Ni halali na kawaida kwa mtu asiyejua kitu fulani kwake kukikosea, hivyo ndivyo ilivyo kwa mtu huyo kushindwa kukieleza kitu hicho kwakuwa ni kigeni kwake kwenye fikra zake, na siku zote unapojitambua kwamba haujui kitu fulani basi unakuwa haujiamini, na mwisho inapelekea wewe kuwa muoga na kuanguka kwakua hauwezi. Kama ni halali kwa mtu asiyejua kukosea, pia kwa mtu asiyejua lugha ngeni ni halalikwake kuikosea kwakua anafikiria kwa lugha yake kisha anaibadili kwa kuitamka kwa kutumia lugha ngeni..yes i wanted to write this article because of this reason..ndio nilitaka kuandika makala hii kwa sababu hii .."something went wrong somewhere" kuna kitu kilikwenda ndivyo isivyo mahali fulani". Kwa kutazama tu hali ilivyo na muonekano wake, kama wewe ni banadamu unayefuatalia nini kinachoendelea basi utakubaliana nami kwamba, kuna jambo lilikwenda ndivo isivyo na kama halikwenda ndivyo isivyo basi, lilipangwa ndivyo isivo na kama halikupangwa ndivyo isivyo basi limeleta matokeo ndivyo isivyo.
Ni wengi wetu bado tuko kwenye mchakato wakutafuta chochote kitu ili tuendane na mdundo wa ngoma tuliyoitengeneza, lakini kwa mfumo tulionao wa this, that, what and where ndio unaofanya wengi wetu washindwe kufika wanapotaka kwenda kwa mfumo ngeni wa fikra kwa lugha ngeni. Kunausemi unaosema "fikra sahihi kwa lugha sahihi zinaunda maana sahihi", hii ni kudhirisha ya kwamba kwakutumia lugha sahihi katika kufikiria na kisha ukatumia lugha sahihi katika kujielezea basi utaeleweka ulichokifikiria baada ya kukisema bila kupoteza maana.
Narudia tena kuna jambo lilifanyika kimakosa, na kama halikufanyika kimakosa basi lilikua sahihi ila limetoa matokeo yenye makosa. Tazama mwanafunzi wa kitanzania amekua kwenye mazingira ya fikra Lugha ya kiswahili ndio Lugha ya Taifa, ila anapokwenda kutafuta Elimu anakutana na Lugha ngeni ndio Lugha ya mawasiliano. Je? atakapokosea katika kujieleza atakua amefanya makosa? lengo sio kutaka kumjua aliyefanya kosa, lengo ni namna gani tutarekebisha kosa lisoloonekana kwani ninayechekwa nikikosea ni mimi wakati mimi sijui kwamba kosa ni langu ama sio langu."Fikra sahihi zinaundwa kwa lugha sahii" sasa nimeunda fikra sahihi ila kwa lugha niliyotumia kujielezea nikawa siko sahihi “Sum sing went rong sum were"
Ukitazama tulipotoka, tulipokuwapo, tulipo na tunapoelekea tupo sawa?, kama hatuko sawa nadhani utakubaliana nami kwamba kuna jambo wakati fulani lilienda ndivyo isivyo. Na kwa hali hii tumejikuta ndani ya matatizo, ingawa matatizo nayo ni sehemu ya walimwengu, ila walimwengu ni walimu na pia ni matatizo, kila penye uzuri mwingi tutegemee pia kupata ubaya mwingi, lakini huu wakwetu umezidi. Kwakua hawatujali nasisi pia hatujali, kwakua hatujali na sisi pia hatujijali, na kwakua hatujijali na wao pia hawatujali. Juzi, Jana, Leo na Kesho imekua kila siku, hakuna tofauti kwakua hatujijali . Hivi tunategemea nini ?,muda unaenda na nguvu zinamalizwa na umri. Kwakua babu alilala, baba nae akalala, sasa watoto wa baba nao wamelala, je wajukuu wataamka wakati watoto wa baba, baba na babu wao wamelala?. Tusitegemee miujiza tusipotatua matatazo yetu wenyewe. Tatizo lipo ndani yetu, tatizo ni sisi na tunajiogopa kujitatua. Tunasubiria yule aanze kutatua tatizo, na yule anasubiria wewe uanze kutatua tatizo, mimi na yule pia ni tatizo. Kwanini isiwe mimi na mimi ili tuondoe ubinafsi kisha tulitatue tatizo, nimechoka kuchekwa mimi, hali hii inanipa ari yakutaka kufanya mapinduzi ya kuondoa ubinasi wa mimi na yeye. Mapinduzi ya ubinafsi ndio yanatakiwa yawe ya kwanza, kisha tupindue uoga ndani ya nafsi, tukishapata ushindi mimi na mimi tulete umoja wa kupigania kilicho haki yetu.
Nakuambia jambo nadhani utaelewa nilichokimaanisha, “wewe uko na shida yako, kisha nikausaidia shida yako, ukapata shida nyingine, nikakusaidia shida yako, lakini nilipokuuliza tatizo linalosababisha shida zako, wewe hukuniambia tatizo ukaniambia shida yako, badala yakutatua tatizo, ukatatua shida, hivyo tatizo linalosababisha shida zako lipo pale pale na litaendelea kuleta shida kwako”.
