Friday, March 23, 2012
Monday, March 19, 2012
Sunday, March 18, 2012
Thursday, March 15, 2012
Weusi-watoto wa mungu.wma - Hulk Share - Music Distribution Platform
Wednesday, March 14, 2012
"Siku Maji yakirudi nyuma"
Litakua ni jambo la kushangaza pengine na kutupumbaza kuona siku hiyo... kivipi maji yamerudi nyuma badala ya kwenda mbele!..., ni mshangao ambao utatufanya wengi wetu tustaajabu ya kuwa ni kivipi maji haya yamerudi nyuma! Tutabaki tukijiuliza kwakua tumekua ni wagumu kuelewa kwamba maji yanaweza yakarudi kama mambo hayatakwenda namna yanavyotakiwa yaende au kama tutaendela na mfumo wetu wakuacha mambo yaende kama wanavyotaka na sio kama tunavyotaka sisi yaende kwa kujishirikisha kwenye shughuli za kila siku za ujenzi wa taifa letu.
Tukiwa kama watazamaji wa mambo yanavyoenda kila kukicha bila kuwa watendaji na washiriki katika kufanikisha mambo yaende vile sisi tunataka, hatuna budi kukubalia na hali itakavyokuja kubadilika kwa kushuhudia maji yanayotoka katika Ziwa letu la Victoria yenye Upendo na Amani ya miaka hamsini kisha kupita katika Mto Naili yakiwa yanasambaza Upendo na Amani kwa nchi za Sudan, Libya, Somali na Misri na kisha kumwagika katika bahari ya Sham yakirudi na chuki, vurugu, vita, mageuzi kutoka nchi ya Misri, Libya, Somalia na Sudani na kurudi nchini kwetu na kusambaza ari hizo kwa wananchi wetu wenye amani na upendo, kwa kusahau kwetu misingi iliyotujengea na kutupa Amani na Upendo kwa miaka hamsini tukiwa huru kwa kujitawala.
Tumeshuhudia yaliyotokea Misri, tumekuwa wazungumzaji wazuri kwa yaliyotoka Libya, tumewahurumia na kushuhudia mgawanyiko uliotokea Sudani. Sasa kwa haya yaliyotokea katika nchi hizi hata nchini kwetu yanaweza yakatokea muda wowote na saa yoyote. Lakini itakuwa hivyo kama tutakuwa wagumu kutambua ni wapi panapokwenda tofauti na namna panavyotakiwa paende.
Kwa namna gani tunatakiwa tuwajibike vilivyo katika shughuli zinazotuhusu.Tusiishie kuwa watazamaji na wasemaji, eti kwakua kuna watu tumewateua wasimamie shughuli zetu basi sisi tukalale tusubiri watufanyie kila kitu , tabia hii itatuletea lawama juu yao na sio juu yetu kwakua hakuna anayetaka kubeba mzigo wa miiba alioujaza yeye mwenyewe. Huyu kakosea yule kamsema, yule aliyesemwa nae kaamua kusema mabaya ya mwenzake. Huyu anakataa kujiuzulu kwakua anapenda madaraka, amekosea lakini hataki kuwajibika kwakua anapenda madaraka. Maji yakirudi nyuma vipi atatulaumu kwanini yamerudi nyuma wakati yeye hataki kuwajibika!.
Tazama wanasema chochote ili vyombo vya habari vipate chakuandika, tazama namna vyombo vya habari vimeteka vichwa vya watu. Kinachoongelewa jioni ya leo kesho utakikuta kwenye kichwa cha habari. Maigizo ya wasanii wasiopenda jina la wasanii. Wanachezea matope kisha wanajisafisha kwa maji yenye matope na kujiita wasafi. Siku maji yakirudi nyuma watatuuliza nani ni mchafu.
Wanachukua kisicho halali kwa njia zisizohalali kwa kuihalalisha kua ni halali. Tazama yatima analia mpaka machozi yanakauka hana wakumdekea, kilicho halali yake kimehalalishwa tumboni kwa walaji, hana chake, aliyetoa katoa kwa asiyenacho, kapokea mwakilishi wake na kimeliwa na mwakilshi wake kwa kujaza tumbo lake, yatima hana chake, anatamani maji yarudi nyuma. Hali ibadilike apate chake, chozi lake thamani yake kwake kwani linampunguzia huzuni iliyomo ndani ya moyo wake. Bora limtoke apate faraja yake kwani baada ya chozi la mwisho kufutika ana imani furaha itajitokeza.
