Thursday, July 5, 2012

Kamchezo haka.


















Nakapenda haka kamchezo,
hakana hata maelezo,
masharti wala vigezo,

porojo tu na mizozo,
lawama ni siri ya mchezo.

Katamu haka kamchezo,
tutawazuga na tuzo,
kuficha wetu uozo,
tutawapa na pambizo,
burudani ni sehemu ya mchezo.

Unaposikia haka kamchezo,
mdomo weka likizo,
sikio lipe uwezo,
uongo nao ni chanzo,
hila ni dira ya mchezo.

Jamani haka kamchezo,
hakana hata ujazo,
thumni wala tozo,
utu kwenye mauzo,
ubaya ni mwanzo wa mchezo.

Ukitambua haka kamchezo,
tumia wako uwezo,
usizubae kama chezo,
usiponielewa anza mwanzo,
kuelewa sio dhamira ya mchezo.


 by Abeid Kajia (Kumkichwa)

No comments:

Post a Comment