Thursday, May 5, 2016

Tafakuri ya Kumkichwa: ADUI YAKO NI NANI?




Kuna vita kubwa sana kati ya moyo na fikra, Kati ya viwili hivi kipi hasa kinachokuongoza katika maisha yako ya kila siku, kipi kinachokupa uhuru wako wa kufanya kile unachoona ni sawa kufanyika sawia katika muda huo sahihi, kipi kitakachofata baada ya hapo na kipi kimeshapita bila kukuletea matatizo. Kuna usemi wa kizungu unasema “mwache mbwa aliyelala alale” na pia kuna wanaosema “mbwa aliyelala hatoweza kupiga kelele”.  Uhuru wa fikra na wakufikiri ni wako mwenyewe na hukupa uhuru pale unapojihisi huru ndani ya moyo na fikra zako. Vipi utakapotambua kua kuna chembe za adui ndani yako, Je utafanyaje?

“Rafiki aweza kua adui na adui aweza kuwa rafiki yako” huu ni usemi unaopendwa sana na na kutumiwa na watu wengi panapotokea kuoneshana au kutoa angalizo panapotokea mfarakano baina ya pande mbili na zaidi.

Je adui ni nani?
Adui ni upande wa pili wako unaokuletea hofu na vikwazo katika maisha yako ya kila siku, upande huu hupingana nawe katika kila kitu unachokifanya na ambacho unafikiria kukifanya katika kila hatua ya maisha yako.  Adui pia aweza kuwa rafiki wa upande wa pili kwani hukuonesha vitu ambayo rafiki yako katika urafiki wa kawaida hawezi kukuonesha. Adui aweza kua yoyote au chochote, adui aweza kua ndugu yako, rafiki yako, adui yako na hata wewe mwenyewe waweza kua adui yako. Lakini je adui yako wewe ni nani?

Kwa namna tulivyo wanadamu tuna hulka za aina mbalimbali na hulka hizi zinatofautiana baina yetu kutokana na ukuaji wetu, maisha tuliyoyapitia na vitu tulivyojifunza katika safari yetu ya kukimbiza upepo. Kuna wengine huwa wanajihisi fahari wakifanya mema na wengine hujihisi fahari wakifanya maovu kwani kuna mambo ambayo ni lazima kuyafanya na pia kuna mambo ambayo ni lazima kuyaacha, lakini kwa hulka zetu zilivyo nafsi zetu hujikuta zinafanya yasiyo ya lazima kufanya na kuishia kuacha yale yaliyo ya lazima kuyafanya, na ndipo uadui huanza kujitokeza.

Wengine hudhani kua uadui huletwa na chuki, lah! sio lazima kila adui awe na chuki nawe, wakati mwingine uadui huletwa na upendo tulionao ndani ya mioyo yetu, na pale fikra zetu zinapopingana na mioyo yetu, mfarakano na kutokuwepo usuluhishi wa tatizo. Kinachopandwa kwa wema huvunwa kilicho chema na pia kinapopandwa cha ubaya nacho ni sawa na kuchimba shimo, huishia kuingia mwenyewe. Umakini unatakiwa ili kuelewa, na pia unatakiwa uelewe kuwa muda uko makini na umakini ni muda, ni vigumu kukuta muda unapoteza muda.

Maisha ni mzunguko kama mzunguko wa jua, litachomoza kisha litazama, mwezi utatoka na utapata mwangaza wa jua bila hiyana ya jua, je kuna uadui kati ya jua na mwezi pale mwezi unapopotea kwa kukosa mwangaza wa jua? kila kitu kina muda wake na muda ndio unaongea, ukiwa na subira basi hiyo ni kheri na pia kama una uvumilivu basi hizo ni mbivu utakazokula. Kilicho cha ukweli kitabakia kua ukweli hata kikisemwa na aliye mwongo na kilicho cha uongo kitabakia uongo hata kisemwe na aliye mkweli. Sio kila kitu kitabadilika kwa maamuzi ya apendaye, vingine vitaishia kumbadilisha mwamuzi apendaye bila maamuzi. Tulichokifanya juzi, jana na leo hakitakua na utofauti na tutakachokifanya kesho, ni sawa na kusema leo ni kesho ya jana.