Najiuliza Siku Maji yakirudi nyuma sijui hali itabadilika, aliye na uwezo wa kuona mbali kwa jicho la tatu, ajaribu kutazama aone namna maji yatakavyorudi nyuma. Ukisoma makala hii kwa makini utanielewa kwanini nawasihi tuombe sana maji yasije yakarudi nyuma. Tazama namna umasikini wetu unavyoujenga utajiri wao, mwerevu atanielewa tofauti na hapo sintowashangaa sana mkinipinga, kwani mi husema niyaonayo. Ukibishana na mjinga atakushinda kwa ujinga, na wewe utakua mjinga mkubwa mbele ya mjinga, ni ujinga kuogopa kifo cha kuku wakati ndio kitoweo ulichonacho, narudia tena matatizo yetu ndio mtaji wao.
Tunapokosa matumaini wao hutupa faraja kwa “mkinichagua mimi nitatatua shida zenu, nawahakikishia kua thamani ya shilingi itapanda, nitawajengea barabara, shule, hospitali, visima vya maji nchi yetu itakua na maendeleo na itapiga hatua kubwa kiuchumi duniani. Miaka inakwenda anashika hatamu, miaka inakwenda awamu inakwisha, hajafanya kitu anarudi tena na matumaini mengine na ahadi nyingine nyingi, akimaliza amamu zake mwingine anapokea kijiti, anaendelea kukikimbiza kwa ahadi zisizotekelezeka na zilizotelekezwa. Sisi tumebakia kulalama kwa maneno makali bila yakujua kesho yetu itakuaje. Tuombeeni maji yasije yakarudi nyuma sababu itakua ni vilio juu ya kilio.
Tuombe usifike wakati ujasiri ukaushinda uoga, kwani kifo kitakua ushujaa na uhai utabakia aibu, wananchi watakapoona fahari ya kupoteza walichokuanacho kwa ujasiri wakupigania wasichokuanacho. Hawatasikia la mwadhini wala la mnadi swala, vijana watakapopita mbele kwa ujasiri wakutaka kumvisha paka kengele. Tuombee maji yasije yakarudi nyuma.
Wengi wameniuliza mbona kila siku wewe huongea tu matatizo bila kutoa suluhisho la matatizo. Ni kwamba shida zetu zinaletwa na matatizo na matatizo yanaletwa na sisi wenyewe kwakua tumekua wagumu wa kuelewa na wakuona ukweli na kuchukua hatua. Tunatatua shida na kuacha tatizo, bila kujua tatizo ni vigumu kwetu sisi kumaliza matatizo yetu. Mfano vijana wanashida ya kupata ajira kwakua kuna tatizo katika mfumo mzima wa ajira kwa vijana, sasa badala ya kuubadilisha mfumo mzima ambao ndio tatizo, tunatatua shida ya ajira kwa kuwapa baadhi ya vijana ajira na kujivunia kua ukosefu wa ajira umepungua.
Nimendika nilichokiona na kinachokuja mbele yetu kama hatakua mstari wa mbele katika kubadilisha mfumo nyonyevu unaotunyonya fikra zetu hai kwa kutuosha kwa starehe zisizo na umuhimu katika maisha yetu ya sasa na ya baadae. Tumetekwa na vyombo vya habari kwakua hatutaki kuchanganya akili zetu na tulichokisikia na tulichoambiwa ama tulichokiona. Mbayuwayu alitaka kua na mdomo uliochongoka, aliambiwa ili uwe mzuri basi aende juu kisha ashuke chini na augonge mdomo wake kwenye jiwe, akafanya kama alivyoshauriwa ila alipokaribia jiwe lile akasema “AKILI KUMKICHWA” nisije ni kafa bure, akaokoka kifo kwa kusikia alichoambiwa na kuchanganya na akili yake, je wewe unachanganya akili yako na ulichoambiwa au unaenda tu kwa amri ya mwenye cheo?, siku maji yakirudi nyuma utanikumbuka kwa kusema kumkichwa ni mimi… ila mimi sintochoka kukukumbusha ya kua KUMKiCHWA NI WEWE!
Tuesday, March 13, 2012
Friday, March 9, 2012
"JITAMBUE KWA FIKRA CHANYA"
Kujijua ama kujitambua ni namna ya kufahamu uwezo wako ulionao katika kuweza na kutokuweza kwako. Kujua ama kutambua ni hali ya kupata ufahamu juu ya kitu au jambo Fulani ambalo ulikua hauna ufahamu nalo hapo mwanzo.
