Thursday, October 11, 2012

"MUONGOZO"

       
       Unapoanza kuusoma uwe makini, weka akili, fikra na nafsi yako sawa ili usipotee katika fikra hizi. Hili ni darasa huru, mwalimu ni wewe na pia mwanafunzi ni wewe, tambua kuwa siku zote walio mbele yako ni walimu wako na walio nyuma yako ni wanafunzi wako, anza kwa kujiuliza unajifunza nini na unawafundisha nini? Unachotakiwa ukipate hapa ni wewe! Hivyo utakapofika mwisho wa muongozo huu uwe umepata maana halisi ya wewe ni nani na unatakiwa ufanye nini? kumbuka kumkichwa ni wewe!

        Je unajitambua wewe ni nani na hapo ulipo umefika kwa uwezo wa nani? je umefika kwa kusukumwa ama umefika mwa maamuzi yako na ndoto zako? Je umefika kwa kushikwa mkono ama kwa muongozo wa walio mbele yako? Nakusihi usipotee kifkra, tambua kuwa uwepo wa nafsi yako hapo ulipofika unathamani kubwa sana. Jambo la msingi ni utambue hapo ulipo na wapi unapoelekea..!!

        Amka, angaza macho yako mbele, wapi unapoelekea? Je utafika unapotaka kufika? Je unapajua unapotaka kwenda? Siku zote ukipajua unapokwenda safari huwa ni fupi na usipopajua unapokwenda safari huwa ni ndefu, Je ni nani atakayekuongoza? utajiongoza mwenyewe au unategemea utaongozwa?


        Je wewe ni tegemezi? utategemea hadi lini? jiulize kama bila wao kuna wewe? Kama wewe ipo bila wao basi acha utegemezi, simama na miguu yako miwili, inapokua ngumu uwe mgumu, hata kigumu kina sehemu laini, tafuta ulaini wake usikate tamaa, rudia tena na tena, ushindi ni kwa asiyekata tamaa na sio kwa mshindani.

        Mazuri ni hufuatwa kwa uzuri na hata Mabaya hufuatwa kwa uzuri. Penye kosa sio kosa tu hata uzuri hupatikana penye ubaya, yote ni mafunzo na utayahitaji ili uweze kupata muongozo. Nakusihi usipotee katika fikra hizi, soma kwa umakini.

        Hapo ulipo usitazame pembeni si kulia wala kushoto, hii ni barabara huru, tazama mbele. Kipi kinachokunyima kuchanua? Nani anayekuvuta shati mpaka unashindwa kusonga mbele? Ni marafiki au maadui, wana umuhimu au hawana? Unawahitaji au hauwahitaji? Ukishamaliza darasa la saba mwalimu wa dalasa la kwanza hana umuhimu tena sio ama ndio? Umuhimu wa kitu ni pale unapokihitaji, wakati huu uliopo na wakati ujao?kama bado utamuhitaji mwalimu wa darasa la kwanza basi kaa nae karibu, kama sivyo basi songa mbele, fungua fikra kwa umakini, tazama mahitaji yako ya nafsi kwa umakini, usilazimishe kufika kumi kabla ya tisa, fuata muongozo baada ya tisa ni kumi. Kwa nafsi uwe na subira, kwa fikra tambua aliyekuumba huwa hawahi wala hachelewi, kila kitu na muda wake, kila muda na kitu chake, kila hatua ina mafunzo, kila mafunzo yana muongozo.

       Sasa kwa hapo ulipofika je umepata muongozo? Hembu tazama maisha yako ulipotoka kuna mafunzo?, je unayatumia kama muongozo?, hembu tazama walio mbele yako ni walimu je unawatumia?, nyuma yako ni wanafunzi je unawafunza? Je imani yako inatambua muongozo wa aliye kuumba, aliyekuumba huwa hakosei , yeye hukuongoza ila wewe ndiye unayepotea katika muongozo wake. Nakusihi usipotee karika fikra hizi. Jitambue wewe ni nani na unatakiwa ufanye nini?

       Mpaka hapo nadhani utakua umepata wewe, kama bado jiulize  nafsi inataka nini na fikra zinawaza nini? je nafsi na fikra zinalandana? je ulicho kifikira ndicho nafsi inataka ufanye hivyo? usijiulize, nafsi na fikra vikishakubaliana huwa hatujiulizi tena huwa tunafanya kwani ndio muda tunaokua sisi, kama wewe ni mtu wa kujiuliza sana basi ujue haujawa wewe, kuwa wewe ili upate wewe na ufanye wewe, ukimuiga yule wewe utakua ni nani sasa? usiogope kubadilisha fikra zako kama nafsi yako inataka hivyo, wala usiogope kubadili nafsi yako kama fikra zako zinataka ufanye hivyo, hakuna ubishani mgumu kama wa nafsi na fikra. Muongozo uliokubalika kwa nafsi na fikra ndio muongozo sahihi, hivyo jitambue kifkra na kinafsi
. Kumkichwa ni WEWE!

No comments:

Post a Comment