Thursday, June 16, 2011

"Kwa miaka 50 ni fikra masikini na sio nchi masikini."

“Umasikini wa fikra ni umasikini mkubwa na hatari sana kuliko umasikini wowote hapa duniani” hii ni kauli ya marehemu Baba wa Taifa. Tokea mwaka kumi na tisa sita na moja mpaka sasa mwaka wa ishirini moja na moja, wimbo wa pili wa taifa umekua "Tanzania, Tanzania ni nchi masikini", lakini kiukweli Tanzania sio nchi masikini, sisi wananchi ndio masikini, tena sio masikini wa vipato, bali masikini wakubwa wa fikra.
Katika kujua/kutambua zuri au baya mtu binafsi aliye na akili timamu ndiye huweza kutiliwa maanani pale anapofanya maamuzi, na maamuzi haya huwa yanafanywa kwa fikra sahihi za mtu huyo na panapotokea mapungufu katika fikra hizo basi ujue hata maamuzi yatakua na mapungufu. Tumekua tukiwalaumu sana watu wengine kwa maamuzi wanayoyafanya wao bila kutambua kua wakulaumiwa sio wao bali ni sisi tuliofanya maamuzi kabla ya kufikiri na kutafakari maneno yao kwa umakini. Kwakua baba wa taifa alishasema "SiASA Ni MCHEZO MCHAFU", sintopenda makala hii ihusishwe na siasa.
Katika fikra zetu kama wanajamii tunatakiwa tuwe ni watu wakufanya maamuzi endelevu yenye vyanzo vyenye uhalisia wa maisha yetu kama watanzania, yawe ni maamuzi ambayo yanaweza kujadiliwa na wanajamii, kukubalika na kisha kufanyiwa kazi na kuleta matokeo endelevu na sio potevu. Hivyo pale tutakapokaa na kuanza kutoa lawama kwa mwingine tujitambue ya kwamba tunakataa uhalisia kwamba wakosaji ni sisi, lakini pale tutakapokaa chini na kutaka kumjua mchawi ni nani, tutaishia kujikamata wenyewe.
Fikra masikini ziko na sisi kwakua tunajihusisha na umasikini ambao hautaki kua karibu na sisi. Nchi yetu sio masikini ila wananchi wake ndio tuna fikra masikini. Hakuna hata siku moja Tanzania itaitwa nchi tajiri kama wananchi wake hatakua na fikra za kitajiri, kwakua fikra masikini zinaleta umasikini, na fikra tajiri zinaleta utajiri. Fikra masikini hizi hazina tofauti na fikra za mrengo wa kushoto ama fikra hasi na pia fikra tajiri ni mrengo wa kulia ama fikra chanya.
Kwa miaka mingi sasa watanzania tumekua ni watu wakukata tamaa na kupoteza malengo kwa kuwa tunajidhania ni masikini, na tukijisahau kwamba kama tukijifikiria kuwa hatuwezi tunajiondolea matumaini ya kutokuweza, je! ni sera ngapi na mipango imekwisha pitishwa bila kufanikiwa?, yote haya yamepotea kama mvuke kwakua hatuna tole la matumaini, tunajiona kwamba hatuwezi, ila kama mtu angetambua umuhimu wa tone moja la maji ya mvua, basi angeheshimu maji ya dimbwi.  Tumekua ni watu wakujidharau kana kwamba ni tone moja katika bahari hivyo halitaleta mabadiliko.
Tutambueni umuhimu wetu ndio unaunda kitu, umoja wetu ndio nguvu yetu, sasa kwanini hatutumii mwanga wa jua kuona, tunasubiri mpaka kiza kiingie ndipo tutoe lawama kwa mtengeneza kandili. Tumekua watu tegemezi sana, tunachezea nguvu na mali kazi zetu, tumekua waongeaji sana kuliko kutenda, wengi wa lawama kwa wao na sio kwa sisi, tumekua sio wenye kujifunza tunapofanya makosa. Tazama asiyejua kusoma anajitamba kwamba anajua kusoma, na asiyetaka kurekebishwa. Tazama asiyejua hataki kufundishwa, tazama anayejua anakataa kumfundisha asiyejua. Tunajiona bora kuliko wabora. Tumekua watu wa bora jana, leo sijui itakuaje, leo ikija, kesho mwenyezimungu ndiye atakayeipanga, jamani kesho haifiki kwakua kuna jana, ila leo ipo kila leo.
Sasa twatimiza miaka hamsini kwa teknohama za wenzetu wakati zakwetu twaogopa kuzitoa eti ni za kishamba!, sasa zipi ni za kiofisi ama za kiwanja ama kijanja,ni fikra tu ndizo zinatufanya tijifikirie vibaya, kwanini tunalionea sana shamba, hakuna mjanja wala mshamba katika ubunifu wa kuleta maendeleo, wenzetu mashamba ndio yayofanya teknohama zinaibuka, sisi mashamba yetu tumeeyaacha tunakimbilia mjini kufanya biashara ya kuuza alichotengeneza jirani yetu. Sisi tumekua wanunuzi wa kila kitu, kuanzia kifaa ,elimu ya kutumia, spea, vifaa vya kufungia.Yaani tumetawaliwa kifkra na kusahau kua ukitawaliwa, mkombozi wako ni wewe mwenyewe kujiondoa kwa mtawala huyo.  Kuna umuhimu mkubwa sana wa sisi kua wazalishaji kuliko kung’ang’ania kuwa wauzaji na wanunuaji, tunapunguza kipato chetu kwa kununua kuliko kuzalisha.
Ukitazama kwa makini utatambua kwamba sisi sio watumwa katika utumwa ule wa zamani, ila sisi ni watumwa wa kileo wa kifikra, tunatafuta kazi kwa mabwana/watwana ili tuwazalishie malighafi zetu, kisha wanatupa ujira, ujira huo tunaenda kununua tulichokizalisha kwa bwana yule, kesho tena tunarudi kuomba kazi, yaani ni kautumwa kaliko kwenye fikra zetu kwa kuwa tumekua wavivu wa kufikiri na kuunda njia mpya za kujikwamua kiuchumi. Hivi ni kwamba nchi yetu haina wataalamu wakuweza kubuni njia ya kuwapatia ajira vijana? Hata kuwamilikisha  mashamba kwa vikundi ni jambo lenye tija, kisha wakishalima serikali iyanunue mazao yao kisha iyapeleke kwenye viwanda au serikali iwatafutie masoko nje ya nchi. Au iwawezeshe kisha vijana watafanya watakavyoona ni sawa kufaanya kwa sera za vikundi vyao.
Watanzania tunaweza kubadili fikra zetu na kisha kuiletea nchi yetu maendeleo. Kuna usemi kwamba “sijafika pale nilipotaka kufika ila ninashukuru hapa nilipofika”, ila kama ndipo hapa tulipo mimi nasema bado kwa sababu kuna wakati hapo nyuma kuna kitu kilienda ndivyo isivyo. Ila kwa miaka hii hamsini ni miaka ya wananchi wenye fikra masikini na sio ya nchi masikini wala ya wananchi masikini. Kumkichwa ni wewe!
                                                                                   Kajiabeid©2011

No comments:

Post a Comment