Nadhani utakua umelielewa tatizo letu, sasa ili tuachane na shida yatupasa tatue tatizo. Inachukua miaka kujenga ila sekunde kubomoa na tusipotatua tatizo tutazunguka na kurudi tupotoka. Kiukweli hakuna anayetaka kutatua tatizo linalorudisha nyuma maendeleo ya jamii yetu. Ni dhahiri ya kwamba lugha ya kiingereza ina tija katika kurahisisha mawasiliano, lakini mbona tatizo linakua kubwa sana. Embu tazama vipengele hivi kwa umakini na kisha uvichambue kwa fikra zako, kumkichwa haitoi suluhisho ila inakupa nafasi ya kufikiri.
Lengo la Kiswahili kufanywa lugha ya taifa ni kwa ajili ya kutuunganisha na kuondoa ukabila wa kila mtu kutumia lugha yake ya kikabila kama lugha ya mawasiliano, tusingeweza kuelewana kama kila mtu angetumia lugha ya kabila lake, hivyo nawapongeza kwani hawakukosea kukifanya Kiswahili lugha ya taifa.
Kufanywa lugha ya kiingereza kuwa lugha ya pili ni kama kufuata matakwa ya mkoloni wa mwisho aliyetutawala, sidhani kama mitaala yetu ingekua kwa lugha kiswahili mpaka katika ngazi ya chuo kikuu, nchi yetu ingekua kichwa cha mwendawazimu, kwakua watu wangejifunza kwa lugha sahihi na pia tungekua huru kufikiria kwa fikra sahihi, kama tungekiheshimu kiswahilli nadhani ingekua ni moja kati ya lugha ambazo zingekua ni nguzo imara ya maendeleo ya nchi yetu. Hatuna lugha moja kivipi tutaweza kuwa na maendeleo, tumeikimbilia lugha ya watu sasa hata mitaala imekua ni ya watu. Tazama sasa tumeshindwa kujiendesha sasa tunaendeshwa tu na mkoloni wetu. Nadhani ni kikwazo kikubwa katika kulisongesha gurudumu letu, nasema hivyo kwa kua ni asilimia kubwa sana ya watanzania walioshindwa kujieleza kwa lugha ya kigeni ingawa vichwani mwao wako na jambo la muhimu sana wanalotaka kulieleza, na pia watanzania wana akili yakutosha ya kuweza kuendelea mbele, ila tatizo la lugha ndio linawarudisha nyuma. Sasa kama lugha ya kigeni inatusaidia mbona tunashindwa kutafsiri mikataba tunayoingia na hao wageni, tunaishia kuibiwa tu kila siku.Kwa Tanzania ya sasa janga la nne kubwa tulionalo ni Lugha, hatujui matumizi ya lugha yakiswahili na pia hatujui matumizi ya lugha ya kiingereza, tumekua majununi funun wa kiswanglish.
Kutumika kwa lugha ya kiingereza katika shule ya msingi/awali kama somo, kisha kama lugha ya kufundishia katika ngazi ya sekondari sidhani kama hapo kuna malengo ya kumuendeleza mwanafuzi wa kitanzania aliyekulia katika mazingira ya Kiswahili. Wote tunatambua kwamba katika ujenzi imara msingi ndio unatakiwa uwe imara, lakini sisi tunaimarisha juu wakati chini hapako imara. Kama vipi wafanye lugha ya kiingereza ifundishwe kuanzia elimu ya msingi ili fikra za wanafunzi hawa zijengeke kwa fikra sahihi na kwa lugha sahihi, tunawapa sana shida vijana wetu kwa kuwafanya wafikirie kwa lugha hii na kisha wajieleze kwa lugha nyingine, kivipi tutafikia malengo kwa malengo potofu kama haya.
Maono yangu ni kwamba kuna jambo linapelekwa ndivyo isivyo, na kama halipelekwi ndivyo isivyo basi linakwenda ndivyo isivyo, na kama haliendi ndivyo isivyo basi limetoa na litaendelea kutoa matokeo ndivyo isivyo, ninaposema ndivyo isivyo namaanisha haliendi kwa namna tuliyotarajia litakwenda hivyo na pia, halitendeki kwa namna tuliyotarajia litatendeka hivyo pia halileti matokeo tuliyoyatarajia. Sina maana ya kuwakosoa walioamua iwe hivyo ila nawonesha namna tunavyoathiriwa na mfumo huo mliouweka wa this, that, where and what kwa kizazi chetu cha fikra Swahili lugha Inglishi. Na kwakua hatujui vizuri lugha ya Kiswahili sahili hata tunapotafsiri lugha ya kiswalili kwa lugha ya kiingereza tunajikuta ni wenye wa makosa.
Ningependekeza tuchague moja kama ni Kiswahili basi kianzie chini mpaka juu, mbona China, Urusi, Hispania, Italia na nchi nyinginezo duniani zinatumia lugha zao kama lugha ya kufundishia na nchi hizo ziko imara na wako na maendeleo kwakua wanatumia fikra sahihi kwa lugha sahihi. Au tufuate mfumo wa Kenya lugha ya kiingereza kuanzia elimu ya awali, ili tupate wataalamu wenye fikra sahihi watakaoleta maendeleo katika nchi yetu yenye Amani na Upendo kwa wananchi wake. Tuonyeshe upendo kwa fikra sahihi, tuonyeshe upendo kwa lugha sahihi, sio mnatuambia kwa kiingereza nchi yetu ni ya“Piece and theft”, halafu mnatutafsiria kwa kiswahili kuwa ni nchi ya “Amani na Usalama” tunashindwa kuelewa mnamaanisha lipi...kumbuka ya kwamba KUMKiCHWA Ni WeWe!