Kuna vita kubwa sana kati ya
moyo na fikra, Kati ya viwili hivi kipi hasa kinachokuongoza katika maisha yako ya kila siku, kipi
kinachokupa uhuru wako wa kufanya kile unachoona ni sawa kufanyika sawia katika
muda huo sahihi, kipi kitakachofata baada ya hapo na kipi kimeshapita bila
kukuletea matatizo. Kuna usemi wa kizungu unasema “mwache mbwa aliyelala alale”
na pia kuna wanaosema “mbwa aliyelala hatoweza kupiga kelele”. Uhuru wa fikra na wakufikiri ni wako mwenyewe
na hukupa uhuru pale unapojihisi huru ndani ya moyo na fikra zako. Vipi
utakapotambua kua kuna chembe za adui ndani yako, Je utafanyaje?
“Rafiki aweza kua adui na
adui aweza kuwa rafiki yako” huu ni usemi unaopendwa sana na na kutumiwa na
watu wengi panapotokea kuoneshana au kutoa angalizo panapotokea mfarakano baina
ya pande mbili na zaidi.
Je adui ni nani?
Adui ni upande wa pili wako
unaokuletea hofu na vikwazo katika maisha yako ya kila siku, upande huu
hupingana nawe katika kila kitu unachokifanya na ambacho unafikiria kukifanya
katika kila hatua ya maisha yako. Adui
pia aweza kuwa rafiki wa upande wa pili kwani hukuonesha vitu ambayo rafiki
yako katika urafiki wa kawaida hawezi kukuonesha. Adui aweza kua yoyote au
chochote, adui aweza kua ndugu yako, rafiki yako, adui yako na hata wewe
mwenyewe waweza kua adui yako. Lakini je adui yako wewe ni nani?
Kwa namna tulivyo wanadamu
tuna hulka za aina mbalimbali na hulka hizi zinatofautiana baina yetu kutokana
na ukuaji wetu, maisha tuliyoyapitia na vitu tulivyojifunza katika safari yetu
ya kukimbiza upepo. Kuna wengine huwa wanajihisi fahari wakifanya mema na
wengine hujihisi fahari wakifanya maovu kwani kuna mambo ambayo ni lazima
kuyafanya na pia kuna mambo ambayo ni lazima kuyaacha, lakini kwa hulka zetu
zilivyo nafsi zetu hujikuta zinafanya yasiyo ya lazima kufanya na kuishia
kuacha yale yaliyo ya lazima kuyafanya, na ndipo uadui huanza kujitokeza.
Wengine hudhani kua uadui
huletwa na chuki, lah! sio lazima kila adui awe na chuki nawe, wakati mwingine
uadui huletwa na upendo tulionao ndani ya mioyo yetu, na pale fikra zetu
zinapopingana na mioyo yetu, mfarakano na kutokuwepo usuluhishi wa tatizo.
Kinachopandwa kwa wema huvunwa kilicho chema na pia kinapopandwa cha ubaya
nacho ni sawa na kuchimba shimo, huishia kuingia mwenyewe. Umakini unatakiwa ili
kuelewa, na pia unatakiwa uelewe kuwa muda uko makini na umakini ni muda, ni vigumu
kukuta muda unapoteza muda.
Maisha ni mzunguko kama
mzunguko wa jua, litachomoza kisha litazama, mwezi utatoka na utapata mwangaza
wa jua bila hiyana ya jua, je kuna uadui kati ya jua na mwezi pale mwezi
unapopotea kwa kukosa mwangaza wa jua? kila kitu kina muda wake na muda ndio
unaongea, ukiwa na subira basi hiyo ni kheri na pia kama una uvumilivu basi
hizo ni mbivu utakazokula. Kilicho cha ukweli kitabakia kua ukweli hata
kikisemwa na aliye mwongo na kilicho cha uongo kitabakia uongo hata kisemwe na
aliye mkweli. Sio kila kitu kitabadilika kwa maamuzi ya apendaye, vingine
vitaishia kumbadilisha mwamuzi apendaye bila maamuzi. Tulichokifanya juzi, jana
na leo hakitakua na utofauti na tutakachokifanya kesho, ni sawa na kusema leo
ni kesho ya jana.