Kuna kutambua/kujitambua kwa aina mbalimbali, kuna kutambua kwa kugundua mwenyewe, kujijua uwezo wako kua unaweza/ huwezi kufanya kitu au kuwa katika hali fulani bila kuambiwa na mtu mwingine bali kwa kutambua mwenyewe, mfano mimi naweza kuchora, kuimba, kusoma au kutangaza kwakua nilishajaribu na nikaweza. Pia kuna kutambua kwa kuambiwa na mtu/watu, hii inatokana na watu hasa walio karibu yako kukujuza kua unaweza kitu fulani ambacho wewe mwenyewe ulishindwa kutambua kua unaweza/huwezi kukifanya mfano; utaambiwa na mtu /watu kwamba “unajua wewe ni mbunifu, kwanini usiendeleze ubunifu wako?” au “unajua wewe sio mwadishi mzuri, jaribu fani nyingine au jaribu kwa njia nyingine!”. Pia kujitambua baada ya kufanya jambo fulani kwa kutambua matokeo ya jambo hilo ulilolifanya, na mwisho kutambua kwa jambo walilofanya walimwengu.
Kwa ujumla kutambua/kujitambua huku huwa kunaweza kuletwa kwa fikra chanya au kwa fikra hasi.
Fikra hasi ni fahamu/hisia zinazomjia mtu kwa hali ya kumfanya ajione ni mwenye kushindwa, fikra hizi mimi hupenda kuziita kuwa ni fikra za mrengo wa kushoto ambao humfanya mtu ajijaze mawazo ya kushindwa kutatua jambo kwa urahisi. Fikra hizi hasi huwa zinaambatana na misukosuko isiyoisha. Huwa zinamfanya mtu kuelekeza baya penye ubaya na kufanya mabaya juu ya mabaya, ingawa kuna muda fikra hasi zinaweza kumsaidia mtu kujitambua ila kama mtu huyu akiwa hasi sana ni vigumu kujua uchanya wa fikra hasi.
Katika kujitambua kifkra, fikra hasi ndizo zinazoshusha munkari, fikra hizi pia huwa na dhana ya kushindwa/ kutokuweza ama kukata tama kabisa, na humfanya mtu adumae kimawazo kwakujiona hawezi. Kwa mfano mtu anaweza kua na fikra chanya na kujitambua kua anauwezo wa kufanya jambo fulani lakini pale anapokutana na kikwazo/vikwazo mtu huyu hujiwa na fikra hasi kuwa hawezi kufanya hilo jambo ndio maana vikwazo hivyo vimejitokeza. Humfanya mtu ajiweke kwenye nadharia mbalimbali za kushindwa na kuwapa lawama wao na sio yeye. Kiuhalisia hakuna anayeshindwa kama atajimbua anaweza na hata akikumbana na vikwazo atavitatua kama atakua na fikra kwamba hakuna kinachoshindikana chini ya jua.
Mtu pia hujitambua mwenyewe uwezo wake kama atapata muda wa kukaa na kujifikiria, kwa kutumia uhasi wa fikra mtu huyu huweza kujitambua kwa kuelewa fikra hasi alizonazo, pia kwa kuambiwa na watu kwamba yuko na fikra hasi, pia jambo atakalolifanya kwa maamuzi yako humpelekea mtu kujitambua fikra hasi zake, pia kwa kutazama mienendo na matendo ya walimwengu mtu huweza kuzitambua fikra hizi. Cha muhimu pale panapokua na fikra hasi ni vizuri mtu kuzitambua kwa uhalisia na kisha kuzichanganua kwa fikra chanya.
Fikra chanya ni zile zenye kuleta matokeo yenye kuendeleza mwenendo bora baina ya watu au mtu. Fikra hizi mimi huziita ni fikra za mrengo wa kulia. Humfanya mtu akajitambue bila kuleta uhasama na bila kutupa lawama kwa wao wala kwa nafsi yake. Kwakua fikra hizi huzaa uchanya panapo uhasi na uchanya penye uchanya, hizi huwa ni fikra bora zinazomjengea mtu imani pale panapotokea ugumu wa jambo au vikwazo , mtu huyu hutambua vikwazo kama nafasi ya kufanikisha anachotaka kukifanya. Fikra zenye uchanya kuwa zinaleta matumaini pale yanapokosekana, fikra hizi muda wote huwa hai na mwenye nazo huwa ni mtu wa kufikiria yaliyo mazuri na kama akiona ubaya huwa anatambua uwepo wa ubaya kua ni chanzo cha uzuri na uzuri unategemea uwepo wa ubaya.
