Sio vibaya kwa mwandishi kuanza kwa kuwauliza wasomaji wake swali na sio vibaya pia mwisho wa makala zake mwandishi huyo kuwapa jibu. Hi ni kawaida kwani panapo swali huwa pana jibu lake. Je wewe unaonaje?. Katika mfululizo wa mashairi, makala na picha nilizozitoa ziko kwenye mfumo wa kuuliza kisha kuchambua kwa vipengele mbalimbali husika na kichwa cha habari ama lengo husika la kilichohusika, iwe ni makala, ushairi ama picha. Ukizitazama kwa makini basi utakua umeona uhusika wa ninayoyasema. Ila swali limenijia je wewe huwa unazionaje? Je unaona zaidi ya niliyoyaona ama nilivyochambua? Je kwa upande wako unaona sivyo ama ndivyo? Je? Je? Je?. Yote haya ni maswali ambayo wewe kama msomaji unatakiwa uyatambue kwa uhalisia wako kisha ujiulize na kupata majibu ambayo yanatokana na uhusika wako katika dunia hii.
Tumeumbwa katika upekee ambao unamfanya kila kiumbe kiwe na muono wake tofauti na wengine. Ila pale panapokua na uhusika halisi na asilia wa kitu basi wote tupate jibu moja, iwe ni ndio au hapana, ama iwe ukweli au uongo. Inategemea na wewe umeonaje.
Ninaposema umeonaje namaanisha, baada ya kukiona kitu ama jambo kisha ukalichambua kwa makini kutokana na namna ulivyokua/ulivyokuzwa kwenye mazingira yako, watu uliokutana nao katika ukuaji wako, vitu/mambo uliyojifunza, tabia zako, malengo yako, umuhimu wake katika maisha yako, unakipenda/haukipendi, unakitambua/haukitambui, hasira, chuki, wivu, uwezo wako ama mapungufu yako. Vyote hivi vinahusika katika kuona na kujua kua unakionaje ama unakichukulia vipi.
Kuna upekee katika vitu, kuna mafunzo, kuna kuweza na kushindwa. Ukiamua kuona utaona, ila je unakionaje? Zaidi ya unavyokiona ama haina haja ya kuona zaidi. Ulichokiona kwa mtu ama kitu ni zaidi ya ulichokiona. Mfano hii ni kalamu. Je kwa matumizi yake unaweza ukaona kua utakitumia kwenye nini?. Kalamu sio kuandika tu, kalamu inaweza ikawa silaha tena hatari sana, ila inategemea umeionaje na umeamua kuitumiaje? Jiulize matumizi zaidi ya kalamu.
Tazama kisu matumizi yake ni kukatia vitu. Lakini kisu kinamatumizi mengi. Mazuri na mabaya. Yenye manufaa na kwa yasiyo na manufaaa. Wewe umekionaje? Je unaweza kukitumia zaidi ya matumizi yake husika. Mfano unataka kufunga screw ila hauna screw driver, kama una kisu unaweza kutumia. Ila matumizi ya kisu sio kufungia screw. Inategemea na mafunzo na mahitaji yako. Je wewe unakionaje? Lengo la makala hii ni matumizi yetu kwenye vitu ama watu katika maisha yetu. Je tunavitumiaje, je tunavichukuliaje? Je tuna vionaje? Namna tunavyoviona na namna tunavyovikuchulia ndio vinapounda matumizi yake na matokeo yake yanatokana na maswali hayo.
Katika dunia ya sasa ya Zama za Habari “Information Age/Information Revolution /Computer Age/Digital Age” ambapo zimefanya mabadiliko makubwa na kuifanya Zama ya Viwanda kupotea kabisa kwenye ramani. Zama hii mpya ya habari inahusisha sana matumizi ya mtandao katika kurahisisha njia za awali zilizotumika katika zama za viwanda. Utakubaliana nami kwamba zama za sasa zimefanya mawasiliano kuwa marahisi sana kuliko kipindi cha nyuma. Ukitaka kufanya biashara, kusoma, kutoa habari ama kupata habari yoyote sasa hivi basi wewe tumia mtandao na utazipata kwa haraka sana. Hii ni kutokana na mfumo mpya wa digital. Ila sasa isiwe tija sisi kuwa katika mfumo huu mpya. Swali langu liko pale pale wewe unaonaje nikimaaniasha wewe unautumiaje huu mfumo mpya wa maisha katika kurahisisha shughuli zako za kila siku na katika kijiletea maendeleo yako, familia yako, jamii yako, taifa lako na duniani kwa ujumla.
