Friday, March 9, 2012

"JITAMBUE KWA FIKRA CHANYA"




Kujijua ama kujitambua ni namna ya kufahamu uwezo wako ulionao katika kuweza na kutokuweza kwako. Kujua ama kutambua ni hali ya kupata ufahamu juu ya kitu au jambo Fulani ambalo ulikua hauna ufahamu nalo hapo mwanzo.

Kuna kutambua/kujitambua kwa aina mbalimbali, kuna  kutambua kwa kugundua mwenyewe, kujijua uwezo wako kua unaweza/ huwezi kufanya kitu au kuwa katika hali fulani bila kuambiwa na mtu mwingine bali kwa kutambua mwenyewe, mfano mimi naweza kuchora, kuimba, kusoma au kutangaza kwakua nilishajaribu na nikaweza. Pia kuna kutambua kwa kuambiwa na mtu/watu, hii inatokana na watu hasa walio karibu yako kukujuza kua unaweza kitu fulani ambacho wewe mwenyewe ulishindwa kutambua kua unaweza/huwezi kukifanya mfano; utaambiwa na mtu /watu kwamba “unajua wewe ni mbunifu, kwanini usiendeleze ubunifu wako?” au “unajua wewe sio mwadishi mzuri, jaribu fani nyingine au jaribu kwa njia nyingine!”. Pia kujitambua baada ya kufanya jambo fulani kwa kutambua matokeo ya jambo hilo ulilolifanya, na mwisho kutambua kwa jambo walilofanya walimwengu.

Kwa ujumla kutambua/kujitambua huku huwa kunaweza kuletwa kwa fikra chanya au kwa fikra hasi.

Fikra hasi ni fahamu/hisia zinazomjia mtu kwa hali ya kumfanya ajione ni mwenye kushindwa, fikra hizi mimi hupenda kuziita kuwa ni fikra za mrengo wa kushoto ambao humfanya mtu ajijaze mawazo ya kushindwa kutatua jambo kwa urahisi. Fikra hizi hasi huwa zinaambatana na misukosuko isiyoisha. Huwa zinamfanya mtu kuelekeza baya penye ubaya na kufanya mabaya juu ya mabaya, ingawa kuna muda fikra hasi zinaweza kumsaidia mtu kujitambua ila kama mtu huyu akiwa hasi sana ni vigumu kujua uchanya wa fikra hasi.

          Katika kujitambua kifkra, fikra hasi  ndizo zinazoshusha munkari, fikra hizi pia huwa na dhana ya kushindwa/ kutokuweza ama kukata tama kabisa, na humfanya mtu adumae kimawazo kwakujiona hawezi. Kwa mfano mtu anaweza kua na fikra  chanya na kujitambua kua anauwezo wa kufanya jambo fulani lakini pale anapokutana na kikwazo/vikwazo mtu huyu hujiwa na fikra hasi kuwa hawezi kufanya hilo jambo ndio maana vikwazo hivyo vimejitokeza. Humfanya mtu ajiweke kwenye nadharia mbalimbali za kushindwa na kuwapa lawama wao na sio yeye. Kiuhalisia hakuna anayeshindwa kama atajimbua anaweza na hata akikumbana na vikwazo atavitatua kama atakua na fikra kwamba hakuna kinachoshindikana chini ya jua.

Mtu pia hujitambua mwenyewe uwezo wake kama atapata muda wa kukaa na kujifikiria, kwa kutumia uhasi wa fikra mtu huyu huweza kujitambua kwa kuelewa fikra hasi alizonazo, pia kwa kuambiwa na watu kwamba yuko na fikra hasi, pia jambo atakalolifanya kwa maamuzi yako humpelekea mtu kujitambua fikra hasi zake, pia kwa kutazama mienendo na matendo ya walimwengu mtu huweza kuzitambua fikra hizi. Cha muhimu pale panapokua na fikra hasi ni vizuri mtu kuzitambua kwa uhalisia na kisha kuzichanganua kwa fikra chanya.

Fikra chanya ni zile zenye kuleta matokeo yenye kuendeleza mwenendo bora baina ya watu au mtu. Fikra hizi mimi huziita ni fikra za mrengo wa kulia. Humfanya mtu akajitambue bila kuleta uhasama na bila kutupa lawama kwa wao wala kwa nafsi yake. Kwakua fikra hizi huzaa uchanya panapo uhasi na uchanya penye uchanya, hizi huwa ni fikra bora zinazomjengea mtu imani pale panapotokea ugumu wa jambo au vikwazo , mtu huyu hutambua vikwazo kama nafasi ya kufanikisha anachotaka kukifanya. Fikra zenye uchanya kuwa zinaleta matumaini pale yanapokosekana, fikra hizi muda wote huwa hai na mwenye nazo huwa ni mtu wa kufikiria yaliyo mazuri  na kama akiona ubaya huwa anatambua uwepo wa ubaya kua ni chanzo cha uzuri na uzuri unategemea uwepo wa ubaya.

