Monday, October 17, 2011

"KAMA HUU Sio UBiNAFSI NI NINI?"



“Maendeleo ni mtoto wa ushirikiano” hii ni kudhihirisha ya kwamba ni muhimu kushirikiana ili tuweze kuvuna matunda ya ushirikiano kwa ushirikiano. Ubinafsi ni hali ya kuwa na fikra mimi, kwanza mimi, wewe hapana, haiwezi kuwa wewe ni mimi, vizuri vyote na mafanikio yote yawe ya kwangu mimi. Fikra hii inawafanya wengi wanashindwa kuendelea kwa kua hakuna anayeweza kufanikisha peke yake bila uwepo wa watu wengine. Ushirikiano unatakiwa hapa ili kutengeneza kilicho bora kutoka katika vichwa vya walio bora na mioyo bora. 
                Wakati mwenyezi mungu alipomuumba Adam, aliona yuko mpweke na kwa hali aliyokua nayo, m/mungu akampa mwenza na msaidizi wake ambaye ni Hawa/Eve. Walishirikiana vizuri mpaka sasa tuna familia kubwa sana imejaa duniani. Haya ni uthibitisho toka katika vitabu vya dini, kwamba ushirikiano baina yetu ndio unaweza ukatusaidia kuondokana na vikwazo vinavyotukabili.
                Wakati Noah anajenga safina hakuwa mbinafsi alishirikiana na wenzake wale ambao hawakumpinga bali walimsikiliza kwani Noah ndiye aliyepewa upeo na muumba kuelewa nini kinakuja na nini anachotakiwa akifanye. Kama angekua mbinafsi asingetengeneza safina, na kama wangekua wabinafsi wasingeingia kwenye safina kwakua wangekua na fikra za kuuliza kwanini yeye  na sio sisi? Kwanini wewe na sio mimi.  Kama huwa unajiuliza maswali haya na huwa unajisikia vibaya mwenzako akifanikisha au akifanikiwa au akisifiwa kua kafanya jambo zuri ujue wewe una moyo na fikra za kibinafsi, na ndizo zinazokunyima wewe kuendelea na kuchanua kwakua fikra zako na matamanio yako yameshikamana na roho ya kwanini wewe na yeye na sio mimi na sisi, ingawa katika iyo sisi bado mwenye roho ya kwanini atauliza kwanini isiwe mimi. Kwa wale waliokua wabinafsi gharika liliwakuta na wakafa maji. Wewe uko wapi? Acha ubinafsi, shirikiana na wenzako, acha roho ya kwanini furahia mafanikio ya wenzako.
               Robert Nester Marley (Bob Marley) alisema “who Jah bless no one curse”. Kwamba kilichobarikiwa na mungu hakuna anayeweza kukizuia.  Unajua mwenzako anapofanikiwa hakuumizi popote wala hakupunguzii chochote zaidi ya kukupa njia/mwanya na mawazo ya kufanikisha kama utashikirikiana naye kwa kumuuliza kivipi umefanikisha/umefanikiwa ili na wewe ujaribu bahati yako. Tunapojenga fikra za ubinafsi tunajenga tabaka la chuki kati yako na yangu. Chuki hizi ambazo ziko kwenye mrengo wa kushoto ama fikra hasi. Fikra zenye kujenga na kuzaa chuki na fikra zisizo na faida kwa binadamu zaidi ya kubomoa kizuri kinachojengwa.
                Umuhimu wa kua na dini ni kueneza upendo na amani. Hakuna dini ya m/mungu wa kweli inayohimiza chuki baina ya watu. Hakuna dini inayohimiza ubinafsi. Katika vitabu vya dini vinatuonesha namna Yesu/ Nabii Isa (Jesus) namna alivyowashirikisha wanafunzi wake kwa kuwapa kisomo kwa wasivyovijua na kwa kuwarithisha elimu aliyoipata. Na wale walioachiwa elimu hiyo hawakua wabinafsi bali walishirikiana katika kuisambaza dini na kuelezea maneno ya bwana.
