Mwanzoni mwa miaka ya nyuma hali ilikua tete katika kijiji chetu na kupelekea babu kufanya mabadiliko makubwa katika mfumo wakuendesha kaya na koo zote, babu yetu ndiye aliyekua mkuu wa kaya zote, yeye ndiye aliyepewa mamlaka ya kuongoza kaya zote katika kijiji chetu kwakua alikua na ujuzi na alipata miwani iliyomuezesha yeye kuona na kuweza kuongoza kaya zote. Wakati babu anakabidhiwa uongozi wa kijiji chetu kulifanyika tambiko kubwa katika moja ya kaya za vijiji vyetu, kaya ambayo babu alipendekeza iwe makao makuu ya kijiji chetu, na kaya nyingine alitaka iwe ya kufanyia biashara. Chakushangaza mpaka leo kaya hiyo bado haijafanywa makao makuu ya kijiji wakati shughuli nyingi za kijiji zikipelekwa kwenye kaya ya kibiashara, hii inaonesha ni kwa namna gani ushauri uliotolewa na babu kwa kutumia miwani yake unavyopuuziwa.
Tokea babu alipofariki kijiji chetu kimekua kikiyumba sana, kwa kua tokea mwanzo hata wakati wa uwepo wa babu tulikua hatuna msingi imara wakuweza kukiendesha kijiji chetu pasipo kutegemea wageni kutoka vijiji vya nje. Hii ilitokana na shinikizo alilolipata babu la kuondolewa madarakani, ambayo ilimlazimu babu kuachia uongozi wakijiji baada ya kuona shinikizo linazidi juu ya mfumo aliouchagua kua ndio utakaofaa kuendesha kijiji chetu. Wakati babu anafariki aliniachia miwani yake, aliniambia mjukuu wangu miwani hii kama utaitumia vizuri basi itakusaidia kuona pale wanapoficha, utawanona pale watakapodanganya, na utawaona wale wasiotaka kufuata misingi tulioinanzisha, na utawaona wasaliti watakaokisaliti kijiji chetu, ila kwakua mjukuu wangu miwani hii ni ufunguo wa maisha yenu, yako na kizazi cha baadae, nakusihi miwani hii iwe msingi wa kukukomboa wewe na kizazi chako, kisha na nyinyi kwa pamoja muwakomboe na wenzenu dhidi ya ubaghili na ubinafsi wa nafsi utakaoingia katika kijiji chetu, kwani kuondoka kwangu najua mengi yatabadilika na nimeshawaona wengi mafisi wakikitamani hiki kijiji chetu ila miwani hii ndio ukombozi wenu, naomba muitumie kwa malengo ya kuleta mabadiliko chanya katika jamii ya kijiji chetu.
Sasa ni miaka mingi imepita tokea kuondoka kwa babu yetu na jemedari aliyelisongesha gurudumu la maendeleo katika kijiji chetu na kuondoka kwake ni kweli mengi yamebadilika, ila kwa kutumia miwani ya babu nimeona mambo mengi yanavyopelekwa ndivyo sivyo, kama babu alivyonisisitizia ya kwamba "kuondoka kwangu mjukuu wangu kwa kutumia miwani yangu utaona mengi yatakavyopelekwa ndivyo sivyo"
Tazama yanayofanywa na wasomi wa kijiji chetu, wameshasahau ya kwamba mategemeo ya wanajamii kwa wasomi ni mabadiliko kutokana na kisomo walichokipata, na sio uharibifu kwa kisomo walichopata. Nakumbuka babu alisema “msomi asisahau jembe, jembe ndilo limempa uwezo wa kuishika kalamu”, lakini kwa miwani ya babu leo namuona msomi analitupa jembe lililompa akili namna ya kushika kalamu. Wasomi wamekua ni watu wasiotaka kuleta maendeleo chanya bali wametuleta uhasi na uhasama ndani ya kujiji chetu. Wamekua ni watu wenye tamaa na wasio na nia nzuri na kijiji chetu. Imefikia mpaka wanakijiji wamepoteza imani na wasomi wa kijiji chetu kutokana na tamaa zao za madaraka, maisha mazuri, kujilimbikizia mali huku wakiwaacha wanakijiji wetu katika kipindi kigumu sana kwani hali ya maisha ya sasa ni tofauti na kupindi alichokuwapo babu.
Miwani ya babu imeona kuwa amani tuliyonayo katika kijiji chetu sio amani kama mioyoni mwetu tuna malalamiko juu ya mfumo wa maisha ya sasa yalivyo na hatuna pakuyapeleka, kwani kwa kutumia miwani ya babu nimeona ya kwamba “amani ni maandalizi ya vita vingine”, na wakati wa vita hivyo tutajaribu kutafuta amani ya kweli ila nayo tutaitumia kuanzisha tena vita nyingine, amani tutakayoipata ni kupumzika kwa amani kwa matumaini ya kupata amani. Babu alisisitiza kuwa kama tunataka tuwe na kijiji cha amani basi yatupasa kuacha chokochoko za kutaka kuvunja muunganiko wa kijiji chetu, tusizungumzie sana kuvunjika kwetu kwamba ndio kutakua chanzo cha maendeleo. Miwani ya babu hapa inaona ubinafsi katika pande moja kwamba kuunganika kwa kijiji chetu na chao ndio chanzo cha maendeleo yao kurudi nyuma. Ila kama wangelijua umuhimu wa muunganiko wa kijiji chetu na chao basi wasingechokoa kuitafuta vita wakati tuko katika kuitafuta amani ya kunyanyasika kisaokolojia na kifikra. Na hii miwani ya babu haitaacha kamwe kuona na kuongea kwakua hatuna imani na amani tuliyopewa na viongozi wa kijiji chetu.