Katika kujitambua kwetu fikra ndio zinatufanya tuwe na uwezo wa kujitambua, na katika aina za kujitambua, ubora uko pale mtu anapojitambua yeye mwenyewe pasipo kuambia. Ugunduzi huu humfanya mtu kujiamini na kujielewa uwezo wake, pia huweza kumbadilisha mtu akawa mwenye furaha kwa kujitambua mwenyewe uwezo wake na mapungufu yake. Kuna usemi unasema “majadiliano bora kuliko yote ni yale unayoyafanya wewe mwenyewe ndani ya moyo wako na ndani ya fikra zako kisha ukakubaliana nazo”

Kuna vitu ambavyo vinatuzuia tusiweze kujitambua, katika vitu hivi vinavyowazuiwa watu kujitambua kimojawapo kikubwa ni muda wa kutafakari mambo yetu na mienendo yetu wenyewe. Na hii ni kwasababu watu wengi hasa Watanzania huwa tunafuatilia sana maisha ya watu kuliko ya kwetu sisi wenyewe. Tuna katabia cha nani kafanya nini? nani alifanya nini? badala ya kujipa muda wakujitambua wenyewe kwamba mimi nafanya nini? nifanye nini? ni wapi nilikosea? wapi nirekebishe? ni wapi kuna nafasi niitumie? kwa muda gani natakiwa niitumie hiyo nafasi ili niweze kufanikisha? malengo yangu ni yapi? je yamefanikiwa? yameshindikana wapi?. Huwa tunajinyima haki ya msingi ya kujitambua wenyewe kwa kuwa tunawekeza muda na fikra zetu kwa wao na yeye kwa  mambo yasiyo na msingi, na kujinyima muda wa mimi nifanye nini kwa yaliyo na msingi ili nitimize malengo yangu. 

Kama ukiweza/umeweza kujitambua kua utaweza/ unaweza nini! Ni vizuri ukaondokana na fikra hasi za kwamba hauwezi, jaribu kutambua uwezo na mapungufu yako kutumia uhalisia wa maisha yako mwenyewe ambayo ni mkusanyiko wa mafunzo mbalimbali ya kuweza na kukosea uliyoyapata tokea umeanza kutambua zuri na baya. Nakusihi  utambue ya kwamba mafunzo yanayochukua nafasi kubwa katika maisha yetu ni yale tunayojifunza wenyewe, ambapo ndipo kujitambua kunapotokea.

Kama binadamu basi sio vibaya sana pale unapokua na fikra mbalimbali juu ya jambo, mtu au kitu, na hii ni kutokana na namna ulivyokuzwa au malezi uliyoyapata, ingawa inaweza ikatokea kua umekulia kwenye mazingira hasi ila ukawa na fikra chanya na pia ukakulia kwenye mazingira chanya ila ukawa na fikra hasi..hii inategemea na njia gani uliyoamua kuichukua baada ya kuona ndio njia bora kwako…ni vizuri pia kama ukiamua kuchukua njia yako mwenyewe na pia kutengeneza njia kwa wengine kama buibui kwa fikra za kwamba nitaweza ili upate amani, imani na ari ya kufika unapotaka kufika…kama hakiendi sawa na ulivyotarajia kiende basi usife moyo…wataalamu wanasema “kama huwezi kukibadilisha basi jibadilishe wewe”.. mfano una rafiki yako ambaye huwa unamfikiria kwa ubaya kwa sababu ya mabaya anayoyafanya,  basi jibadilishe fikra zako bila kumbadilisha yeye, kisha utaona uzuri wake... Usijinyime furaha kwakua huwawezi, amua kuungana nao ili uwajue ama ujue kisha utajua nini kinaendelea, ama amua kuachana nao kisha ufanye kitu kingine…tumia nafasi unapoitambua, usianze kuchanganua tena nafasi uliyoipata wakati muda unakuacha. Unaweza ukasimamisha saa lakini hauwezi kisimamisha wakati.

          Lengo ni tujipe muda wakujitambua mapungufu yetu na uwezo wetu, tambua ya kwamba mapungufu makubwa ni kujizuia watu wasijue mapungufu yao. Nakumbuka katika makala ya "A Mirror"… “KIOO” niligusia umuhimu wa kuwa karibu na watu tunaowaona wanaendana na sisi, na maana ya kwamba: kuwa karibu na watu ni kama kujitazama kwenye kioo, kwamba ukaribu wetu na watu ndio tunavyojiona vizuri, kama tunavyojitazama kwenye kioo,u kiwa karibu ndio unavyojiona vizuri. Kwani watu hawa wanakua kama kioo na wanatuwezesha tujitambue uwezo wetu na mapungufu yetu. katika makala hii niliwashauri kua pale unapoona kioo kinaonesha picha mbaya, basi usijaribu kukivunja kwa kua ubaya hauko kwenye kioo bali ndani yako wewe, hivyo ondoa huo ubaya ndani yako na kioo kitataonesha picha nzuri. Mfano kama mume anamuona mke wake ni mbaya, basi ajue ubaya ule uko ndani yake yeye mume hivyo aondoe huo ubaya ndani yake na mkewe atonekana msafi…narudi kauli hii “huwezi ukamhisi mtu ni mwizi kama wewe sio mwizi, kama haujui kuiba kivipi utahisi kua unaibiwa?” ..KUMKICHWA ni WEWE!  

No comments:

Post a Comment