Hembu tazama mifano ya watu hawa na kwa kutumia mtandao wa jamii wa FACEBOOK.
MSANII: - Kama kuna msanii yuko kwenye mtandao wa facebook, msanii huyu ataona facebook kama sehemu ya kutangazia jina lake, kutolea nyimbo zake, kuwajulisha mashabiki wake nini kinaendelea juu yake, pia kujua idadi ya mashabiki wake. Anaweza pia kuitumia kama sehemu ya kuwavuta mapromota ili waweze kumpa dili la kufanya kazi nae. Pia kwakua msanii huyu ni kioo cha jamii basi sehemu hii msanii anatakiwa aiheshimu kwani matumizi ya kioo ni kutazama, sasa kama huyu msanii atachafua kioo hiki basi asilaumu mashabiki wake watakapo mkimbia.
MFANYABIASHARA: kama kuna wafanyabiashara katika mtandao wa facebook basi hawa watakua wanaiona kama sehemu muhimu ya kuwafikia wateja wao kwa kutangaza biashara zao na pia kupata maoni namna ya kuboresha huduma na bidhaa zao. Pia ukiwa na idadi kubwa ya watu waliojuinga katika ukurasa wako kama wateja pia inamfanya mfanyabiashara huyu kujua bidhaa yetu imesambaa mpaka wapi na wapi tunatakiwa tuifikishe. Hii inategemea na mfanyabiashara huyu ameuonaje mtandao huu.
MWANASIASA: - kwa wanaojihusisha na siasa wanaweza kuhamisha jukwaa lao kuwa kurasa kwa kueleza sera zao kupitia mtandao. Hii inatokana na kuwa mtandao huu unakua kwa kwasi kuliko soko lingine kwa dunia ya sasa. Anaweza kupata pia habari za nini kifanyike kwa wanachama wake, pia aweza kuona mtandao huu kama sehemu ya kujua idadi ya wanachama wake.
Ila kuna hili kundi la vijana wa kike na kiume, kundi hili limekua na tabia nyingi tofauti kutegemea na matumizi ya mitandao hii ya jamii. Kundi hili mara nyingi liko katika mafunzo ili waweze kupata upeo wa kuweza kukabiliana na maisha yao wakati wao utakapofika. Lakini kundi hili nadhani wanashindwa kutofautisha matumizi ya kisu na kalamu. Wanatumia kisu kuandikia na kalamu kukatia. Kundi hili litakuja kuamka wakati jua linazama au litakumbuka shuka wakati jua ndio linachomoza. Nimejaribu sana kutafuta njia ya kuliongoza kundi hili katika kuona utofauti wa mambo na kuona vitu tofauti na vinavyoonekana ila inavyoonekana kwamba inaweza ikapelekea kamvunja samaki huyu anayejilazimisha kukauka kwa kujaribu kwangu kutaka kumkunja angali mbichi na mbishi.
Hivyo kwa kutumia maandishi haya, najaribu tena kuwapa mwongozo wa namna ya kutazama kitu ama jambo tofauti na linavyooneka ama linavyosemwa. Kwa mfano ninaposema kumkichwa ni wewe, sijui kuwa huwa unanielewaje? Au unaona kuwa kumkichwa ni kumkichwa tu kama ilivyo kumkichwa. La sio hivyo, hembu itazame kumkichwa kwa namna tofauti kwa upeo wako wewe. Kisha ukipata jibu tuilia nalo. Dunia ya sasa imekua ya mapinduzi ya mtandao kwa mtandao. Unajua kua mtandao wa YOUTUBE unaweza ukafanya Tanzania ya leo ikabadilika sana tofauti na unavyoiona. Tazama kwa makini matumizi yako ya simu ya mkononi ni zaidi ya kupiga picha na kusikiliza muziki, hembu zama zaidi unaweza ukapata jibu la swali langu kuwa je wewe unaonaje, kwa matumizi ya vitu na watu unaowaona. Kumkichwa ni wewe!
No comments:
Post a Comment