Wednesday, November 2, 2011

"Usijaribu kubisha! Jaribu kuelewa"

MEDITATION



          Katika tafakuri zetu za kina za kila siku kuna ukweli ambao miongoni mwetu tunatakiwa tuukubali kama ulivyo. Ingawa miongoni mwetu huwa tunapingana nazo kwa kutaka ziende vile nafsi zetu zinavyotaka, na kwa tafakuri hiyo tunajikuta tunapingana na ukweli ulivyo kwakua tuna katabia kanachoitwa ubishi wa kubishia nafsi zetu palipo na ukweli. Sasa hembu tujaribu kutazama palipo na ukweli na kisha tuukubali kwa kuuelewa ukweli huo ili tufanye maisha yetu yawe marahisi, kwani kwa namna tunavyokataa ukweli wa tafakuri za kina ndipo tunapoyafanya maisha yetu ya kila siku kuwa magumu na yenye matatizo tunayo yatengeneza sisi wenyewe na kisha kuyatupa kama lawama kwa wao, yeye ama wewe, kunapopelekea kuunda tatizo lingine. Hembu tafakari kwa kina kuhusu haya niyasemayo kisha ujaribu kuelewa. Kwakua wewe ni binadamu kama mimi najua utabisha kwani binadamu tumeumbwa na hulka zifuatazo.

                Kusahau:- ni hali inayomtokea mwanadamu na kumfanya asiwe na ufamu wa jambo kila wakati, kupoteza picha halisi ya tukio ama jambo fulani, hii inatokana na kuwa binadamu hupitiwa na mawazo mengine ambayo humfanya binadamu asiwe na kumbukumbu ya jambo fulani kila mara. Kiwango cha kusahau huwa kinatofautina baina ya mtu na mtu kutokana na umuhimu wa jambo ama hicho kitu kwa mtu huyo. Kusahau kunaendana na kukumbuka, huwezi kuzungumzia kusahau ukaacha kulitamka neno kukumbuka. Ni vitu viwili vinavyotegemeana sana. Sasa kwanini tunasahau na kwanini hatukumbuki. Tuuchukulie mfano wa KIFO ambao ni kitu kichungu na kinachompa mwanadamu wasiwasi na uoga juu ya maisha yake. Ukimwambia mtu kinyume cha kusahau atakuambia kukumbuka tena kwa furaha, lakini ukimwambia kinyume cha kuwa hai atajibu kifo huku nusu ya furaha yake ikiwa imepungua. Tujaribu kuelewa kuhusu kukumbuka na kusahau pia kuwa hai/kuishi na kufa ama kifo. Huwa tunafiwa na wale tuwapendao lakini pia huwa tunawakumbuka sana kwa kua walikua wana umuhimu katika maisha yetu ya kila siku. Lakini kuwakumbuka kwetu sio kama ilivyokua siku waliotutoka. Kifo hakisahauliki ila huwa kikiwa ni kwako wewe huwa unakisahau. Kwakua tafakuri hii inakusuhu wewe basi utakubaliana nami kua huwa tunajisahau kuwa ipo siku tutaondoka katika dunia hii. Na hii ni hulka ya mwanadamu aliyopewa na muumba wake ili asisononeke sana pale anapo fiwa ama anapokumbuka kuwa kuna siku nitakufa. Hembu tujiulize ni tabu gani tungeipata kama tungekua na hulka ya kujua kua kesho ndo siku yangu ya kufa. Jaribu kuelewa na usikariri. Kusahu kupo na kuna umuhimu wake katika maisha yetu ya kila siku. Ila kumbuka kumuomba muumba wako ili siku hiyo ikifika uvune vinono ulivyovipanda ingawa najua kuwa utasahau..