                Katika dini ya kiislamu tunasoma namna Mtume Muhammad (s.a.w) alivyopata visomo vya dini ya kiislamu na kisha akavisambaza visomo hivyo kwa wafuasi wake. Hakuwa mbinafsi na wafuasi wake pia hawakua wabinafsi kwani nao walisambaza yale waliyojifunza kutoka kwa mtume Muhammad  (s.aw).
Ukitazama maendeleo ya dini hizi yamekua makubwa sana duniani kutokana na ushirikiano baina ya viongozi na wafuasi wao, pia ushirikiano baina ya wafuasi wa dini hizo. Kama dini hizi zingekua ni biashara basi waanzilishi hawa wangekua matajiri waliofanikiwa sana kwa kazi walioifanya kuzieneza bidhaa zao sokoni. Ila viongozi hawa walifanya kazi hii ya m/mungu kwa kujitolea na kwa mioyo mikunjufu, kwa ajili ya watu wao bila ubinafsi. Hawakua na roho ya kwanini ni wawafaidishe wao na sio niifaidi mimi mwenyewe hii dini ya m/mungu. Kwanini niende nao peponi? Kwanini nisiende peponi pekeyangu niwaache zao peke yao. Na hawa wafuasi kuna waliojiuliza kwanini wao na kuna ambao hawakua hata na chembe ya ubinafsi na walijiunga kwenye dini hizi.
                Sasa sijui ubinafsi tulionao unatoka wapi! Mimi nadhani tumeingiliwa na mfumo wa kibinafsi wa kibeberu ambao unahimiza kila mtu kufanya peke yake. Unajua Yesu/Nabii Isa (Jesus) aliposema “kila mmoja atabeba msalaba/mzigo wake” hakumaanisha kwamba kila  mtu awe mbinafsi ila alituhimiza kuwa kila jambo baya na kila jambo jema litabebwa na aliyelifanya, malipo na adhabu zitakua kwa kila atakayeubeba mzigo wake mwenyewe. Na kwamba kila mmoja atawajibika kwa dhambi zake ama kwa aliyoyafanya.
Ila kwa ninayo yaona leo yananishangaza kwani watu wamejawa na ubinafsi, na nashindwa kuelewa je huu ni ubinafsi? Ama ni chuki? Ama ndio ushindani? Ama ndio njia ya mafanikio? Ama ni mfumo gani huu? Ama ni mdudu anatakiwa aondolewe?. Mbona dini zimefanikiwa kwa kushirikiana anakuaje sisi tunashindwa kushirikiana katika yaliyomema wakati wa sasa ambapo elimu imekua pana kwa kila binadamu, tumekua na uwezo wa kutofautisha jema na baya. Au yote yaliyo katika jamii ni mabaya ndio maana hatutaki kushiriki? Sidhani kama huu ni ukweli.
Hivyo hembu tujaribu kuuondoa huu ubinafsi ulio ndani ya mioyo yetu na kwenye fikra zetu. Tuache fikra za kwanini iwe yeye? kwanini iwe wewe? kwanini isiwe mimi? kwanini isiwe sisi?. Fikra hizi hazitatufikisha kokote. Fikra hizi zinatuzibia riziki  kwakua tunakesha tukiomba Yule akose badala ya kuomba tuongezewe kwa pamoja. Fikra hizi zinatunyima mwanya wa kujuana, zinatunyima mwanya wa kushirikiana, zinatunyima mwanya wa kusonga mbele kwakua tunang’ang’ana na kwanini yeye amefanikiwa na sio mimi?, kwanini ameanzisha kile na sio mimi? badala ya tuwe kundi moja ili tujiulize “tufanye  nini ili tuendeleze walichokianzisha? Tumsaidie vipi ili afanikishe alilolianzisha” tumsaidie mawazo gani ili na yeye afanikishe anachokifanya?.  Sasa itakuaje kama na sisi tukianza kujiuliza kwanini tunaandaa makala hizi? Kwanini tunaziandika? nawauliza kama huu sio ubinafsi ni nini? Kumkichwa ni wewe!
                                                                                                                                                                                     

No comments:

Post a Comment