo wako ndio mwisho wako, kila mmoja macho kwenye mstari wa mwisho, pumzi na malengo visije vikapotea njiani, katika hii dunia ya washindani na mshindi hajulikani, kuna watakao anza kwa nguvu na kukaa mstari wa mbele na kuna watakao baki nyuma na kusubiria kufika mbele, kwa aliye mbele malengo yake kumpita aliye mbele yake lakini moyoni anahofia kupitwa na aliye nyuma yake.

Siku zote aliye nyuma humtazama wa mbele yake kwa makini kwa lengo lakutaka kumpiku na aliye mbele huwa anamhofia aliye nyuma yake kua anatambua huenda akampiku. Dunia ya ushindani ya mwenye kisu kikali ndie mlaji, wenye makali wanapowanyima vinoleo wasio na makali ili wasije wapiku kwa makali.

Dunia ya ushindani imejaa fitna na visa, tazama kwa makini usije ukawa mtumwa wa mtumwa wako, tazama waliopita na walioko juu namna wanavyohaha kuhofia walioko chini yao. Walio chini nao hawajui kua wananguvu kushinda walioko juu, ila fikra huru zimeingiwa na mdudu chuki, aliyemsafi kachafuliwa na wachafu kwa kuogopa usafi wake, hivi ni visa juu ya kisa. Kinachosemwa sio kilicho/wala kinachofanyika.

Panga kisha pangua, wagawe kisha watawale, nani asiyejua kua umoja ni nguvu, ili kuvunja vijiti vilivyoungana basi vigawe kisha vunja kimoja kimoja. Waahidi wanachohitaji ili upate unachohitaji, dunia ya ushindani, mwenye kisu ndie mlaji, asiye na makali ndio mtaji.

Tuanze na wewe kwanza, je upo kwa ajili yako ama kwa ajili yao? ubinafsi wa nafsi unavyozitesa nafsi . Mimi kwanza imefana machoni na mioyoni, kila kizuri kianze na mimi, moyo wa imani ya tule kwa pamoja kwa jasho imeshatoswa kwenye maji yenye kina kirefu.

Ongea pasipo kutenda, tenda pasipo kuulizwa, jenga kisha bomoa, jichotee kisha kana, mawazo ni mawazo hata kama hayana maana. Fikra za kweli hazifai wala hazina faida, changanya maji na mafuta ili twende sawa.

Nakusihi usichanganywe, usichanganye wala usichanganyikiwe, hizi ni fikra za ushindani ndani ya dunia ya washindani. Utakapo amua kufanya ukubali changamoto, hakuna atakayekuacha uteremke palipo na mlima, mkwamishaji wa kwanza ni wewe na nafsi yako, kumbuka ukiamua kufanya fanya, hakuna atakaye kuzuia, ila ni changamoto zinazokufanya uwe na fikra za kushindwa kwakua umeyaita ni matatizo/vikwazo badala ya changamoto. Kilicho bora kimeundwa kwa changamoto, kimeruka vikwazo, hakikutetereka, kilisimama na kutazama wapi kinakwenda na sio tu wapi kinakanyaga...!

Amkaa, Elimisha, Imarisha, Okoa kisha Unganisha. Panapo mwangaza angaza kwa kuamsha, pia elimisha kwa kutoa na kuingiza unavyovijua na usivyovijua, imarisha kwa kuvipa muongozo, okoa vilivyokosa tumaini na nafasi yakuona nafasi, waunganishe wawe kitu kimoja. Unapogawa unaondosha nguvu, unapounganisha unaongeza nguvu. Tazama kwa makini malengo yako je ni wewe au wewe na wao? Je kama ni wewe peke yako kwanini unalaumu wao kua hawana ushirikiano na wewe wakati hautaki kutambua umuhimu wa wao. Bila wao hakuna wewe, wewe na wao ni umoja, panda bora uvune bora..kiushindani kilicho bora ndio mshindi. Kuwa sehemu ya bora kwa kusaidia vilivyo bora..kumkichwa ni wewe!

No comments:

Post a Comment