Nakumbuka babu alituambia tusiuguse mbuyu ule mpaka tutakapopata wataalamu wa kuvuna mabuyu ya mti ule, sasa hali imebadikika tokea kuondoka kwa babu, wageni wengi toka vijiji vya nje wanamaliza mabuyu na kutuachia mibuyu mitupu. Miwani ya babu imeona usaliti wa viongozi wa kijiji chetu ambao babu aliniambaia kwa kutumia miwani hii utawona wasaliti. Kijiji chetu kimejaa wasaliti kwakua hakuna aliye na uzalendo, uamninifu, anayewajibika, anayesimamia haki. Kupotea kwa misingi hii kunasababisha viongozi wa kijiji chetu wenye tamaa kulipeleka ndivyo sivyo gurudumu la maendeleo ya kujiji chetu. Mibuyu yote wamewaachiwa wageni eti wao ndio wanautaalamu wakuyavuna mabuyu hayo, ila sisi tutapata faida kwa kuwakatoza ushuru na kwa kupata gawiwo kwa mavuno hayo. Kwa kweli mimi nimeshindwa kuwaelewa viongozi wa kijiji chetu. Yaani wanawaachia wageni wamumunye utamu wote wa mabuyu, kisha sisi watuachie matetere ya ubuyu, hivi tunakipeleka wapi kijiji hiki?.
Babu alituhimiza kua kijiji chetu kisiwe na utengano wa koo, tusijitambue kwa koo wala tusiendekeze ubinafsi wa koo. Ila kwakutumia miwani ya babu naona ubinafsi wa koo umeingia katika kijiji chetu. Hii inajitokeza kwa baaadhi ya koo fulani kuweka ubinafsi kwa tamaa ya kujiletea maendeleo wao kwa wao, na ilidhihirika wakati wa kumchagua viongozi wapya wa kijiji chetu, kwani ukoo wa babu ndio unaoongoza kijiji chetu tokea kuwepo kwa babu hadi sasa. Imefikia kipindi maendeleo yanagawanywa kwa kuangalia ukoo, hali hii inaleta uhasama ndani ya kijiji chetu kwani ndio moja ya amani amabayo sio amani bali maandalizi ya vita vingine. Ingawa babu alisema “vita vikali vitatokea ndani ya ukoo wangu na vitazidi vita kati ya ukoo wangu na ukoo mwingine” kwa tamaa ya madaraka iliyowatawala viongozi wa kijiji chetu na hali ya malalamiko ya wanakijiji ilivyo sasa, panaweza pakazuka vita kali sana. Na kwakua kijiji chetu hakijawahi kuingia katika vita kati ya ukoo na ukoo, hali itakua mbaya sana kwani hatujui ni kwa namna gani tutaweza kuimaliza vita hiyo na kufikia muafaka. Miwani ya babu pia imeoma ubinafsi wa viongozi wa kijiji chetu kutaka kuwatumia vijana na wanakijji kama ngao yao wakati wa wamapigano yao. Wamekua ni watu wa kuwajaza vijana uongo ili vijana waone kwamba wanapigania haki kumbe hakuna chochote wanachopigania bali matakwa na tamaa za madaraka ya viongozi.
Ndio maana Babu alitushauri kwamba tusome kwa bidii ili tuwe na ufahamu wa mambo, kwamba tuwe na malengo na tunavyovitafuta. Alituambia malengo ya elimu tunayopata ni kutuwezesha kukabiliana na mazingira yetu yanayotuzunguka. Alisema kipimo kizuri cha akili tuliyonayo ni namna utakavyoikabiliana na hali itakavyotujia au mazingira yatakavyokujia katika kipindi ambacho haujajiandaa au haukuifahamu. Na kwa kutumia miwani hii ya babu, maneno haya aliyoyanena mwishoni ndio miwani ya babu aliyonipa kuweza kuchambua hali ilivyokua, ilivyo na itakavyokua. Hivyo nakushauri kijana mwenzangu, tumia miwani hii ya babu kutambua ni miwani gani ya babu aliyotuachia. Ukishaitambua miwani hiyo basi ukae chini na kuangalia wapi ulipotoka, wapi ulipo na ni wapi unapoelekea. Usikubali kupelekwa pelekwa tu na mfumo nyonyevu kama bendera mbele ya upepo. Kama kijana wa kileo unatakiwa ujue nini kinaendelea katika dunia yetu na wapi kijiji chetu kilipo, na kwa namna gani unaweza kushiriki kama kijana kusongesha mbele gurudumu la mendeleo. Tambua kijana kwamba hakuna kisicho na umuhimu kilicho hai {chenye kuishi}, hivyo uwepo wako unamaana kubwa sana kama utatambua kwamba uwepo wako una maana kubwa. Ndio maana sintochoka kukuambia na kukukumbusha ya kwamba umoja wetu ndio nguvu yetu, tukijiunga mimi na mimi tunapata sisi. Kumbuka kumkichwa ni wewe!
No comments:
Post a Comment