Sunday, May 8, 2011

"MAPiNDUZi YA KWANZA Ni KUUSHiNDA UOGA NA UBiNAFSi"

   
          Kwa kipindi kirefu tumejikuta tumekua ni watu wa kuongea sana kuliko kutenda. Kila mmoja miongoni mwetu amekua na fikra za uyeye na familia yake huku tukisahau umuhimu wa kuwa na jamii pamoja nasi. Tumesahau kua yule anazalisha kile ili na sisi tukizalisha hiki twende sawa. Ubinafsi wa nafsi umetuingia katika fikra zetu na kutunyima mwanya wakufikiria yajayo kwa taifa la kesho la wajukuu zetu, na hili limechangiwa kwa kiasi kikubwa na uoga uliopo katika nafsi zetu, kumbuka hatuwezi kuongelea taifa letu la kesho kama hatutalijenga leo, na kwa mapinduzi ya uoga ndani ya nafsi zetu utakua ni ushindi mkubwa sana kama baina yetu tutalitilia maanani suala hili.

              Uoga ni hali ya kuhisi kwamba uko kwenye hali ya hatari au jambo lolote baya linaweza kukutokea, au hali ya hatari itatokea wakati wowote. Uoga huu upo miongoni mwetu hasa pale tunapofikiria kufanya mabadiliko kwenye mfumo wetu wa maisha. Ndio maana wataalamu wanawaita watu walio katika kundi hili wahasi (mtizamo mbaya), kundi lilopoteza matumaini ya kuzishinda nafsi zao mbele ya vikwazo vinavyowarudisha nyuma.
              Nikimnukuu mwanahistoria mmoja alisema" katika ugunduzi mkubwa wa binadamu ni kwamba binadamu anaweza kubadili maisha yake kama ataweza kubadili fikra zake", alisisitiza kubadili fikra kwakua ndizo zinazompelekea mwanadamu kufanya kitakachomjia katika fikra zake. Kama fikra zitakua za uoga, basi mtu huyu atajiona yuko kwenye hatari hata kama hakuna hatari yoyote inayomkabili. Kuna usemi unaosema uking'atwa na nyoka hata ukiguswa na ujani basi utadhani ni nyoka, hii inatokana na kuwa na fikra za uoga, kama wewe ni jasiri pambana na nyoka huyo, pia kama hakuna nyoka ya nini kuogopa jani.
             Jambo la muhimu na la msingi ni kusimama imara kwa fikra zenye matumaini katika kila jambo pasipokua na uoga. Ni dhahiri binadamu tumekua na hulka ya kujisaliti wenyewe kabla hatujasalitiwa, na hii inadhihirisha pale tunapoamua kulala wakati jua linachomoza, tunapofurahia mkulima anapokula mbegu, tunapojadili kila siku ni nani wakumfunga paka kengele, tunapolaumiana kwa kunyoosheana vidole kwamba yule kafanya vile huyu kafanya hivi, tunaposhangilia mtoto wa jirani yetu anapoanguka anapojaribu kutembea wakati mtoto wako angali bado yupo tumboni mwa mama yake.
              Ningependa kuwasisitiza sana vijana wenzangu kwamba mapambano bado yanaendelea, uwe umeyaona ama hujayaona, na maisha yenyewe ni mapambano tosha, na kwa ubinafsi na uoga tulionao, hatutafika popote, tutazunguka na kurudi pale pale tulipotoa. Mabadiliko yanahitajika miongoni mwetu katika jamii zetu, mapinduzi ya kuushinda uoga katika nafsi sio madogo, ingawa  hayahitaji kushika mtutu, bali kukaa na kuangalia ulipotoka ni wapi na ni wapi unapotaka ufike. Kuna mbinu mbalimbali za kushinda, ila kwakua ubinafsi na uoga ndio vimetutawala, yatupasa tuanze na nafsi zetu kwanza kwa kuondoa fundo la mchanga lililo machoni mwetu, kisha ndipo tumtazame jirani yetu tumtoe kakijiti kalicho jichoni mwake. Mapinduzi haya yanaanza kwako wewe mwenyewe, kisha yatasambaa yenyewe kama yatakua ni yenye harufu nzuri, ila ukishindwa usinilaumu mimi kwakua mapinduzi haya yanaanza na wewe. Ndio maana tunasema Kumkichwa ni WeWe!  


kajiabeid(c)2011

No comments:

Post a Comment