                 Kutoridhika:- ni hali ya kutokutosheka na ulichonacho ama ulichokipata wakati unatafuta. Binadamu ana hulka ya kutokuridhika na hii inatofautiana baina ya mtu na mtu. Kuna wengine watasema huwa naridhika ila hata upewe kila kitu bado utataka kitu kwakua haturidhiki. Kuna hulka ya kutafuta zaidi ya ulichokipata kwakua ni hulka yetu kutokuridhika. Masikini haridhiki anapopata riziki, tajiri nae haridhiki kwakua nae anataka riziki zaidi ya aliyoipata. Yote hii inatokana na kusahau na kutokuridhika. Katika tafakuri za kina ukilitazama tumbo namna mwenyezi mungu alivyoliumba hata ulipe nini haliridhiki ila huwa tunaridhisha kwa kutoa shukrani kwa tulochokipa. Ila baada ya muda huwa tunalipa tena yoyote riziki ilituweze kutafuta kingine kwakua haturidhiki. Kwakua haturidhiki basi tunatakiwa tutoe shukurani kwa tulichokipata. Ili tutafute kingine chenye Baraka kutoka kwa muumba wetu. Tukumbuke kutoa shukurani kwa tulichopata kwakua kina ubora kuliko tulichokikosa. Hivyo jaribu kuelewa na wala usibishe ingawa najua kuwa pia utasahu kwakua haturidhiki.

                 Kutafuta:- ni hali ya kutaka kupata kile unachotaka na unachodhani kuwa kina umuhimu katika maisha yako ya kila siku. Katika kutafuta kuna kupata na kukosa, na katika kupata kuna kushukuru ama kukufuru, halikadhalika unapokosa unatakiwa ushukuru na sio kukufuru. Binadamu huwa anatafuta kisha anapumzika, kisha anaanza tena kutafuta. Kwakua tuna hulka ya kusahau na kutokuridhika, basi yatupasa kutafuta kwa moyo mmoja na kwa hali na mali. Hali ikisimama kwa maana ya uwezo wako wa nafsi na mali kwa uwezo wa vitu vinavyokuzunguka. Lakini ili kuweza kufanikisha haya katika kutafuta binadamu huwa anajisahau kuwa hata akipata anachokitafuta kuwa hataridhika. Hivyo binadamu huyu anaishia akitafuta anachokijua na asichokijua. Jaribu kuelewa na wala usibishe kwani usiposahau utaridhika na ukiridhika hautatafuta. Muombe muumba wako akuongoze katika kutafuta.

                 Matatizo:- ni hali ya kutokua na utulivu wa nafsi, moyo na akili. Ni sehemu ya maisha yetu kwakua tunajisahu, haturidhiki na hatuchoki kutafuta. Huwa tunafikiria kuwa matatizo ndio yanamkuta mwanadamu, sio kweli kwakua kunachokukuta basi kitakuacha, lakini ukifanya tafakuri ya kina utagundua kuwa banadamu ndio anayoyakuta kisha anayaacha. Tatizo sio matatizo ila tazizo ni binadamu. Binadamu na vitu vilivyopo katika dunia hii ndio matatizo au ndio tatizo. Matatizo hayajitengenezi ila sisi ndio tunayatengeneza matatizo. Hivi unajua kuwa kiumbe kilichokufa ama ambacho bado hakijazaliwa hakina matatizo. Basi elewa kuwa sisi ndio matatizo. Kwaku tunasahau, haturidhiki na tunatafuta kwa hali na mali. Hivyo kutokukamilika kwetu ndio kunakotuletea matatizo na ili kuweza kufanikisha haya yote yakubidi kuelewa na sio kukariri kwani maisha ni marahisi ili sisi ndio wazito katika kuyaelewa.