Si vyema kujidanganya kwa kujipa sababu za
kushindwa kufanya jana ulichokipanga juzi, kwakua utakifanya leo ambayo ni
kesho ya jana. Kumbuka muda uko makini na muda haupotezi muda, siku zinakwenda,
tunafanya tunayoyafanya kila siku, jua linachomoza na kuzama, mwezi unatokea
siku imekwisha na giza limeingia, juzi ni jana ikiwa leo ni kesho ya jana, bado
tunaendelea kujipa sababu ya kushindwa
kwa kuituliza nafsi kwa uongo wa kujidanganya wenyewe. Embu jiulize
unajisikiaeje pale unapodanganywa na mtu, kisha weka hiyo hali pale
unapojidanganya mwenyewe. Kwa ninavyoona
ni bora udanganywe kuliko ujidanganye.
Usijinyime kuendelea kwakua umeamua
kua hauwezi, hii ni hali ya kujizuia kwenda mbele kwa kua unajiogopa mwenyewe,
huwa kuna hulka ya kujizuia kufanya ya lazima unayotakiwa kuyafanya wakati unatumia
muda mwingi kufanya yaliyo ya lazima kuyaacha. Ni sawa kuamua kufanya na kuamua
kutokufanya, yote ni maamuzi ila faida na hasara zake ndivyo vyenye tija.
Kutokujua unachotaka na unachotakiwa
kufanya nacho ni hatari sana, ni sawa na kwenda usipopajua safari huwa ndefu
sana na kufika kwake ni kwa mashaka sana, hii inasabishwa na sisi wenyewe kutokutenga
muda wa kufikiria na kutafakari tulipotoka, tulipo na tunapotaka kufika.
Baada ya kabla na kabla ya
baada, kifikra zinachanganya ila kiuhalisia kuna wakati maisha huwa yana
changamoto zake, zingine huletwa na watu na zingine huwa tunazitengeneza
wenyewe, kuna wakati utajisikia uko chini na kuna wakati utajihisi uko juu,
kuna watakao kuvuta chini na kuna watakaokusukuma uende mbele, kila mmoja na
malengo yake kwanini uende mbele na kwanini urudi nyuma, zote ni changamoto za
maisha. Wote wana mategemo binafsi kwako, wengi wao ikiwa kuona ni vipi utakua
baada ya kabla na kabla ya baada uliovyosema utakua ama walivyodhani ndivyo
ulivyo. Kuna wanaobadilika baada na kuna wanaobadilika kabla. Adui ajae baada
ya kabla yuko nawe na aliyenawe kabla ya baada hubaki kuwa nawe, chaguo ni lako
kutambua na kuamua kumtumia yupi, zote hizi ni changamoto za maisha, pata kisha
potea au poteza, kosa kisha laumu au kufuru bado ni yuko wewe!
Muda upo ila haupo na wewe,
ila wewe ndio unatakiwa ujiweke karibu na muda, kila unachokijenga kama hakina
msingi ulioimara basi usitegemee kuvuna kwa kupanda changarawe. Mwanzo ni mgumu
ila anza, kisha komaa nacho, kifikirie kila saa na kiweke mbele yako, tazama
mbele zaidi ya upeo wa macho yako, angalia mwisho wa mwanzo wako na mwanzo wa
mwisho wako, je kuna jema, kama lipo kaza buti kisha songa mbele, changamoto ni
sehemu ya maisha, adui ni changamoto. Usipokubali kuishi kwa changamoto katika
hali uliyopo basi hautaishi na haujaishi, ni sawa na kukataa kuvuna
ulichopanda, Kila kilichopo kina sababu yake na sio sababu yako, wewe nawe ni
sababu yake, ila ni jukumu lako kutafuta sababu yako kwanini upo hapo ulipo na
kivipi utatataua changamoto yako ambayo ni wewe! kumbuka Kumkichwa ni wewe!
No comments:
Post a Comment