Wednesday, September 28, 2011

"Ni Uoga ama ni Ujasiri"




Katika makala iliyopita ya "MAPiNDUZi YA KWANZA Ni YA KUUSHiNDA UOGA NA UBiNAFSi" niligusia uoga na ubinafsi uliotawala nafsi za watu na kupelekea kwetu kushindwa kuleta mabadiliko chanya katika jamii zetu. Ila kwa mada ya leo ningependa tuelewe uoga ulio ndani yetu ni upi. Je ni uoga wa kuogopa ama ni ujasiri wa kutokuogopa.
Siku zinakwenda kila siku na miaka inapita kila mwaka, leo hakuna tofauti na ilivyokua jana na jana haina tofauti na juzi. Tumekuwa watu wa bora jana leo ni kali zaidi, kesho ikifika bora jana. Umekua wimbo wa watu walio katika hali ya chini ambao malalamiko kwao hayaishi kila siku. Wamekua watu wa “tungejua ukweli kabla, tusingempa vema”, Tabaka hili sijui niliite la watu wavumilivu kwa ujasiri ama wavumilivu kwa uoga, ama waoga kwa ujasiri ama wavumilivu wa uoga. Ni vituko vinavyofanyika katika maisha yetu ya kila siku.
Kwa upeo wako najua utakua umeyasikia maigizo haya kwenye baadhi ya vyombo vya habari. Yule kashutumiwa kaiba kiasi fulani, huyu katumia ofisi vibaya, mwingine kaingia mkataba wa uongo, mwingine kachangisha fedha za kuwapoozea wenzake. Maigizo yasiyo na mwisho kwakuwa waigizaji hawa wanapokezana nafasi ya muigizaji mkuu. Ndio maana nashindwa kuelewa hawa nao niwaweke katika tabaka lipi. Je hawa ni majasiri katika kufanya mambo yao ya kurudisha nyuma gurudumu letu ama nao ni waoga ndio maana wamekosea mpaka wakajulikana.
Kama kweli sisi ni majasiri basi tuwe majasiri wa vitendo na sio majasiri wa kuongea lakini waoga wa vitendo. Tatizo letu sisi tunaongea sana kuliko kutenda, na ujasiri wetu wa kuongea tungali ugeuza ukawa wakutenda na uoga wa kuongea tungekua tumepiga hatua kwa kuwawajibisha wanaotusaliti.
Nisingependa kuongea sana kwakua mimi mwenyewe ni mtanzania, ila kwakua nasherehekea miaka 50 ya Uhuru kwa huzuni kwani tunakuongea sana lakini matendo hakuna, huzuni ya kutokuwawajibisha wakwapuzi wa mali zetu. Ningependa kuwauliza wananchi wenzangu kwamba Ujasiri tulionao ni upi? wakuvumilia maovu?, ni ujasiri kwa kua tuna matumaini mwokozi atarudi?, ujasiri wa kuogopa kuwawajibisha waovu?, ama ni uoga wa kufanya maamuzi.
Maana mimi ninavyoelewa kwenye kisanduku cha kuweka vema uko peke yako, nikimaanisha uko wewe, akili yako, ufahamu wako wa sera za ukweli na uongo. Hivi sisi ni majasiri wa uongo ama wa ukweli, au ni kwamba hatujielewi,  haiwezekani vema uweke wewe, kisha lawama umpe yeye na yule. Embu jaribu kuwa jasiri wakati wakuweka vema, chagua kilicho bora kwa ujasiri, kwani uoga wako kwa binadamu mwenzako ni kumtukuza asiyestahili kutukuzwa. Hofu na uoga unatakiwa ni kwa aliye juu mbinguni na sio kwa aliye juu madarakani hapa duniani. Wazazi wanawarithisha watoto uoga, watoto nao wanawafundisha wenzao uoga.
Mimi nadhani tunahitajika tubadilike sisi kwanza ndipo na sisi tunaweza kufanya mabadiliko ya kimaendeleo. Mabadiliko yoyote huanza na sisi wenyewe, tujibadilishe kwanza sisi wenyewe ndipo tutaweza kushirikiana katika kuleta maendeleo ya jamii yetu. Namaanisha uitakase nafsi yako kwanza ndipo utapata ujasiri wa kuitakasa nafsi ya mwenzako. Kama wewe ni mkosefu huwezi kupata ujasiri wa kuwakosoa wenzako, lazima utawatetea wakikosea. Utasikia tu "kila binadamu anakosea, tusimlaumu sana Mzee wetu, mwacheni apumzike, amefanya mengi sana". Nauliza mengi yapi? Je ni mazuri ama mabaya"?. Tusikae kulalama ama kusubiri mkombozi wetu arudi au aje. Wakombozi ndio sisi wenyewe na ukombozi wa makombozi ni kujikomboa wewe mwenyewe. Kumbuka kumkichwa ni wewe!

No comments:

Post a Comment