Friday, July 27, 2012

Ukweli uko wapi?


              Ni miaka kumi tayari imeshapita toka nihitimu elimu ya msingi, na kwa kipindi hicho fikra zangu na za utoto wa rika langu huwa tunamini na kufuata kila tunachokisikia na kuambiwa, ila baada ya miaka hiyo kwa sasa sina tena uwezo ule, kwani maswali mengi yamekua yakiibuka kwa nia na shauku ya kutaka kujua undani wa baadhi ya vitu kama sio kila kitu. Na swali moja wapo ni "Je ukweli uko wapi?"

             Nakumbuka wakati huo wa udogo Wazazi wetu walituambia mimi na pacha wangu "Mkishindwa kufaulu kwenda kidato cha kwanza basi mjue mtakua waendesha mikokoteni”, Mzee akatuahidi kua atatupa matairi ya gari lake ya nyuma na mbele, kila mmoja mawili mimi na pacha wangu na Mama naye atatupa mbao ili tutengeneze mikokoteni kwakua tulikua hatupendi kujihusisha na elimu au tulikua hatutilii mkazo elimu kama namna tulivyokua tumewekeza muda kwenye michezo. Tuliamini kua ni kweli wangetuacha tuwe wasukuma mikokoteni na walikua wanatuadhibu kama wakitukuta hatujasoma na tumeenda kucheza mpira. Bakora zile kwa upande wangu sikuzipenda kabisa kwa wakati ule, niliona kama naonewa ila kwa sasa kwa fikra hizi ndipo natambua umuhimu wake. Ukweli ni kwamba bakora zile zilikua ni za kutujenga na sio uonevu kama nilivyodhania mwanzoni.

             Sasa nimekua kifikra na kiakili, maarifa yameongezeka kiupeo, na uchambuzi wa mambo umekua mkubwa. Kutokana na maisha yalivyo nikajikuta najiuliza “Je Ukweli uko wapi?”

             Kwa ninavyofahamu Muda ni kitu muhimu sana, ambacho ukiwekeza kwa umakini basi faida yake itakua nzuri sana. Sasa kama ukweli ndio huu Je! ni kweli muda wetu tunauwekeza kwa umakini ili kupata faida ama tunategemea hasara?

             Wanasema vijana ni taifa la kesho na taifa la kesho linajengwa leo, ikimaanisha muda wa vijana wa leo umewekezwa katika kulijenga taifa la kesho lililo bora kwa kuwa hakuna anayewekeza penye hasara. Sasa ukweli upo wapi, Je! kwa hali halisi ya mambo yanavyokwenda, ni kweli vijana tumewekeza/zwa kwa ajili ya kesho ama tunatumiwa leo ili waijenge kesho yao?. Anza na wewe, jitazame wewe mwenyewe, kisha tazama kwenye mtaa wako, chambua hatua kwa hatua mpaka ufikie Vijana wa taifa zima. Kama ndio tumewekeza/zwa kwa faida yetu, huenda basi tukafaidi taifa letu la kesho, ila kama sio jiulize ukweli uko wapi?

             Tazama vijana kwenye biashara ya siasa, wanajaribu kuwekeza pasipo kujua kuwa wao ndio rasilimali ya mwanasiasa. Wanahangaika kutafuta mgodi wakati wao ndio madini.

             Chanzo ni nini? UTEGEMEZI. Tumaini la vijana lipo kwa mtu/mwanasiasa, shida za vijana ni mtaji wake, ambaye atautumia muda wao kuwakusanya ili awapumbaze kwa ahadi za mabomba ya Asali na Maziwa. Vijana hawa wataishia kupukutika na kuwa vilema kwa tip za toyo na vibajaji. Hivi hamjajua kua matatizo yetu ndio mitaji kwao. Unataka tiba, elimu, mtaji, ajira ila hautovipata bure. Unadhani watakuchapa bakora? unadhani watakutisha kua utasukuma mkokoteni? Laah.. bali watakuahidi vizuri ili ubweteke na uwe tegemezi kwao. Wakirudi wakukute pale pale na shida nyingine nyingi. Kijana amka, utawategemea mpaka lini, jaribu kusimama na miguu yako miwili, ila kabla ya hapo jiulize UKWELI UKO WAPI?.. Kumkichwa ni wewe!

No comments:

Post a Comment