 Si vyema kujidanganya kwa kujipa sababu za kushindwa kufanya jana ulichokipanga juzi, kwakua utakifanya leo ambayo ni kesho ya jana. Kumbuka muda uko makini na muda haupotezi muda, siku zinakwenda, tunafanya tunayoyafanya kila siku, jua linachomoza na kuzama, mwezi unatokea siku imekwisha na giza limeingia, juzi ni jana ikiwa leo ni kesho ya jana, bado tunaendelea kujipa sababu  ya kushindwa kwa kuituliza nafsi kwa uongo wa kujidanganya wenyewe. Embu jiulize unajisikiaeje pale unapodanganywa na mtu, kisha weka hiyo hali pale unapojidanganya mwenyewe.  Kwa ninavyoona ni bora udanganywe kuliko ujidanganye.

Usijinyime kuendelea kwakua umeamua kua hauwezi, hii ni hali ya kujizuia kwenda mbele kwa kua unajiogopa mwenyewe, huwa kuna hulka ya kujizuia kufanya ya lazima unayotakiwa kuyafanya wakati unatumia muda mwingi kufanya yaliyo ya lazima kuyaacha. Ni sawa kuamua kufanya na kuamua kutokufanya, yote ni maamuzi ila faida na hasara zake ndivyo vyenye tija.

Kutokujua unachotaka na unachotakiwa kufanya nacho ni hatari sana, ni sawa na kwenda usipopajua safari huwa ndefu sana na kufika kwake ni kwa mashaka sana, hii inasabishwa na sisi wenyewe kutokutenga muda wa kufikiria na kutafakari tulipotoka, tulipo na tunapotaka kufika.

Baada ya kabla na kabla ya baada, kifikra zinachanganya ila kiuhalisia kuna wakati maisha huwa yana changamoto zake, zingine huletwa na watu na zingine huwa tunazitengeneza wenyewe, kuna wakati utajisikia uko chini na kuna wakati utajihisi uko juu, kuna watakao kuvuta chini na kuna watakaokusukuma uende mbele, kila mmoja na malengo yake kwanini uende mbele na kwanini urudi nyuma, zote ni changamoto za maisha. Wote wana mategemo binafsi kwako, wengi wao ikiwa kuona ni vipi utakua baada ya kabla na kabla ya baada uliovyosema utakua ama walivyodhani ndivyo ulivyo. Kuna wanaobadilika baada na kuna wanaobadilika kabla. Adui ajae baada ya kabla yuko nawe na aliyenawe kabla ya baada hubaki kuwa nawe, chaguo ni lako kutambua na kuamua kumtumia yupi, zote hizi ni changamoto za maisha, pata kisha potea au poteza, kosa kisha laumu au kufuru bado ni yuko wewe!

Muda upo ila haupo na wewe, ila wewe ndio unatakiwa ujiweke karibu na muda, kila unachokijenga kama hakina msingi ulioimara basi usitegemee kuvuna kwa kupanda changarawe. Mwanzo ni mgumu ila anza, kisha komaa nacho, kifikirie kila saa na kiweke mbele yako, tazama mbele zaidi ya upeo wa macho yako, angalia mwisho wa mwanzo wako na mwanzo wa mwisho wako, je kuna jema, kama lipo kaza buti kisha songa mbele, changamoto ni sehemu ya maisha, adui ni changamoto. Usipokubali kuishi kwa changamoto katika hali uliyopo basi hautaishi na haujaishi, ni sawa na kukataa kuvuna ulichopanda, Kila kilichopo kina sababu yake na sio sababu yako, wewe nawe ni sababu yake, ila ni jukumu lako kutafuta sababu yako kwanini upo hapo ulipo na kivipi utatataua changamoto yako ambayo ni wewe! kumbuka Kumkichwa ni wewe!