Tuesday, August 9, 2011

"SAFARi YA MiAKA MiTATU"


Ilipoanza ni kama safari ndefu isiyo na matumaini ya mimi kufikia mwisho wake, kwakua mengi niliyoyasikia kuhusu safari hii na changamoto zake nje ya uwanja/mfumo zilinipa wakati mgumu katika kujifikiria ya kwamba,ni kwa namna gani nitaweza kufika mwisho wa safari hii. Safari hii ni ya muda unaojulikana ingawa kuna ambao walikata tamaa tulipoianza, kuna  waliochishwa njiani mwasafari kwa sababu tofauti tofauti na kuna walioshindwa kabisa kuendelea na safari hii ingawa walishaianza. Elewa ya kwamba kusafiri kwake ni safari ya maisha, ila kwa mafunzo yake kwa miaka ilikua ni mitatu tu.

Mwanzo wa jambo huwa ni mgumu siku zote, kwakua mtu huhitaji muda wakukaa ,kujifunza, kutambua kisha kujiweka sawa, na kwa mazingira ya safari hii ilinibidi kuyajua kwanza ili niweze kuendana nayo kiuhalisia kwa kuyabadili au kwa kujibadili kama kinyonga. Mwanzo wa Safari yangu ulianza kwa ugumu, kwani ilihitajika mimi kuyafanya mazingira yaweze kuendana nami ama mimi niendane na mazingira hayo ya safari. Kwakua nilithamini umuhimu wangu na kutaka kuwa mimi na sio kinyonga, niliamua kuyafanya mazingira yaendane na mimi na sio mimi niendane na mazingira ya safari  kwani ipo nafasi ya mimi kupoteza uhalisia wangu kwa kuyafuata mazingira ya safari hii. Hapa pia  ndipo nilipotambua umuhimu wa mimi kuwa mimi na sio mimi kuwa kama kinyonga kujibadili kuendana na mazingira yasiyoniridhisha eti nami nionekane ni mmoja kati ya wao. 

Mbinu nilizozitumia zilitokana na kukubali uhalisia wa maisha niliyoishi na namna nilivyokuzwa kwa mazingira yangu, kutambua kwangu umuhimu wangu katika jamii yangu, na kukumbuka kwangu wapi nilipotoka, na kutazama kwangu wapi ninataka kufika ni mojawapo ya mbinu zilizonisaidia kufika hapa nilipo. Katika safari hii ilinibidi kuongeza upeo kwa kuchanganua na kuchunguza ni mambo gani ninaweza kuyachukua kama yalivyo, kuyaacha kama yalivyo ama kuyabalili yalivyo ili yaendane na mimi. Kipindi hiki cha mwanzo kilikua kipindi kigumu sana wakati wa safari hii, kwani ilifika wakati ilinipelekea kutoka katika mstari wa safari hii, ila kwakua nilipata muda wa kutambua nilipokosea, nilifanya mabadiliko ya haraka na kurudi katika mstari wa safari hii.

Katikati mwa safari hii kulikua ni wakati wa kufanya marekebisho na muendelezo wa mbinu za mwanzo kwa kufanya kwa vitendo vyote nilivyovidhania kwamba ni muhimu kuvifanya ili kuifanya safari yangu iwe na umuhimu zaidi ya kusafiri, nilijifunza vingi kuliko nilivyofundishwa, nilijifunza kuona vilivyofichwa kwa kutumia akili ili wanaotumia macho na masikio wasivielewe. Nilijifunza kujiandaa kabla na kukubali matokeo baada, kuthamini ulichanacho, ulivyo na matakwa yako. Kuacha kisicho, kukwepa visivyo na kung'ang'ania kilicho. Kipindi ambacho umuhimu wa safari ulianza kuonekana kwa vitendo, na watu walitambua uwepo wangu kama mmoja kati ya wasafiri kamili wanaotambua wapi wanapoenda. Ingawa vikwazo na binadamu wake hawakucheza mbali katika kunirudisha nyuma, muumba aliye juu aliniepusha na majaribu yao kwani istiqaama niliyonayo ili imarika kadiri walivyonijaribu kwa mbinu zao. Nilithibistisha ya kwamba hakuna tatizo lisilo na suluhisho, kwani kwa kipindi hicho nilimuomba  muumba anijaalie uvumilivu, usikivu na utulivu kwa matumaini ya kula mbivu.

Mwishoni mwa safari hii ndipo makumbwa mengi yenye tija yalipoibuka kwani hata lisilowezekana ilithibitika kwamba linawezekana  kama utatumia muda wako na fikra zako kwa wakati maalumu na kwa sababu maalumu. Nilikua nikiamini ya kwamba kila mtu amezawadiwa zawadi yake na maulana na kwa kipindi hiki nilikua nikitamani kuijua zawadi yangu toka kwa maulana, na ndipo  kipindi hiki nilipo igundua zawadi hiyo na kuanza kuitumia. Katika safari hii kwa ujumla nilijifunza mengi hasa urafiki wa marafiki na unafiki wa marafiki, katika maisha haya ya sasa sio kila  anayekupenda kweli anakupenda na pia sio kila anayekuchukia kweli anakuchukia, kila mmoja yuko katika maisha yako ili atimize sehemu ya maisha yake, yaani kujaza kitabu chake kwa uwepo wako.

Kiukweli  hakuna anayeaminika ila cha muhimu ni  kujiamini wewe mwenyewe na kama ukimuamini mtu usimuamini shetani aliye ndani yake. Binadamu huwa tunabadilika na pia huwa tunabadilishwa, kuna wanaomaua kubadilika kwa matakwa yao  na wanaobadilishwa kwa matakwa ya kinacho wabadilisha, mtazame uliyenae na uliokua nao sio wote wako kama zamani na sio wote watabaki kama zamani. Ndio maana tunasema akili kumkichwa  ni kwa kichwa yako wewe, usipokua makini na ulimwengu na walimwengu wake  utabaki unatupia dua lako la kuku kwao  mwewe. Wewe cheza nafasi yako na sio uchezee nafasi yako, amini usiamani ukiwa nje ya uwanja/mfumo hakuna atakayekujali/atakayekuthamini. Wakati ndio huu amka wewe uliyelala….Kumbuka kumkichwa ni wewe!

No comments:

Post a Comment