Katika kujitambua kwetu fikra ndio zinatufanya tuwe na uwezo wa kujitambua, na katika aina za kujitambua, ubora uko pale mtu anapojitambua yeye mwenyewe pasipo kuambia. Ugunduzi huu humfanya mtu kujiamini na kujielewa uwezo wake, pia huweza kumbadilisha mtu akawa mwenye furaha kwa kujitambua mwenyewe uwezo wake na mapungufu yake. Kuna usemi unasema “majadiliano bora kuliko yote ni yale unayoyafanya wewe mwenyewe ndani ya moyo wako na ndani ya fikra zako kisha ukakubaliana nazo”
Kuna vitu ambavyo vinatuzuia tusiweze kujitambua, katika vitu hivi vinavyowazuiwa watu kujitambua kimojawapo kikubwa ni muda wa kutafakari mambo yetu na mienendo yetu wenyewe. Na hii ni kwasababu watu wengi hasa Watanzania huwa tunafuatilia sana maisha ya watu kuliko ya kwetu sisi wenyewe. Tuna katabia cha nani kafanya nini? nani alifanya nini? badala ya kujipa muda wakujitambua wenyewe kwamba mimi nafanya nini? nifanye nini? ni wapi nilikosea? wapi nirekebishe? ni wapi kuna nafasi niitumie? kwa muda gani natakiwa niitumie hiyo nafasi ili niweze kufanikisha? malengo yangu ni yapi? je yamefanikiwa? yameshindikana wapi?. Huwa tunajinyima haki ya msingi ya kujitambua wenyewe kwa kuwa tunawekeza muda na fikra zetu kwa wao na yeye kwa mambo yasiyo na msingi, na kujinyima muda wa mimi nifanye nini kwa yaliyo na msingi ili nitimize malengo yangu.
Kama ukiweza/umeweza kujitambua kua utaweza/ unaweza nini! Ni vizuri ukaondokana na fikra hasi za kwamba hauwezi, jaribu kutambua uwezo na mapungufu yako kutumia uhalisia wa maisha yako mwenyewe ambayo ni mkusanyiko wa mafunzo mbalimbali ya kuweza na kukosea uliyoyapata tokea umeanza kutambua zuri na baya. Nakusihi utambue ya kwamba mafunzo yanayochukua nafasi kubwa katika maisha yetu ni yale tunayojifunza wenyewe, ambapo ndipo kujitambua kunapotokea.
Kama binadamu basi sio vibaya sana pale unapokua na fikra mbalimbali juu ya jambo, mtu au kitu, na hii ni kutokana na namna ulivyokuzwa au malezi uliyoyapata, ingawa inaweza ikatokea kua umekulia kwenye mazingira hasi ila ukawa na fikra chanya na pia ukakulia kwenye mazingira chanya ila ukawa na fikra hasi..hii inategemea na njia gani uliyoamua kuichukua baada ya kuona ndio njia bora kwako…ni vizuri pia kama ukiamua kuchukua njia yako mwenyewe na pia kutengeneza njia kwa wengine kama buibui kwa fikra za kwamba nitaweza ili upate amani, imani na ari ya kufika unapotaka kufika…kama hakiendi sawa na ulivyotarajia kiende basi usife moyo…wataalamu wanasema “kama huwezi kukibadilisha basi jibadilishe wewe”.. mfano una rafiki yako ambaye huwa unamfikiria kwa ubaya kwa sababu ya mabaya anayoyafanya, basi jibadilishe fikra zako bila kumbadilisha yeye, kisha utaona uzuri wake... Usijinyime furaha kwakua huwawezi, amua kuungana nao ili uwajue ama ujue kisha utajua nini kinaendelea, ama amua kuachana nao kisha ufanye kitu kingine…tumia nafasi unapoitambua, usianze kuchanganua tena nafasi uliyoipata wakati muda unakuacha. Unaweza ukasimamisha saa lakini hauwezi kisimamisha wakati.
Lengo ni tujipe muda wakujitambua mapungufu yetu na uwezo wetu, tambua ya kwamba mapungufu makubwa ni kujizuia watu wasijue mapungufu yao. Nakumbuka katika makala ya "A Mirror"… “KIOO” niligusia umuhimu wa kuwa karibu na watu tunaowaona wanaendana na sisi, na maana ya kwamba: kuwa karibu na watu ni kama kujitazama kwenye kioo, kwamba ukaribu wetu na watu ndio tunavyojiona vizuri, kama tunavyojitazama kwenye kioo,u kiwa karibu ndio unavyojiona vizuri. Kwani watu hawa wanakua kama kioo na wanatuwezesha tujitambue uwezo wetu na mapungufu yetu. katika makala hii niliwashauri kua pale unapoona kioo kinaonesha picha mbaya, basi usijaribu kukivunja kwa kua ubaya hauko kwenye kioo bali ndani yako wewe, hivyo ondoa huo ubaya ndani yako na kioo kitataonesha picha nzuri. Mfano kama mume anamuona mke wake ni mbaya, basi ajue ubaya ule uko ndani yake yeye mume hivyo aondoe huo ubaya ndani yake na mkewe atonekana msafi…narudi kauli hii “huwezi ukamhisi mtu ni mwizi kama wewe sio mwizi, kama haujui kuiba kivipi utahisi kua unaibiwa?” ..KUMKICHWA ni WEWE!
Subscribe to:
Posts (Atom)