Ni muhimu kwa kila mwanadamu kutambua zawadi aliyopewa na aliyetuumba, ingawa tatizo tulilonalo ni namna ya kutambua zawadi uliyopewa,pia namna tutakavyozitumia zawadi hizo, wengine wamepewa nguvu,wengine akili, vipaji,uwezo wakuchambua masuala mbalimbali yanayohusu jamii zetu kama vile siasa, michezo, sanaa, utamaduni, historia, kusaidia jamii, ubunifu pamoja na uwezo wa kufanya jambo likawavutia wanajamii wanaokuzunguka. Wengine kuongea na watu, kuchekesha pamoja na kuigiza. Wengine kuelewa lugha za watu kwa urahisi, kuelewa jambo kwa urahisi na wengine pia hata kulea familia, kupika, usafi na uteteaji wa haki za wanjamii.
Vyote hivi ni vipaji tulivyobarikiwa na aliyetuumba ili tuweze kuvitumia kwa malengo ya kuleta mabadiliko chanya katika jamii zetu na sio kwa lengo la kuzipotosha jamii zetu. Umuhimu wetu katika jamii ni kuelimisha, kurekebisha, kuilinda na kuitunza kwa kadiri ya uwezo wetu. Ingawa baina yetu wapo baadhi ambao malengo yao yapo kwa uhasi kwa kuiharibu na kuipotosha jamii na kizazi chake kwa ujumla. Sisi tujifunze kuwa watu wakukubali uhalisia, tusikatae uwepo wa fikra hasi kwani ndio zinazotupa uwezo wakujenga fikra chanya zilizo hai, na sio kwa kujenga fikra za sisi kushindwa kutumia zawadi zetu kwa uchanya, hivyo tuelewe kuwa “uwepo wa chanya kiuhalisia kunahitaji uwepo wa hasi”. Ila uwepo wao usitumiwe kama kigezo cha kuipotisha jamii kwa zawadi walizopewa. Umuhimu wa zawadi ni kuitumia kwa uchanya ili tupate jamii iliyo bora.
Mwanzo wa kila jambo huwa ni mgumu, kwa walio wengi iliwawia vigumu sana kutambua zawadi walizopewa au zawadi walizonazo, ingawa wengine kwao haikuwa kazi ngumu kuzitambua, ila kwa wasiotambua zawadi zao wajue kua kila binadamu amebarikiwa zawadi na aliyetuumba. Na huu ndio muda kukaa chini kwa makini na kutafakari ili ujue zawadi ulizobarikiwa/ulizonazo. Kiukweli pale unapotambua zawadi uliyopewa kwa muda maalumu na kisha ukaitumia vizuri kwa muda maalumu, zawadi hiyo itakusaidia wewe na jamii yako kwa njia moja au nyingine. Wapo waliofanikiwa kuzitambua zawadi zao na mpaka sasa zinawalipa mafao mazuri kwakua wamezitumia vizuri mbele ya jamii zao na jamii zao pia zikawakubali, pia wapo waliozitumia vibaya zawadi zao nao zikawalipa vibaya, kwa kuwa malengo yao mabaya waliyoyaweka mbele ya jamii hayakukubalika na kupelekea jamii yao kuwakataa. Hivo utakapo tambua zawadi yako uwe mvumilivu na jamii yako kwani ni sio vigumu kukubaliwa na wanajamaii ila ni vigumu kuendelea kukubaliwa na wanajamii. Wewe jipange vizuri na tumia zawadi yako vizuri kwani leo ina tofauti kubwa sana na kesho na ukipanda chanya leo basi kesho utavuna chanya, ila ukipanda hasi leo usitegemee kesho utavuna chanya.
Tatizo la zawadi hizi tulizopewa ni namna tunavyozitumia vibaya katika jamii zetu. Tutambue ya kwamba kizazi kinachukuja na kilicho chini yetu kinatutegemea, sasa kwanini tunakipotosha badala ya kukielimisha? ikumbuke kwamba “majuto yetu si kwa watoto wetu bali kwa wajukuu zetu” tuacheni kabisa fikra hasi wakati tunapotumia zawadi zetu, tujenge imani na fikra chanya ili zitujengee uvumilivu wakati wa mapambano na fikra hasi dhidi ya jamii zetu.
Katika mapambano haya tunatakiwa tuwe wabunifu wakutambua jamii yetu inataka nini? imekosa nini? na ingetamani kuwa na nini? Na inategemea nini kutoka kwetu? tusiwe wabunifu wa kuiga kwani zawadi tulizopewa zina upekee wake kama tukiwa wabunifu. Pia tusiwe wabunifu wakusubiria kutafuniwa na kulishwa, vingine vinaweza kua ni sumu kwa jamii yetu, mwisho wake ni kupoteza uhalisia kwa kuipotosha jamii kwa kuilisha sumu na kupekekea kushindwa kutumia zawadi zetu vizuri. Jaribu kuitazama jamii yako inayokuzunguka kwa makini, nitazame mimi, yeye, sisi na wao, sio wote tuliopewa zawadi kama ya kwako, ingawa zawadi nyingine hufanana ila katika kila zawadi kuna upekee wake unaomtambulisha mhusika wa hiyo zawadi. Na huo uhalisia wa upekee wako ndio utakaokupa heshima yako mbele ya jamii yako.
Unachohitaji ni muda wa kukaa chini na kuumiza kichwa chako ili uweze kutambua zawadi yako kisha uitumie katika kuitunza na kuelimsha na kuijenga jamii yako iwe bora, pia wewe kama mmiliki wa zawadi ujijengee misingi iliyo bora ili zawadi yako ikuletee matunda bora, kumbuka matunda bora yanatoka katika mti bora. Naomba nieleweke kua hakuna binadamu aliyenyimwa zawadi hizi na aliyetuumba, kwa njia moja au nyingine tambua kua una umuhimu katika jamii iliyokuzunguka, ila ni sisi wenyewe ndio tunaojinyima muda wakutambua na kutafakari umuhimu wa kutumia vizuri zawadi zetu. Tushirikiane mimi na mimi au wewe na yule au yeye na sisi katika kutambua na kutumia vizuri zawadi zetu.
Ila yote haya yatafanikiwa kama ukianza na wewe, kwa kua maamuzi, uwezo, nguvu na imani viko ndani wewe. Ni uamuzi wako ndio utakaokuwezesha kuijenga jamii baada ya kutambua zawadi yako. Usijinyime zawadi yako pia usiinyime jamii zawadi yako. Kumbuka zawadi kubwa tuliyopewa ni maisha na kuwa na uhai. Ila zawadi nyingine ziko ndani yako wewe na ndo maana tunaanza na wewe kwakua KUMKiCHWA Ni WEWE!
Kajiabeid(c)2011
Oooh yeah!!! Kumkichwa club for life. Endelea kupost mengi na tunaahidi kukuunga mkono.
ReplyDeleteTanx Comrade..naona umetumia zawadi yako kwa kuelewa hii post..ahsante sana kwa ushirikiano wako..tuzidi kushirikiana kwa uchanya..
ReplyDelete