                Uchungu:- ni hali inayoleta maumivu katika kitu ama mtu, uchungu unaumiza na hasa kitu ama mtu mwenye uhai ndiye anayepata uchungu huu. Kwenye Agano La Kale imendikwa “mwanaume atatafuta kwa uchungu ana mwanamke atazaa kwa uchungu”. Je ni uongo ulioandikwa kwenye vitabu hiki? Sidhani, kama ukibisha au unataka kubisha, fanya tafakuri ya kina na kisha utazame hali halisi ya maisha yetu ilivyo ndipo ubishe kua huu ni uongo. Ni kweli kwamba atakayeamua kutafua atatafuta kwa uchungu na atakayeamua kuzaa atazaa kwa uchungu. “Penye uchungu pana utamu na penye utamu pana uchungu” jaribu kuelewa na usikariri kisha ukabishana na ukweli wa tafakuri za kina. Inaleta uchungu pale mtu anaposahau jambo lenye umuhimu na pia inaleta furaha pale mtu anaposahau jambo lenye uchungu. Tafuta kwa uchungu, ukipata najua pia hautaridhika ila endelea kutafuta tena kwa uchungu.

                 Kufanikisha:- ni hali ya kupata kile ulichokua unakitaka/unakitafuta, kiwe ni kidogo ama ni kukubwa, ukikabiliana nacho ukakishinda basi ujue umefanikisha, ama kinachokutatiza katika kupata amani ya nafsi, moyo na akili kisha ukaweza kuondoa ukinzani huo basi umefaniakisha. Kwa mfano ikihisi njaa unakosa amani ya nafsi na akili, lakini ukishatatua tatizo hilo basi umefanikisha, lakini chakula utakipata wapi ili utatue tatizo hilo, nao pia ni ukinzani, ukitatua nalo umefanikisha. Hivyo matatizo ni ukinzani kwa mwanadamu, mwanadamu hapendi alichonacho anapenda asichonacho, lakini akikipata asichonacho hakitaki tena, binadamu huyu anajisahau, banadamu huyu haridhiki, banadamu huyu anatafuta, binadamu huyu anapata uchungu, binadamu huyu anafanikisha. Lakini hajui kua amefanikisha kwakua anasahau, haridhiki, anatafuta, anauchungu anataka kufanikisha kila kitu. Jaribu kushukuru pale unapofanikisha hata kitu kidogo usijisahau sana eti kwakua hauridhiki na kwakua unatafuta kwa uchungu mpaka ufanikishe.

                     Hivyo nataka ukubaliane nami kua sisi binadamu hatujakamilika, ingawa kulirudia neno banadamu hatujakamilika ni kuonesha ni namna gani sisi binadamu hatujakamilika kwakua tumeshakubali kua hatujakamilika. Tunasahau, haturidhiki, tunatafuta kwa kushindana kuukimbiza upepo ama kukimbizana na upepo, tuna uchungu ambao hatuwezi kuuondoa bali tunaushahau kwakua hatujakamilika, tunafanikisha ingawa sio vyote tunavyovifanikisha kwakua huwa tunasahau kutoa shukurani tunapofanikiwa ama tunaposhindwa kufanikisha. Kwa hiyo tunapofanya tafakuri ya kina (meditation) yatupasa tukubaliane na ukweli, pale tunapopata tafakari ya kina yenye ukweli basi tuikubali kama ilivyo, wala tusijaribu kuipinda ikawa ni uongo, kwani “kuna ukweli ambao hauwezi kuwa uongo na uongo ambao hauwezi kuwa ukweli”. Ukikubaliana nami kuhusu haya basi utakuwa miongoni mwa watu wanoishi maisha marahisi yenye furaha kwakua wanajaribu kuelewa na sio kukariri na kubishana na ukweli wa nafsi zao. Ni rahisi kumbishia binadamu mwenzako na ukamshinda ila ukibishana na nafsi yako utashindwa. Tuzidi kumuomba muumba/mola/mwenyezi mungu atusamehe makosa yetu wakati kabla ya kuanza tafakuri na wakati tunamaliza tafakuri zetu kwani hapo ndipo tunapogundua mabaya na mazuri tuliyoyafanya. Tubu na utasemehewa. Kumkichwa ni wewe!

No comments:

Post a Comment