Wednesday, March 14, 2012

"Siku Maji yakirudi nyuma"






Litakua  ni jambo la kushangaza pengine na kutupumbaza kuona siku hiyo... kivipi maji yamerudi nyuma badala ya kwenda mbele!..., ni mshangao ambao utatufanya wengi wetu tustaajabu ya kuwa ni kivipi maji haya yamerudi nyuma! Tutabaki tukijiuliza kwakua tumekua ni wagumu kuelewa kwamba maji yanaweza yakarudi kama mambo hayatakwenda namna yanavyotakiwa yaende au kama tutaendela na mfumo wetu wakuacha mambo yaende kama wanavyotaka na sio kama tunavyotaka sisi yaende kwa kujishirikisha kwenye shughuli za kila siku za ujenzi wa taifa letu. 


Tukiwa kama watazamaji wa mambo yanavyoenda kila kukicha bila kuwa watendaji na washiriki katika kufanikisha mambo yaende vile sisi tunataka, hatuna budi kukubalia na hali itakavyokuja kubadilika kwa kushuhudia maji yanayotoka katika Ziwa letu la Victoria yenye Upendo na Amani ya miaka hamsini kisha kupita katika Mto Naili yakiwa yanasambaza Upendo na Amani kwa nchi za Sudan, Libya, Somali na Misri na kisha kumwagika katika bahari ya Sham yakirudi na chuki, vurugu, vita, mageuzi kutoka nchi ya Misri, Libya, Somalia na Sudani na kurudi nchini kwetu na kusambaza ari hizo kwa wananchi wetu wenye amani na upendo, kwa kusahau kwetu misingi iliyotujengea na kutupa Amani na Upendo kwa miaka hamsini tukiwa huru kwa kujitawala.


Tumeshuhudia yaliyotokea Misri, tumekuwa wazungumzaji wazuri kwa yaliyotoka Libya, tumewahurumia na kushuhudia mgawanyiko uliotokea Sudani. Sasa kwa haya yaliyotokea katika nchi hizi hata nchini kwetu yanaweza yakatokea muda wowote na saa yoyote. Lakini itakuwa hivyo kama tutakuwa wagumu kutambua ni wapi panapokwenda tofauti na namna panavyotakiwa paende.


Kwa namna gani tunatakiwa tuwajibike vilivyo katika shughuli zinazotuhusu.Tusiishie kuwa watazamaji na wasemaji, eti kwakua kuna watu tumewateua wasimamie shughuli zetu basi sisi tukalale tusubiri watufanyie kila kitu , tabia hii itatuletea lawama juu yao na sio juu yetu kwakua hakuna anayetaka kubeba mzigo wa miiba alioujaza yeye mwenyewe. Huyu kakosea yule kamsema, yule aliyesemwa nae kaamua kusema mabaya ya mwenzake. Huyu anakataa kujiuzulu kwakua anapenda madaraka, amekosea lakini hataki kuwajibika kwakua anapenda madaraka. Maji yakirudi nyuma vipi atatulaumu kwanini yamerudi nyuma wakati yeye hataki kuwajibika!.


Tazama wanasema chochote ili vyombo vya habari vipate chakuandika, tazama namna vyombo vya habari vimeteka vichwa vya watu. Kinachoongelewa jioni ya leo kesho utakikuta kwenye kichwa cha habari. Maigizo ya wasanii wasiopenda jina la wasanii. Wanachezea matope kisha wanajisafisha kwa maji yenye matope na kujiita wasafi. Siku maji yakirudi nyuma watatuuliza nani ni mchafu.


Wanachukua kisicho halali kwa njia zisizohalali kwa kuihalalisha kua ni halali. Tazama yatima analia mpaka machozi yanakauka hana wakumdekea, kilicho halali yake kimehalalishwa tumboni kwa walaji, hana chake, aliyetoa katoa kwa asiyenacho, kapokea mwakilishi wake na kimeliwa na mwakilshi wake kwa kujaza tumbo lake, yatima hana chake, anatamani maji yarudi nyuma. Hali ibadilike apate chake, chozi lake thamani yake kwake kwani linampunguzia huzuni iliyomo ndani ya moyo wake. Bora limtoke apate faraja yake kwani baada ya chozi la mwisho kufutika ana imani furaha itajitokeza.


