Monday, January 7, 2013

"Ukweli Wetu"



         Walinishangaa nilipokua nasikitika walipokua wanajadili eti kama kungekua hakuna kifo kungekua na maisha tele, nikawauliza je vipi kama kungekua hakuna furaha mngekubali huzuni tele? Wakabaki wanashangaa. Ukweli ni kwamba hatuujui ukweli, hata kama tukiambiwa huu ndio ukweli bado tutauliza "ni kweli?”

         Ni kweli bila maisha kusingekua na kifo, vitu hivi vinashabihiana, ni sawa kukataa ya kwamba utajiri mwingi sio umasikini mwingi, wingi  kwa wingi, hata ujamaa ni kwa wajamaa wa jamaa.

         Tunapozungumzia Ukweli Wetu lazima tuugusie upendo wetu kwao, ukweli ni kwamba tuupende upendo kwakua tuna chuki, hatutaweza kuishi kwa upendo kama hatutoziondoa chuki zetu baina yetu. Huu ni ukweli wangu ambao utageuzwa kuwa uongo kama kuna chuki ndani ya msema ukweli.
 

         Malengo binafsi nayo huweza kuwa ya kweli kwa mtu binafsi, ila yaweza kua ya uongo kwa jamii, maamuzi madogo yanafanywa hadharani wakati maamuzi makubwa yanafanywa ndani chumbani. Ukweli wetu ni kwamba tunautambua uongo wenu, ila upendo wetu ndio unatufanya tuuamini kua ni ukweli, uongo ukirudiwa maranyingi hugeuka kua ukweli, huo ni uongo wetu ambao kwetu ni ukweli wenu.
 

          Ukimya wetu hauko kimya, tunaongea na nafsi zetu baina yetu, tunaongea kwa sauti ingawa kwenu ni kama tumenyamaza, sisi wakosefu wakudai haki yetu, wajeuri kwa kukataa uongo wenu. Maneno juu ya maneno ili kuvuruga maana halisi ya maneno. Uongo wao ni kwamba wameukubali ukweli wetu.
 

          Laa sitamani kujua ukweli wenu kwakua ni uongo kwetu, bora uongo wenu kwakua unatufanya tuone ukweli wetu, sauti zetu zenye busara na kauli zao zenye masihara. Wanaujua ukweli wetu kua tumekubali uongo wao, ukweli hubaki kua ukweli hata kama ukisemwa na mwongo, ila usiamini ukweli wa anayesema uongo, ni sawa na kukubali kua kipofu ni chongo mbili, au kukataa kua anaitwa bubu kwakua hasikii au haongei.

          Ukweli wetu ni kwamba msiongee uongo muda wote kama hamna kumbukumbu, kuna muda tunakubali kudanganywa na kuna muda hatukubali, eti bora kwa kila mmoja wakati msemaji mwenyewe sio bora. Tudanganye kwa muda ila sio kwa muda wote kwakua sio wote watakubali uongo wako.

          Unapovunja uaminifu haimanishi aliyekuamini ni mjinga, bali amekupa usichostahili "uaminifu wake kwako", sio kila anayekubali amekukubali, ila wengine wanakubali kwakua muda unaruhusu kukuamini kwa muda, ukienda juu kwa uongo utarudi tu chini kwa uongo, tazama alama za nyakati kwa wakati usije ukafka chini ukanza kuongea ukweli kua wewe sio mwongo, hata kwa hongo kipofu sio chongo wa macho mawili..Kumkichwa ni wewe!

 

No comments:

Post a Comment