Monday, January 17, 2011

KiZAZi KWAPUZi


                                                                        

    Tokea kuondoka kwa Papa, bahari imekua ikikumbwa na mawimbi mbalimbali yanayosabishwa na ukwapuzi wa mali za baharini. Suala hili limekua likiwasumbua sana samaki mpaka kupelekea baadhi ya samaki wakubwa wa hadhi za juu baharini kujiuzulu na wengine kuikimbia bahari kutokana na kuogofya  kwao matendo yao machafu waliyoyafanya.
      Ukwapuzi ni mchakato ambao ulichukua sura mpya katika maisha ya wanasamaki huko baharini na suala hili limepelekea wanasamaki wake kupoteza imani na matumaini na bahari yao. Ingawa samaki wakubwa wamejaribu kutimiza ahadi mbalimbali walizoziweka ili kuifanya bahari iwe shwari ila bado mioyoni mwa wanasamaki walio wengi kuna jeraha kubwa lisiloponeka la ukwapuzi.
      “Kwa kweli samaki wakubwa wasipokua makini katika bahari yao wanaweza kupoteza imani kwa wanasamaki wake walio wengi na wenye matumaini finyu na uongozi wa samaki wakubwa”, hayo ni maneno ya mmoja wa wanasamaki asiye na matumaini ya kupona. Hali hiyo kwa namna ilivyo inaweza kupelekea wanasamaki kufanya migomo, vurugu na hatimaye kufikia hatua  kupiga kura kuwa  hawana imani na bahari yao. Hatua hii itakua hatua kubwa ingawa pia panaweza pakazuka jambo kubwa zaidi ya hilo, “kama fikra zako wewe zinaona mbali basi utakua umeshapata hisia wapi bahari hii inapoelekea” alisikika samaki mwingine akieleza kwa uchungu, ni kweli hata katiba ya bahari inasema “Pale panapotokea wanasamaki wakawa wanalalamika sana kuwa wakuu wao wa bahari hawawajali na wala hawajali maslahi ya bahari yao, basi wanasamaki wanaweza kuwakataa viongozi wa bahari kwa kusema hawana imani nao”. Vyanzo vya ukwapuzi huu ni vingi lakini vikubwa vikuu vilivyotajwa na kuonekana ni kukosekana kwa uadilifu, uaminifu, uzalendo, uwajibikaji /uwajibishwaji wa viongozi wakubwa wa baharini.
      Ni kweli tusipokua makini na mdudu huyu wa fikra kwapuzi, kizazi na vizazi vinavyokuja vitadhurika na kuadhiriwa na mdudu huyu, kwani madhara ya mdudu  huyu yameingia na kutafuna ubongo wa wanasamaki walio wengi, hali ilivyo mdudu huyo amefika hadi kwenye kizazi cha sasa, kwani kila samaki mdogo  aliye katika mafunzo tayari ameshaanza kufikiria naye kuchukua chake mapema ili nae ajinome kama walivyofanya masamaki wakubwa. Kizazi samaki hiki kimekua na fikra kwapuzi, kila samaki anayekaribia kumaliza mchakato wake wa kukesha usiku kwa kusoma alama za bahari, naye amekua na fikra kwapuzi kwamba atajipooza kwa kukwapua fungu lake kisha nae atokomee nalo, kwakua hakuna atakaye mkamta. Kama samaki mkubwa amepenya na hajavuliwa kwa nyavu iliyotupwa baharini?, iweje mimi kisamaki kidigo nikamatwe na nyavu hiyo?.
      Wanasamaki wamekua wakishuhudia michezo michafu inayoendelea baharini ya samaki wakubwa kuvikamata visamaki vidogo na kuvitafuna bila huruma, kwakua samaki wakubwa ndio wenye nguvu na madaraka ya kutawala bahari hiyo. Ni kweli wameshuhudia pale alipotokea samaki mdogo na kutaka kutoa taarifa kwa wana bahari kuwa samaki wakubwa wanamaliza maliasili za baharini samaki, wakubwa hawakumchelewesha. Na pale wanasamaki walipojaribu kuwasemea, samaki wakubwa wamekua wakiwatishia kuwaweka hatiani hata kuwamaliza, hali hii imefikia kuleta hisia kwa wanasamaki kwamba wanabahari wanawaogopa masamaki makubwa.
        Usia wangu kwa samaki wadogo, wasiwe na fikra kama za samaki wakubwa kwani samaki wakubwa wameshapotea kwa tamaa zao, wanatamani kurudi katika hali zao za zamani za fikra huru bila kuwa na fikra kwapuzi ila wanashindwa kwakua baada ina tofauti kubwa na kabla, ndio maana wanazidi kuwa na fikra kwapuzi tu hadi haki zetu wanazikwapua. Hivi pale unapochukua kisicho jasho lako au pale unapodhulumu iliyo ya halali yake yeye unajisikiaje wewe samaki mkubwa ndani ya moyo wako?, hata kama hauna imani na yalionenwa na waliotumwa na aliye juu, jaribu kuweka uzalendo mbele kabla gharika halijakukumba wewe na kizazi chako, kwani leo tunacheka ila kesho tutamimiana vilivyo vya moto na milio ikipishana kama mbio za magari.
        Samaki uliyemchanga badili fikra zako za kikwapuzi mapema na kuwa na fikra huru za kutafuta kwa jasho, fikiria kizazi samaki kitakachokuja kitatumia nini na kitaishi vipi? kama wewe samaki mwenzao haujali maslahi ya baharini kwenu. Baadhi ya samaki wamesikika wakisema kuwa "hatutakuwa na huruma kwa wale watakao kwapua eti kwakua wamerithi kutoka kwa samaki wakubwa". Hivyo Samaki mdogo tambua kuwa  siku moja moto utawaka baharini, na moto huo utakapowaka utachoma kila kitu, sasa nazidi kukuasa wewe kuwa makini usije ukawa nawe ni mmoja kati ya kila kitu, na moto huo hauzimiki kwa maji ya aina yoyote. Na moto huu unachoma roho kwa roho mpaka majivu. Kumbuka kwamba KUMKiCHWA ni wewe!                                                                                                                                                                                                                             Kajiabeid©September,2010

No comments:

Post a Comment