Wahenga walisema utaicheza ngoma kadiri utakaisikia midundo yake, na hii inadhihirisha kwamba mdundo utakaposimama basi yakubidi kusimama. Dunia tunayoitengeneza ndio Dunia tutakayoishi. Ukiutazama mfumo wa maisha tunayoishi ni mfumo ambao tunautengeneza sisi wenyewe kwa maaumuzi yetu kisha tunaufuata mfumo huo kama unavyotutaka tuufate. Matakwa yetu ndio yanayotufanya tuunde mifumo hii ya maisha, kisha ili kutimiza matwaka yetu inatupasa kuufata mfumo tuliouunda.
Dunia imekua kama ngoma tunayoiunda sisi wenyewe kisha tunaanza kuicheza kufuatana na midundo yake. Kuna midundo mbalimbali inayotoka katika ngoma hii tuliyoitengeneza, ambayo inatubidi tuifate wenyewe, na baadhi ya midundo ni lazima uifate sio hiari yako, kuifata ni lazima ili uendane na wenzako walio katika mfumo.
Katika sayansi na teknolojia tunazoziunda kila siku, tunajikuta tunaunda na kuvumbua aina mbalimbali za mashine na taaluma mpya kila kukicha. Kwa mafano nguvu za nyuklia ni moja ya matokeo ya sayansi na teknolojia ya wanadamu katika ugunduzi, lakini gharama za kuitunza na athari zake ni kubwa mno. Hivyo walipounda ngoma hii ikawabidi waicheze kama inavyotoa midundo yake. Juzi juzi tumeshuhudia tetemeko la ardhi lililotokea baharini huko Japani na kusababisha vinu vya nyuklia kulipuka, ikawabidi wajapani kuicheza ngoma kama walivyoisikia midundo yake. Hii ni hali halisi inayodhihirisha namna dunia tutakayoiunda ndio tutakayoifuata kama inavyotutaka twende.
Katika mfumo wa maisha, binadamu alijikuta anaunda fedha kama njia ya kubadilisha bidhaa ama kitu chenye thamani. Ila katika njia hizo binadamu hujikuta katika wakati mgumu katika kuzitafuta fedha hizo. Ila kwa kua binadamu huyo huyo ndiye aliyeunda ngoma inayotoa mdundo wa fedha, inambidi acheze kwa mdundo wa fedha, yakupasa kuamka kila siku asubuhi, ukizifikiria pesa, yakupasa kulala usiku ikizifikiria pesa, fedha imekua ngoma isiyosha masikioni mwa binadamu, yampasa kuicheza kila mdundo wake inaposikika kwa kua ndio dunia aliyoitengeneza mwenyewe. Ukicheza tofauti na mdundo utajikuta uko nje ya mfumo na huo ndo mwanzo wa kuunda mfumo mwingine ambao nao utabidi uucheze kama unavyodunda ili kuufuata mdundo.
Katika siasa nako kumekua na midundo mbalimbali mfano wa demokrasia ni mdundo ambao unachezwa na jamii nyingi duniani kwakua eti ndio unoleta usawa katika nyanja ya siasa. Kuna modundo ya kubepari, kijamaa, kifalme, kitwana, kitumwa na mingine mingi. Kwa mdundo mtakaouchagua ndio mdundo matakoufata. Kwa mfano walio katika mfumo wa kifalme yawabidi kuzicheza ngoma za kifalme, kwa walio katika mfumo wa kawaida kwa kumchagua kiongozi wao wenyewe, nao watacheza ngoma yao wenyewe, kama watamchagua kiongozi mbaya itawabidi kufuta midundo yake, wakipata kiongozi mzuri basi na midundo yake itakua mizuri na watamchagua tena. Kwa hiyo yatupasa kua makini wakati wakufanya maamuzi makubwa kama haya wakati wa kuwachagua viongozi wetu kwakua tunaiunda ngoma tutakayicheza kama inavyotaka.
Katika mfumo muhimu kuliko yote ni elimu. Mfumo huu ukekua mzuri sana kutokana na namna unavyorembwa na maneno matamu kama “ELiMU Ni UFUNGUO WA MAiSHA/MAFANiKiO”, “ELiMUNi MWANGA”, “ELiMU Ni BAHARi”, waliyoyaweka maneno haya wanajua utamu wa elimu upo wapi, pia wanatambua kua kuna misukosuko inayomtokea yule mtafutaji elimu, na ndio maana wakaweka maneno matamu kama haya ili watafutaji wa elimu wasikate tama mapema, kwani ukiipata elimu vizuri basi utamu wa elimu hiyo utakuchezesha ngoma uliyitengeneza mwenyewe, kama uliunda ngoma yako vibaya basi na mdundo wake utakua mbaya kama ulivyouunda. Ila ikumbukwe kwamba unapotegemea matokeo mazuri uje uko kwenye hali mbaya, unapochumia juani basi utalia kivulini, machungu na matamu ya elimu anayajua yule mtafutaji asiyekata tamaa ya kutafuta elimu. Utamu wake haupo tu katika kupata mafanikio, bali kua na uwezo wa kuelewa mambo kwa urahisi na kutambua ukweli wa dunia na midundo yake. Ukiwa na elimu Nzuri unaweza kutengeneza mfumo mzuri wa maisha ambao utaweza kucheza kwa kufuata midundo yake bila wasiwasi wa vikwazo vyovyote.
Kwa ujumla mambo tunayoyafanya kila siku yanaunda kesho yetu, utakachokifanya leo kesho kitaleta matokeo yake, sasa yategemea matokeo yake utayakubali ama utayakimbia, utakapoyafata utakua umecheza kufuatana na mdumdo wake, pia kama ukikimbia matokeo yake utakua unaunda ngoma nyingine ambayo nayo itakubidi uifuate midundo yake ya kukimbia. Jambo la muhimu ni kuwa makini wakati wa kuangalia aina ya ngoma unayoitengeneza, midundo mingine ni migumu katika kuifata, yatupasa kuicheza huku mioyo ikilalamika. Kwa mfumo wa maisha ya sasa wengi wanalalamika ila ndio ngoma mlioitengeneza kwa ubora mlioahidiwa, kwa kipindi kinachuguja tuwe makini wakati wa kuchagua ngoma ya kucheza kwakua Ngoma tunayoitengeneza wenyewe tutaicheza kama inavyotaka kwa midundo yake, na ngoma hii ni Dunia tunayoitengeneze kila siku. Tambua kwamba KumKichwa ni WeWe.
Kajiabeid©2011