Saturday, November 5, 2011

Naandika





"Kalamu ni bora kuliko upanga" haya sio maneno yangu bali ni nukuu ya wahenga, ikimaanisha ukichagua kalamu ama elimu wewe ni bora kuliko aliyechagua upanga. Maswali yataibuka kwanini una andika? Sababu moja kubwa ndio iliyonifanya/inanifanya niandike. UPENDO WA DHATI. Sijui kwanini napenda kuandika ila huwa najikuta naandika makala mbalimbali na huwa najikuta ni mwenye furaha pale ninaposoma makala zangu au makala iliyoandaliwa na mtu yoyote, awe ni rafiki au mtu yoyote yule.

Kuna maandiko yanayotoka kichwani na yanayotoka moyoni. Maandiko yote haya yana umuhimu sana. Kwa maandiko yanayotoka moyoni mwa mwandishi haya huingia moyoni mwa msomaji, na kwa maandiko yanayotoka kichwani nayo pia huingia kichwani kwa msomaji. Kwa maandiko yanayotoka mdomoni mwa mwandishi bila kuchanganywa na hisia ama akili za mwandishi, haya huishia machoni ama masikioni mwa msomaji au msikilizaji. Hivyo sababu kubwa ya kuandika ni hisia toka moyoni zikichanganyika na akili za kichwani zinazonisaidia kupanga mfuatano visa na maneno yatakayotumika ili wasomaji waweze kunielewa na hata kupata hisia ya nilichokiandika.

Kwa maisha yalivyo kuna vitu vingi sana vya kuandika ili kuwajuza wasomaji, na pia kutumia ulichonacho ama unachokifahamu. Unaeza kuwa na makala hata mia moja zinazongumzia kitu kimoja lakini katika nyanja mbalimbali. Unaweza ukawa una sauti kubwa kusikika ila sauti yako ikashindwa kuwafikia walengwa. Unapoongea waliokuwepe ndio watakao kusikia ila hawatafikisha ujumbe wako kama ulivyo, wapo watakao ongeza na watakao punguza baadhi ya maneno ambapo hupelekea kupoteza utamu na uhalisia wa ujumbe wako. Lakini unapoandika, kwanza ujumbe halisi humfikia mlengwa, pia maandiko haya yatakaa na kudumu muda mrefu katika kumbukumbu.

Kwa sababu napenda kusoma zaidi ya ninavyofundishwa. Maisha ni kujifunza na katika kujifunza kuna baadhi ya vitu huwa tunavigundua katika maandishi ya waandishi. Mwandishi mzuri ni yule anayetumia muda wake kusoma maandishi ya waandishi wengine. Hauwezi kwenda benki ukatoa fedha ambazo haujaziweka,na hauwezi kutoa kiasi kikubwa zaidi ya ulichokiweka. Basi utakubaliana nami kuwa huwa tunatoa tulivyoweka.

Siridhishwi na mwenendo wa mambo unavyoenda, hivyo pale ninapoandika kuhusu jambo ambalo haliniridhi huwa najisikia huru kwani nimeongea na fikra zangu na moyo wangu kwa maandishi. Ukiangalia makala zangu nyingi nimendika kuhusu matatizo ya jamii zetu. Hasa pale mambo yanapokwenda kombo. Hivyo pale matatizo yatakapokwisha ndipo nitaacha kuandika na matatizo huisha pale binadamu anapo ondoka katika dunia hii.

Napenda kuwashauri marafiki, ndugu, wanafunzi wenzangu, walimu, wakubwa zangu hata na wadogo zangu. Andikeni, andika kitu chochote kile, utapata amani ya moyo nafsi na akili. Andika chochote unachodhani kina umuhimu na heshima mbele yako kabla hakijafika mbele za wasomaji. Andika kuhusu maisha yako katika nyanja zote.Tambua katika kila kiumbe kuna somo la kujifunza kwa aliyojifunza au kwa alivyoishi. Anza wewe kwa kutambua ya kuwa  KUMKiCHWA NI WEWE! 

No comments:

Post a Comment