Najiuliza Siku Maji yakirudi nyuma sijui hali itabadilika, aliye na uwezo wa kuona mbali kwa jicho la tatu, ajaribu kutazama aone namna maji yatakavyorudi nyuma. Ukisoma makala hii kwa makini utanielewa kwanini nawasihi tuombe sana maji yasije yakarudi nyuma. Tazama namna umasikini wetu unavyoujenga utajiri wao, mwerevu atanielewa tofauti na hapo sintowashangaa sana mkinipinga, kwani mi husema niyaonayo. Ukibishana na mjinga atakushinda kwa ujinga, na wewe utakua mjinga mkubwa mbele ya mjinga, ni ujinga kuogopa kifo cha kuku wakati ndio kitoweo ulichonacho, narudia tena matatizo yetu ndio mtaji wao.


Tunapokosa matumaini wao hutupa faraja kwa “mkinichagua mimi nitatatua shida zenu, nawahakikishia kua thamani ya shilingi itapanda, nitawajengea barabara, shule, hospitali, visima vya maji nchi yetu itakua na maendeleo na itapiga hatua kubwa kiuchumi duniani. Miaka inakwenda anashika hatamu, miaka inakwenda awamu inakwisha, hajafanya kitu anarudi tena na matumaini mengine na ahadi nyingine nyingi, akimaliza amamu zake mwingine anapokea kijiti, anaendelea kukikimbiza kwa ahadi zisizotekelezeka na zilizotelekezwa. Sisi tumebakia kulalama kwa maneno makali bila yakujua kesho yetu itakuaje. Tuombeeni maji yasije yakarudi nyuma sababu itakua ni vilio juu ya kilio.


Tuombe usifike wakati ujasiri ukaushinda uoga, kwani kifo kitakua ushujaa na uhai utabakia aibu, wananchi watakapoona fahari ya kupoteza walichokuanacho kwa ujasiri wakupigania wasichokuanacho. Hawatasikia la mwadhini wala la mnadi swala, vijana watakapopita mbele kwa ujasiri wakutaka kumvisha paka kengele. Tuombee maji yasije yakarudi nyuma.


Wengi wameniuliza mbona kila siku wewe huongea tu matatizo bila kutoa suluhisho la matatizo. Ni kwamba shida zetu zinaletwa na matatizo na matatizo yanaletwa na sisi wenyewe kwakua tumekua wagumu wa kuelewa na wakuona ukweli na kuchukua hatua. Tunatatua shida na kuacha tatizo, bila kujua tatizo ni vigumu kwetu sisi kumaliza matatizo yetu. Mfano vijana wanashida ya kupata ajira kwakua kuna tatizo katika mfumo mzima wa ajira kwa vijana, sasa badala ya kuubadilisha mfumo mzima ambao ndio tatizo, tunatatua shida ya ajira kwa kuwapa baadhi ya vijana ajira na kujivunia kua ukosefu wa ajira umepungua.

Nimendika nilichokiona na kinachokuja mbele yetu kama hatakua mstari wa mbele katika kubadilisha mfumo nyonyevu unaotunyonya fikra zetu hai kwa kutuosha kwa starehe zisizo na umuhimu katika maisha yetu ya sasa na ya baadae. Tumetekwa na vyombo vya habari kwakua hatutaki kuchanganya akili zetu na tulichokisikia na tulichoambiwa ama tulichokiona. Mbayuwayu alitaka kua na mdomo uliochongoka, aliambiwa ili uwe mzuri basi aende juu kisha ashuke chini na augonge mdomo wake kwenye jiwe, akafanya kama alivyoshauriwa ila alipokaribia jiwe lile akasema “AKILI KUMKICHWA” nisije ni kafa bure, akaokoka kifo kwa kusikia alichoambiwa na kuchanganya na akili yake, je wewe unachanganya akili yako na ulichoambiwa au unaenda tu kwa amri ya mwenye cheo?, siku maji yakirudi nyuma utanikumbuka kwa kusema kumkichwa ni mimi… ila mimi sintochoka kukukumbusha ya kua KUMKiCHWA NI WEWE!

  

1 comment: